LONDON, ENGLAND
MAMBO ni mazito sana Anfield na Kocha, Jurgen Klopp anakuna
kichwa kusaka dawa ya kuiangamiza Manchester United. Awali, mashabiki wa
Liverpool walikuwa wanacheeka baada ya kupata habari kuwa Man United itawakosa
Paul Pogba, Rojo, Fellaini, Michael Carrick na mpachika mabao wake hatari
Romelu Lukaku, lakini sasa mambo yamegeuka.
Taarifa mpya ni kwamba, straika matata wa Liverpool, Sadio Mane
ameumia na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja hadi Desemba hivyo, ataukosa mchezo
dhidi ya United.
Jumamosi, Liverpool itaikaribisha Man United kwenye uwanja wake
wa Anfield, mchezo ambao utakuwa mgumu kutokana na historia ya klabu hizo,
ambapo imebainika kuwa Mane amepata majeraha ya misuli.
Taarifa ambazo zimezua hofu huko Anfield ni kwamba, Mane atakosa
mechi 10 na sasa ataungana na mastaa wenzake Adam Lallana na Nathaniel Clyne
ambao pia ni majeruhi.
Pia, Mane atakosekana kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya
dhidi ya Maribor na Sevilla ambazo zinatarajiwa kuamua hatma ya kikosi cha
Klopp kwenye michuano hiyo.
Mechi nyingine muhimu ambazo Mane aliyetolewa uwanjani dakika ya
87 kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Cape Verde, atazikosa ni
dhidi ya Tottenham Hotspurs na Chelsea.
Post a Comment