NA PRIVA ABIUD
MIAKA 50 ijayo Cristiano Ronaldo na
Lionel Messi watazungumziwa kama Pele na Diego Maradona wanavyozungumza sasa. Sijawahi kuandika chochote kuhusiana na hawa watu. Leo nimeamua kuandika ila sio kama nataka kusema ni yupi bora zaidi ya mwingine.
Sasa ili nifikishe ujumbe wangu salama nianze na kusema wote ni wachezaji bora kulingana na hisia zako wewe msomaji wangu. Wewe ndiye mwamuzi wa yupi bora. Ukiwazungumzia hawa watu basi unazungumzia hisia za mashabiki wengi sana.
Sitaki kubadili hisia za mtu. Baki na unachokiamini. Leo natamani kuzungumzia majukumu ya wachezaji hawa.
Kabla sijasema hayo naomba kubeti (kuwa Ronaldo atatwaa Tuzo ya Ballon d’Or kwa mara ya nne). Mabao ya Messi na Ronaldo yanazidi mabao yote ya Manchester United katika Ligi Kuu. Inamaana hakuna klabu England yenye mabao ya hawa jamaa. Wakati nasema Ronaldo anatarajia kutwaa Ballon d’Or ya nne inamaana hawa jamaa watamiliki Ballon d’Or tisa tu hii imekuwa kama hizi tuzo sio zawadi, bali ni mali zao.
Kila mmoja ana nafasi yake! Ila ningetoa maksi kama hivi, Ningewagawa kama ifuatavyo
Mshambuliaji wa Mwisho no 9/10 Ronaldo-nampa A (mabao 538 michezo 790, Messi- pia nampa A (499 michezo 631).
Winga, Ronaldo anastahili A (ana wastani wa 2.12 katika kupiga krosi, Messi-B. (ana wastani wa 0.48).
Kiungo mchezeshaji (play maker) Ronaldo-C (asisti 180), Messi-A (asisti 201). Nimetoa C kwa Ronaldo maana hapendelei sana kucheza kama kiungo.
Messi
Kiungo wa kati, Ronaldo-C (wastani
wa pasi 70%), Messi-B (wastani wa pasi 82.5%) hii ni kutokana na mifumo ya timu
zao. Kwenye suala la kukaba wote sifuri tu. Tukiachana na hayo kwa msimu huu, Messi ameonekana kuelemewa! Ametolewa kwenye namba yake na kupewa jukumu la Ronaldo wa Manchester United kwa kucheza winga wa kushoto. Pep Guardiola alipofika Barcelona alimweka Messi kama false 9 (namba 9 hewa) na hii ndiyo iliyomyosababishia Messi kufikisha mpaka mabao 90 kwa msimu. Tangu mwaka 2007 hadi 2009, Ronaldo alicheza nyuma ya kina Carlos Tevez, Dimitar Bebertov akisaidiwa na Wayne Rooney akicheza winga ya kulia na kushoto chini kocha Sir Alex Ferguson ambaye alimshauri ili aweze kupambana na Messi, basi acheze kama Messi yaani atokee pembeni aende mbele (no 9/10). Msimu huu Messi ametolewa kwenye boksi anacheza nyuma ya Luis Suarez na Neymar akisaidiwa na Andrés Iniesta na Sergio Busquets ambao wamepaka nywele zao piko wakitudanganya kwamba hawana mvi. Hii imemfanye Messi abebe jukumu zito ambalo litamweka katika wakati mgumu kupambana na Ronaldo.
Hii imeonekana wazi kwa namna anavyoteseka kuitafutia timu matokeo badala ya kupigania rekodi zake binafsi.
Ukiachana na takwimu hizo hapo juu, Namwamini zaidi Ronaldo katika kufunga kwa utaalamu wake wa kupiga mashuti yenye nguvu na kasi na hasa yenye ufundi wa hali ya juu.
Lakini Messi amejaliwa sumaku mguuni, ana uwezo wa kukaa na mpira kwenye kikundi cha watu kadhaa na asiupoteze. Kitu kingine ambacho Ronaldo anachojivunia ni umbo lake, hasa kwenye mipira ya hewan.
Messi naye anatumia umbo lake fupi hasa katika fiziki na kasi, hivyo inakuwa tabu kumwangusha kirahisi, achana na vimpira vya kuchopu, Ronaldo amekuwa mchezaji anayejua kununua viwanja, naamanisha anakuwa kwenye eneo husika hasa wakati wa kufunga (kuji-position).
Ronaldo anaweza akawa anafunga mabao mengi zaidi kwenye boksi, faulo na penalti ukilinganisha na Kirikuu (Messi) ambaye vigoli vyake vingi vya ajabu ajabu (vichopu).
Hii inaonesha ni kwa jinsi gani anavyojua kulenga nyavu kuliko kitu kingine, yaani mawazo ya Ronaldo ni kwenye goli tu, hajui kama anacheza na wenzie, yeye mletee kwenye boksi watajuana na kipa mbele ya safari.
Messi amejijenga zaidi kitimu ukilinganisha na mwenzake, Madrid imejijenga zaidi kumtegemea zaidi Ronaldo na inategemea zaidi uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, hii ina maana Busquet au Rakitic Ivan Rakitić wakienda Madrid hawawezi kupata namba.
Mabao ya Messi mengi yanavutia kutokana na staili ya uchezaji wa Barcelona pamoja na uwezo wake binafsi. Itapita miaka 10 au zaidi mataifa ya Ulaya kumpata mtu zaidi ya Ronaldo, lakini inaweza ikapita hata miaka 50 mpaka karne duniani kumpata mtu anayecheza kama Messi (Maradona) ni kiumbe kilicho mbioni kupotea duniani.
Messi na Ronaldo
Ni lazima dunia ikubali kwamba
Ronaldo anasifika zaidi kwenye uwezo wake mkubwa wa kufunga, lakini Messi anaacha
watu mdomo wazi kwa staili yake ya uchezaji. Wengi wanaotazama mpira kwenye Tv wanawalaumu sana mabeki kwa nini wanashindwa kumkaba Messi? Lakini kwa namna Ronaldo anavyofunga huwezi kumlaumu mtu maana anafunga ma bao ya jitihada binafsi au niseme jitihada za kibinadamu lakini Kirikuu haijajulikana bado dawa yake ni nini.
Philippe Mexès alisema kumkaba Ronaldo unahitaji kumchezea rafu nyingi na vurugu kibao ili kumkatisha tamaa lakin kumkaba Messi inahitajika sala.
Huwa nina swali ambalo wengi wanalikwepa, kwa mfano tuondoe mabao waliyofunga, na tutupilie mbali Ballon d’Or zao, ukiulizwa hebu wasifie Messi na Ronaldo kila mmoja utamweleza vipi na utampa sifa gani?
Hapa ndipo ubishi unakuja. Watu wa Messi wanajivunia uwezo wake wa kuutumia mpira ila wa Ronaldo wanajivunia uwezo wake wa kufunga.
Sawa Messi anafunga pia sawa na Ronaldo naye ana uwezo, lakini takwimu za Ronaldo katika Ligi ya La Liga zinatisha kidogo. Kama unahitaji No 9 duniani Ronaldo ni chaguo sahihi. Ila kama unataka No 10 Messi pekee yake ndoye anayestahili.
Kuna wale wanaopiga kelele kwamba Messi amekutwa La Liga na Ronaldo. Hicho sio kigezo cha kusema ni yupi bora maana ni kama wote wapo sawa tu.
Sasa iko hivi. Tangu wameanza wote La Liga 2009, Messi michezo 233 mabao 254 asisti 95, Ronaldo michezo 232 mabao 255 asisti 75 hizi ni takwimu za La Liga tu lakini kwa takwimu zote kwa jumla tangu Ronaldo ametua Madrid ni Ronaldo mabao 359 michezo 342 asisti 99, Messi 363 mabao 369 asisti 134.
Hizi takwimu ni za Aprili 13. Hivyo Ronaldo amezidiwa bao moja tu na Messi. Ndo maana nasema tofauti yao ni ndogo kama mshahara wa mgambo. Mmoja ni Dj mwingine ni mkata mauno. Wote wanaburudisha jukwaani. Suala la ni yupi bora ni hisia zako. Zangu zipo wazi kwamba ukinuliza namtaka yupi aje kunisalimia n’tasema Ronaldo maana hana nyodo tutapiga stori lakini ukinuliza nani aende Manchester United sasa n’tasema nini zaidi ya kumchagua Kirikuu? Kinachoniumiza ni kwamba neema hii niliyojaliwa na Mungu ya kuona viumbe bora duniani inafikia ukingoni.
Misimu ya nyuma mpaka sasa Ronaldo alikuwa na mabao 54, Messi 54 lakini sasa hivi hata Granada hawazifungi. Umri unawakimbilia. Akili inaniambia wanakuja kina Paulo Dybala, Neymar, na Pierre-Emerick Aubameyang, achana na koke, Antoine Griezmann, Anton Martial na Costa Douglas kuna mtoto anaitwa Gabriel Jesus Mungu atujalie maisha marefu nikione hiki kiumbe Ulaya.
Post a Comment