0


               IMEANDIKWA NA PRIVA ABIUD
WAKATI Man United ikiumana na Celta Vigo na Midjytland kuna kijana mmoja mweusi alikuwa amekamata dimba la kati kwa jina anaitwa Pione Sisto.
Huyu kijana alionekana kung’ara alipokuwa Midjytlan na hata kwenye mchezo wa majuzi akiwa na Celta -Vigo, huyu nitamuongelea baadaye ngoja niwazunguzmie kaka zake kwanza.
Wakati nazaliwa mwaka 1992 kikosi cha Kocha Richard Moller Nielsen kiliishangaza dunia, kwa kuichabanga Ujerumani waliokuwa mabingwa wa Kombe la Dunia kwenye michuano ya Euro.

Pione Sisto
Kichapo kile cha Denmark ilichokitoa kilimfanya nguli wa nchi hiyo, Michael Laudrup kustaafu soka. Denmark ilikuwa ikiongozwa na mlinda mlango anayeaminika kuwa bora kuwahi kutokea, Peter Schmeichel.
Hicho ndicho kilikuwa kizazi bora kwa Denmark kwa wakati ule na katika historia ya nchi hiyo. Katika historia ya taifa lile hatuwezi kuacha kumzungumzia Brian Laudrup ambaye amewahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Denmark kwa mara nne na pia aliwahi kutajwa na Fifa mwaka 1992 kuwa mchezaji wa tano kwa ubora duniani kwa mwaka ule.
Ni mchezaji ambaye mchawi wa soka, Pele alimtaja katika orodha yake kuwa ni mmoja kati ya wachezaji bora duniani kuwahi kutokea akimweka nafasi ya 125. Michael Laudrup ni kaka yake na Brian Laudrup ni mmoja kati ya wachezaji bora kukumbukwa katika ardhi ya Denmark akikukumbukwa kwa mafanikio yake aliyopata ndani ya Barcelona, Ajax, Real Madrid na Juventus.

Michael na Brian Laudrup
Ni mmoja kati ya viungo waliong’ara kipindi cha Johan Cruyff alipokuwa kocha mkuu wa Barcelona, walipotwaa mataji tisa. Mwaka 1999 alitajwa kuwa mchezaji bora wa kigeni wa Ligi Kuu Hispania, La Liga kwa kipindi cha miaka 25. Mwaka 2006 alitajwa na chama cha soka cha nchini humo kuwa mchezaji bora wa muda wote kutoka Denmark.
Wakati Laudrup mkubwa akitajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea katika nchi za Scandinavia (Sweden, Norway, Denmark n.k) akimpiku mtu kama Zlatan Ibrahmovic pia ni mmoja kati ya wachezaji waliochezea mahasimu wawili Barcelona na Real Madrid na kupata mafanikio katika vipindi vyote.
Anatajwa pia kuwa kati ya wachezaji 11 bora wa kigeni katika historia ya Real Madrid. Kizazi cha kina Laudrup kimeshaondoka Denmark. Kimekuja kizazi kingine kabisa. Kizazi hiki kilianza mizizi yake kwenye michuano ya Uefa ya wachezaji wenye chini ya umri wa miaka 21 mwaka 2014. Kikosi kile kilicheza michuano yote ya kufuzu michuano ile bila kufungwa hata mchezo mmoja kwa kushinda michezo minane na kutoa sare miwili.

Hojbjerg
Katika kikosi kile kilikuwa na kijana mmoja anayeitwa Pierre Emile Hojbjeng ambaye akiwa na miaka 14 tayari Wadenmark washamwita Zinadine Zidane wao. Akiwa na miaka 17 alisajiliwa Buyern Munich. Mwandishi maarufu kwa jina la Jonathan Fadugba mwaka 2016 alisema kuwa kijana huyu aliyeanzia maisha FC Copenhagen ambaye kwa sasa anakipiga Southampton anaweza akawa na balaa kuliko staa wa taifa hilo kwa sasa Christian Eriksen anayekipiga Tottenham Hotspur.
Kijana huyu akiwa na miaka 17 na siku 251, aliweka rekodi ya mchezaji mdogo kuwahi kucheza kwenye mchezo wa mashindano ndani ya klabu ya Bayern Munich mwaka 2013. Mbali na baba yake kukutwa na matatizo ya kansa Kocha Mkuu wa Bayern Munich, Pep Guardiola alimsaidia baba yake na Hojbjerg kuhakikisha anapata matatibu. Hojbjerg anasema siku ya kwanza Pep kukutana na baba yake, Pep alitoa machozi kutokana na hali ile. Tukiachana na huyo kuna fundi mwingine aliyemtoa kijasho Jose Mourinho. Anajulikana kama Pione Sisto. Mashabiki wa Man United watamkumbuka vizuri kwenye mchezo wao dhidi ya CeltaVigo.
Ni kiungo wa katikati hivi, mweusi, anakata mbuga kama N’golo Kante vile. Huenda Wadernmark wasimsahau Michael Laudrup lakini huyu naye atakuwa mmoja kati ya lulu walizobarikiwa kwa miaka ya hivi karibuni ukiachana na Christian Ericksen. Akiwa na miaka 18 alikipiga katika klabu ya Midjylland na alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka akiwa na miaka 18 tu. Aliifungia klabu yake mabao 20 katika michezo 90, kwa idadi hiyo huku akiwa kiungo wa kati tu,  Barcelona Juventus Milan na Porto zilimmendea kwa miaka kadhaa kabla ya Arsene Wenger naye kupeleka ofa yake.
Wakati Manchester United ilipofungwa na Midjytlland mabao 2-1 yeye alifunga bao moja na alikuwa balaa mbele ya mabeki wa United.

Christian Ericksen
Pia, kuna kijana mwingine anayeitwa Andreas Christensen, nadhani mashabiki wa Chelsea wanaweza kumwelezea vizuri maana alijunga na academy ya klabu hiyo akitokea kwenye klabu ya kwao iitwayo Brondby. Cheslea alicheza mchezo mmoja tu kabla ya kuelekea Ujerumani. Kocha Antonie Conte alitaka kumrudisha kikosini Januari mwaka huu. Amekuwa ndio kiongozi wa Borussia Monchengladbach akiwa na wastani wa 4.5 kati ya 5, akiwa amejikusanyia alama 624 kutokana na kituo maarufu cha kutoa takwimu za wachezaji kijulikanacho kama Squawka. Kwa msimu huu amezuia mipira ya juu kwa asilimia 64, amekuwa na wastani mzuri wa pasi kwa asilimia 90 amemzidi hata Paul Pogba.
Ana uwezo mkubwa wa kuzuia mipira, umakini katika kupiga pasi na utulivu wa kipekee uwanjani, yaani ni kama Michael Laudrup amerudi tena uwanjani.
Ajax nao wana Mdenmark mmoja anajulikana kama Kasper Dolberg ukimwona akiwa amevaa jezi ya Ajax unaweza ukadhani yule dogo ni Mholanzi lakini sio. Aliyeibua kipaji cha kijana huyu ni yuleyule skauti aliyewaleta Zlatan, Ericken, na Fischer sokoni. Msimu huu ndani ya Ajax ana mabao 18 na ametengeneza mengine sita katika michezo 38
                                          Kasper Dolberg

Kwa takwimu hizo huyu naye ana balaa na ndo kwanza ana miaka 18. Huu ndio kwanza msimu wake wa kwanza katika kikosi cha kwanza ndani ya Ajax na tayari amefanya balaa.
Kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Ajax ndio nilianza kumwelewa kijana huyu baada ya kuipatia klabu yake bao la pili dhidi ya Olympic Lyon.
Ndani ya Ligi kuu uholanzi tayari ameshafunga mabao 15 latika michezo 25 huku michuano ya Ulaya akiwa na mabao matatu katika michezo sita huku michuano ya Uefa akiwa na bao moja katika mchezo mmoja tu. Mpaka kufikia sasa yeye ndiye mchezaji bora ndani ya Ligi Kuu ya Uholanzi akiwa na wastani wa 3.5 (Squawka).
Nataka pia nikumegee tena na mtoto mmoja mchafu sana anajulikana kama Jens Odegaard, achana na Martin Odergaad yule wa Real Madrid, huyu ana miaka17 tu, na kwenye michuano ya Uefa ya miaka 17 tayari ameshakuwa gumzo huko. Wadernmark wanamwita Marco Van Bastern wao, ni mshambuliaji wa mwisho.

Kasper Schmeichel
Wapo wachezaji wengi kama kipa wao, Kasper Schmeichel anayekipiga Leicester City, pia yupo Ericksen anayekipiga Tottenham. Pia, yupo kiungo wa zaman wa Ajax ajulikanae kama Viktor Fischer mwenye umri wa miaka 22 ambaye aliichezea Ajax michezo 80 na kufunga mabao 25 huku akiwa na mabao matatu timu ya taifa kwenye michezo13 alitajwa kuwa mchezaji chipukizi mara mbili akiwa Denmark na baadaye akiwa Ajax. Pia, akiwa kwenye michuano ya wachezaji wa chini ya miaka17 aliweza kuifungia timu yake ya taifa mabao 20 katika michezo 30 na kufikisha nusu fainali ya kombe hilo kabla ya kufungwa na Ujerumani.
Babu yake Fischer pia alikuwa mcheza soka wa zaman wa taifa hilo, Poul Pedersen ambaye alikuwa akisakata kabumbu kama winga teleza miaka hiyo.
 Nini hasa lengo langu kuwazungumzia hawa,? Kwanza ukiangalia Taifa la Ubelgiji lilikuja kwenye raman za soka baada ya wachezaji wake wadogo kutambulishwa katika ligi kubwa barani Ulaya huku pia wakiwa wachezaji tegemezi ndani ya klabu hizo. Kwa kuangalia namna Ubelgiji walivyovuma, ni kama nao Denmark wanapitia njia ileile. Kwa mfano ukiangalia vijana hao wote, wapo chini ya miaka 23, maana yake miaka sita ijayo Denmark itakuwa na vijana zaidi ya wanane ambao tayari ni wachezaji wakubwa na tegemezi katika kikosi chao.

Sisto Pione
Vijana hao wameshaonesha viwango vikubwa kiasi kwamba tayari ni chachu kwa vijana wengine walibakia. Sisto Pione ambaye ni mzaliwa wa Uganda tayari ameshaonesha kiwango cha aina yake. Sisto ameikataa Uganda na kuitumikia Denmark kwa sababu tayari ameshauona mwanga mbele yake.
Tayari academy za Lyseng IF, academy ya Lyngby BK, Aalborg bila kusahau academy ya Midjytlland ambayo imekuwa gumzo kwa sasa zitapata mwamko wa kuzidi kuendelea kuinua vipaji zaidi.
 Natoa angalizo ni mapema sana kufananisha kizazi hiki na kile cha mwaka 1992 kwa upande wa mafanikio lakini tayari wameshaonesha cheche.

Post a Comment

 
Top