0


                      LISBON, URENO
SUPASTAA Cristiano Ronaldo amethibitisha amekuwa baba wa watoto pacha na atakwenda kusherehekea kuzaliwa kwao baada ya yeye na timu yake ya Ureno kutupwa nje kwenye nusu fainali ya Kombe la Mabara na Chile kwa mikwaju ya penalti 3-0.
Baada ya kipigo hicho cha juzi Jumatano usiku, Ronaldo aliruhusiwa na mabosi wake wa Timu ya Taifa ya Ureno kwenda kufurahia tukio hilo la kupata watoto wengine wawili wa kwa njia ya kupandikiza.
Mtoto wa kwanza wa Ronaldo, Cristiano Ronaldo Jr mwenye umri wa miaka saba, naye alipatikana kwa njia hiyohiyo kama hii iliyotumika kwa pacha hao.
Mwanzoni mwa mwezi huu, ripoti za kutoka Ureno zilithibitisha taarifa iliyotolewa na Gazeti la The Sun, supastaa Ronaldo anajiandaa kupata watoto pacha kutoka kwa mama aliyefahamika na sasa Ronaldo mwenyewe amethibitisha hilo.
Ronaldo aliandika hivi kwenye ukurasa wake wa Facebook: “Nilikuwa kwenye timu ya taifa, nikijitolea kwa kila kitu kama ilivyozoeleka kila siku, licha ya kutambua watoto wangu wamezaliwa.
“Kwa bahati mbaya tumeshindwa kufikia lengo letu kwenye michezo, lakini naamini tutaendelea kuwapa furaha watu wa Ureno. Rais wa shirikisho la soka Ureno na kocha wa timu ya taifa wote waliona umuhimu wa jambo langu kitu ambacho siwezi kukisahau. Nina furaha kwa sababu hatimaye sasa nitakuwa na wanangu kwa mara ya kwanza.”
Taarifa rasmi ilibainisha: “Rais wa Shirikisho la Ureno na kocha wa timu ya taifa walikuwa na taarifa kabla hata ya Kombe la Mabara nahodha Cristiano Ronaldo amekuwa baba wa watoto wengine.

                   Ronaldo na mchumba wake wa sasa.
“Mchezaji mwenyewe, licha ya kufahamu watoto wake wamezaliwa bado aliamua kubaki kwenye timu yake ya taifa na hivyo baada ya timu kutolewa, alipewa ruhusa ya kwenda kuwaona watoto wake hao.”
Kituo kimoja cha televisheni huko Ureno, SIC kiliripoti pacha hao wa kiume na kike, ambao majina yao ni Mateo na Eva walizaliwa na mwanamke aliyefahamika wa kutoka Pwani ya Magharibi mwa Amerika kwa kupitia upandikizaji wa mbegu za kiume.
Mastaa wengine, akiwamo Mwanamitindo, Tyra Banks nyota wa luninga, Jimmy Fallon na Mwigizaji, Sarah Jessica Parker ni miongoni tu mwa watu maarufu wenye watoto wa kupandikiza. Kitaalamu mama anayetumika kuzaa watoto wa aina hiyo anaitwa surrogate.

SURROGATE NI NANI

Ronaldo na mwanaye wa kwanza.
Surrogate ni mwanamke anayebeba uja uzito na kujifungua watoto kwa ajili ya mtu mwingine. Huu ni mtindo ambao umekuwa ukitumiwa na wale watu ambao hawezi kuzaa watoto wenyewe. Kwa mujibu wa taasis inayojihusisha na mambo hayo, COTS, imesema kuna aina mbili za mtindo huo, ambao wa kwanza ni ule wa kienyezi ambapo mbegu za baba husika wa watoto zinapandikizwa moja kwa moja kwa mwanamke anayepaswa kubeba huo ujauzito na njia nyingine ni ile ya kuchukua vinasaba tu vya wazazi wawili na kisha vinakwenda kupandikizwa kwenye mwanamke mwingine ambaye atazaa watoto kwa ajili yao.

                   
                   WATOTO WANNE WA RONALDO
Baada ya kupokea pacha hao, si muda mrefu, Ronaldo atakuwa na watoto wanne baada ya huyo mpenzi wake wa sasa kuripotiwa kuwa na ujauzito. Ronaldo, ambaye sasa watoto wake watatu, Cristianinho, Mateo na Eva wataungana na mwenzao, mwingine ambaye bado hajafahamika watakuwa na jinsi gani kufuatia mrembo Georgina Rodriguez, anayetoka na staa huyo kwa sasa kuwa mimba ya miezi mitano. Hivi karibuni, Ronaldo alionekana akishikashika kitumbo cha mrembo huyo kuashiria kuna kitu kinatarajiwa kutoka kwa Georgina.
Mmoja wa pacha wa Ronaldo anaitwa Mateo, jambo hilo litamfanya kuwa na mtoto anayefanana jina na wa mpinzani wake wa uwanjani, Lionel Messi, ambaye pia ana watoto wawili wa kiume, Thiago na Mateo.

Post a Comment

 
Top