SYDNEY, AUSTRALIA
MESUT OZIL angalau ameweza kuwashusha
presha mashabiki na Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger baada ya kutoa msimamo wake
kuhusu klabu hiyo.
“Sijui kuhusu Sanchez, lakini
mimi nabaki. Hicho ndicho alichokisema staa huyo wa kimataifa wa Ujerumani
akiwaambia mashabiki wa Arsenal.
Ozil yupo katika mgogoro mkubwa
wa mkataba klabuni hapo wakati huu mkataba wake ukiwa umebakiza miezi 12 tu na
anataka alipwe kiasi cha Pauni 350,000 kwa wiki katika mkataba mpya kwa ajili
ya kubakia Emirates kwa miaka mingine.
Kiungo huyo aliyenunuliwa na
Arsenal kwa dau la Pauni 42 milioni Agosti 2013, amedai chaguo lake la kwanza ni kubaki Arsenal
na atazungumza nayo juu ya mkataba mpya mara tu timu hiyo itakaporejea London
kutoka Australia.
“Ni wazi chaguo langu la kwanza
ni kubaki. Ni klabu kubwa na siku zote nimesema najisikia vizuri kuwa Arsenal. Tutakaporejea London
tutakaa chini na kujadili kuhusu hatma yangu ya baadaye,” alisema Ozil.
Ozil
“Kwa sasa kitu muhimu ni maandalizi
ya msimu mpya na kufanya ziara hii kwa ajili ya mazoezi na kujiweka fiti.
Nitakaporudi London tutakaa na kuzungumza kuhusu mkataba mpya.”
...akizungumza na Wenger
Sakata lake linakwenda sambamba
na la Sanchez ambaye naye amebakiza miezi 12 katika mkataba wake wa sasa na
amekuwa akihusishwa kuondoka Arsenal na kutua Manchester City katika dirisha
hili la uhamisho.
Hata hivyo, Ozil amedai hajui
lolote kuhusu hatima ya baadaye ya Sanchez na amekiri hakufanya mawasiliano na
nyota huyo wa Chile wakati wa likizo.
“Nilikuwa likizo na
sikumfikiria mtu mwingine yeyote. Nilijaribu kutuliza akili yangu mwenyewe na
kuachana na mambo mengine. Ni wazi Sanchez inabidi afikirie kuhusu hali yake ya
baadaye na maamuzi yatakuwa yake. Ni kitu ambacho kila mtu itabidi akiheshimu,”
alisema Ozil.
Hata hivyo, Ozil amekiri litakuwa
pengo kubwa kwa Arsenal kama nyota huyo aliyekuwa mmoja kati ya wafungaji bora
wa msimu uliopita, ataamua kuondoka klabuni hapo katika dirisha hili na kwa
kiasi kikubwa atashusha matumaini ya ubingwa.
...akishangilia bao na Sanchez
“Litakuwa pigo kubwa kwa timu
kama akiondoka kwa sababu siku zote ni mchezaji ambaye anafanya mambo makubwa
uwanjani. Itakuwa pigo katika mbio za kuwania ubingwa, lakini hata hivyo mwisho
wa siku ni maamuzi ya mchezaji mwenyewe,” alisema.
Endapo Sanchez ataondoka
mashabiki wa Arsenal watakuwa wamepozwa makali hayo na jinsi ambavyo kocha wao,
Arsene Wenger, amekuwa bize katika dirisha hili la uhamisho na tayari amevunja
rekodi ya uhamisho kwa kumchukua mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa,
Alexandre Lacazette kutoka Lyon.
Wenger pia ana uhakika wa
kumnasa winga wa Monaco, Thomas Lemar, pindi atakapotoa ofa yake ya tatu ya Pauni
45 milioni kwa staa huyo wa Ufaransa wakati huu ambapo ofa zake mbili za awali zimekataliwa.
Ozil
Wenger anamtaka Lemar kabla ya
pambano la Ngao ya Hisani dhidi ya Chelsea Agosti 6 mwaka huu huku siku chache
baadaye wakicheza na Leicester City katika pambano la ufunguzi wa Ligi Kuu
England usiku wa Agosti 11.
Arsenal ipo Australia na Alhamisi
ilikipiga na Sydney FC na itarudi tena uwanjani wikiendi hii kukipiga na Western
Sydney Wanderers.
Baada ya hapo itaelekea China
kucheza mechi nyingine za kirafiki kabla ya kurudi London kucheza mechi za
michuano yao ya Emirates Cup.
Post a Comment