0



                           TOCOPILLA, CHILE
ALEXIS SANCHEZ (pichani chini) ameongeza presha kwa mashabiki na bosi wa Arsenal, Arsene Wenger baada ya kudai msimu ujao anataka kuichezea timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. 
Straika huyo wa kimataifa wa Chile amedai ndoto yake ni kuchezea Ligi ya Mabingwa Ulaya, kitu ambacho hawezi kukifanya akiwa na Arsenal ambayo msimu ulioisha imetupwa nje ya nne bora.
Arsenal itashiriki Europa League na kauli hiyo inatoa ishara kwa Manchester City ambayo inashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na ilishaonyesha nia ya kumtwaa nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 ina nafasi ya kufanya hivyo.
Akizungumza kwa lugha yake ya asili ya Chile, Sanchez alisema: “Uamuzi sio wa kwangu tu, lakini binafsi tayari nimeshaamua. Sasa nasubiri jibu kutoka Arsenal wananiambie wanachohitaji.”
Alipoulizwa ni kitu gani anachohitaji, Sanchez aliongeza: “Kucheza Ligi ya Mabingwa na kushinda. Ni ndoto niliyokuwa nayo tangu utotoni.
'Kwa sasa niko Arsenal, mkataba wangu unaisha mwaka ujao.” 

Ijumaa usiku, Kocha Wenger alimtumia ujumbe Sanchez kumshawishi kubaki Arsenal.
“Bila shaka”, Kocha Wenger alisema pindi alipoulizwa kama Sanchez atabaki kuwa mchezaji wa Arsenal.
“Hakuna matatizo juu yake. Nilizungumza naye kupitia ujumbe mfupi na hakukuwa na shida.  Mtazamo wangu siku zote ni chanya juu yake.”
Mapema wiki hii, kocha huyo Mfaransa alikanusha taarifa za nyota huyo kuomba kuondoka Arsenal.
Ofa mpya ya mshahara wa Arsenal ni pungufu ya Pauni 300,000 kwa wiki thamani ambazo Sanchez anazitaka, pamoja ya kuwapo kwa ongezeko la bonasi la asilimia 20 kama Arsenal itafuzu kwa Ligi ya Mabingwa katika msimu mpya.

Post a Comment

 
Top