0


                         LONDON, ENGLAND
ARSENAL imeangalia kisha ikagundua kumbakisha Alexis Sanchez anayetaka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao inaweza kuwa kazi kubwa unajua imeamuaje? Imeiambia Manchester City: “Tupeni Sergio Kun Aguero (pichani chini) ili tuwape Sanchez mnayemtaka."
Lakini kwa kwa mujibu wa taarifa za ndani Chelsea imeamua kuingia kwa nguvu zote na kumtaka nyota huyo wa kimataifa wa Argentina.
Mabingwa hao wa England lazima wasajili straika katika usajili huu wa majira ya joto kuziba pengo la Diego Costa, ambaye ameambiwa hayupo katika mipango ya Kocha Antonio Conte msimu ujao.
Baada ya kumkosa Romelu Lukaku aliyetua Manchester United, Chelsea Imeonyesha nia ya kuwataka mastraika Alvaro Morata (Real Madrid), Pierre-Emerick Aubameyang (Borussia Dortmund), Andrea Belotti (Torino) na sasa Aguero.
Lakini watetezi wa Ligi Kuu watakuwa na wakati mgumu kumpata Aguero kwa sababu Manchester City inasita kumuachia.
Tangu klabu hiyo iliponunuliwa na Abu Dhabi United Group mwaka 2008, haijawahi kumwachia mchezaji ambaye bado inamhitaji.

Mwezi Mei, Mwenyekiti wa Manchester City, Khaldoon Al Mubaraak alipoulizwa kama Aguero atabaki klabuni hapo alisema: " Bila ya shaka. Hakuna wasiwasi juu ya hilo. Nimesoma uvumi mwingi juu ya hilo na huo ni upuuzi tu.
"Sergio Aguero ni mmoja kati ya wachezaji bora duniani. Siye ni timu yenye ushindani ambayo tunatamani kushinda kila shindano. Kuwa na Sergio Aguero kama sehemu ya kikosi bila shaka ni lazima. Jambo hilo halijawahi kutiliwa wasiwasi."
Aguero, ambaye alikuwa mfungaji bora wa Man City baada ya kupachika mabao 20 msimu uliosha wa Ligi Kuu, alikuwa katika wakati mgumu baada ya ujio wa Mbrazili, Gabriel Jesus ndani ya kikosi hicho­­.
Pia Kocha wa Machester City, Pep Guardiola pia alisisitiza straika huyo hatauzwa msimu huu.
"Kila mkutano na waandishi wa habari (swali hili limekuwa likiulizwa)," alisema. "Sawa, jamani. Atabaki (ManCity) msimu ujao. Mmefurahi?" alisema Guardiola.
Aguero alisajiliwa kutoka Atletico Madrid kwa Pauni 38 milioni mwaka 2011 na amebakisha miaka mitatu katika dili lake na Man City. Ameifungia timu hiyo ya Etihad mabao 169 ndani ya miaka sita, ameshinda mataji mawili ya Ligi Kuu England mwaka 2012 na 2014.

Post a Comment

 
Top