0
                                LONDON, ENGLAND
ANTONIO CONTE ameongeza mkataba Chelsea baada ya kusaini dili la miaka miwili lenye thamani ya Pauni 20 milioni.  Awali Conte alihusishwa na tetesi za kurejea Italia katika msimu huu wa majira ya joto, lakini sasa amemaliza tetesi hizo. Katika msimu wake wa kwanza kocha huyo aliipa Stamford Bridge taji la Ligi Kuu.
Conte alisema: “Nina furaha sana kusajili mtakaba mpya na Chelsea. Tulifanya kazi ngumu katika mwaka wa kwanza na kufanikiwa kupata kitu cha kushangaza, ambacho najivunia sana. Sasa tunatakiwa kufanya kazi ngumu zaidi kuendelea kukaa kileleni.
“Mashabiki wa Chelsea wamenisapoti vya kutosha tangu nilipowasili hapa mwaka mmoja uliopita na ni muhimu tutaendelea kufanikiwa pamoja.”
Kocha Conte na kikosi chake wataanza ziara barani Asia kwa ajili ya maandalizi ya msimu wiki hii ambako huko watacheza dhidi ya Arsenal, Bayern Munich na Inter Milan.
Bosi huyo wa zamani wa Juventus amekuwa kipenzi cha mashabiki Stamford Bridge kutokana na uwepo wake katika benchi la ufundi.
Pia, Conte amepata wasaidizi wawili wapya katika majira haya ya joto, Paolo Vanoli atakakuwa kocha msaidizi na Davide Mazzotta aliyepewa jukumu la uchambuzi.

Mkurugenzi wa Chelsea, Marina Granovskaia alisema: “Antonio (Conte) amepata mafanikio makubwa msimu ulioisha, ameweza kwenda na mazingira ya soka la Kiingereza kwa haraka na kutwaa taji la Ligi Kuu.
“Mkataba huu mpya unaonesha imani yetu kwake kwamba anaweza kuendelea kutupa ya Ligi Kuu na kutoa ushindani katika mashindano ya Ulaya.”

Mapema kocha huyo wa Chelsea aliripotiwa kutokuwa na furaha kutokana na mwenendo wa usajili ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo, mpaka sasa Chelsea imesajili wachezaji watatu nyota wa Monaco, Tiemoue Bakayoko na Antonio Rudiger kutoka Roma. Kipa wa zamani wa Man City, Willy Caballero pia amesajiliwa na kikosi hicho kinachojipanga kutetea taji lake.

Kabla ya kuanza mbio za Ligi Kuu, Chelsea itacheza mchezo wa Ngao ya Hisani Agosti 6, dhidi ya Arsenal uwanjani Wembley. Timu hiyo imerejea Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuikosa msimu uliopita.


Post a Comment

 
Top