0
                             MANCHESTER, ENGLAND
ILIKUWA hadithi fupi ya kusisimua, lakini mwisho wake umefika mapema sana. Ndoa ya Manchester United na staa wake wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic jana ilitazamiwa kupata talaka yake baada ya United kuamua kutoendelea naye.
Ijumaa ilikuwa siku ya mwisho kwa klabu kutangaza wachezaji ambao, haitaendelea nao msimu ujao na Manchester United ilitazamiwa kuliweka juu jina la staa huyo, ambaye ilimsaini kwa mkataba wa mwaka mmoja msimu uliopita.
United imeamua kuachana na Zlatan baada ya kugundua kuwa staa huyo mwenye umri wa miaka 35 hatakuwa fiti mpaka mwakani baada ya kuumia vibaya goti lake katika pambano la michuano ya Europa dhidi ya Anderlecht msimu ulioisha.
Hata hivyo, Man United inataka kuachana kwa amani na staa huyo, ambaye aliwabeba vilivyo msimu uliopita kwa kufunga mabao 28 katika michuano mbalimbali huku akionekana kuwa mfano kwa mastaa wengine wachanga.
United pia inataka kuachana na mshahara mkubwa inaomlipa staa huyo, ambaye kwa wiki alikuwa akichukua kiasi cha Pauni 367,640 huku akiwa miongoni mwa wachezaji watatu wanaolipwa zaidi Old Trafford sambamba na Wayne Rooney na Paul Pogba.
Mara ya mwisho Zlatan alionekana akiwa na wachezaji wenzake wa United katika pambano la fainali dhidi ya Ajax jijini Stockholm ambapo, alijumuika nao kusherehekea ubingwa huo uliowapa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

                                                                       Ibrahimovic
Kwa sasa Zlatan amekuwa akifanya mazoezi mepesi huku akiendelea na matibabu na daktari wake, Dario Fort ambaye pia ni rafiki yake wa karibu huku akiwa amepewa ofa ya kuendelea kuutumia uwanja wa mazoezi wa United, Carrington mpaka atakapomaliza mkataba wake Julai mwaka huu.
United imekuwa ikihaha kusaka mshambuliaji mahiri wa kuziba pengo hilo ambapo kwa sasa Kocha Jose Mourinho ameelekeza macho yake kwa staa wa Real Madrid, Alvaro Morata baada ya kumkosa Romelu Lukaku, ambaye ameamua kurudi timu yake ya zamani Chelsea.
United pia imekuwa ikimsaka mshambuliaji wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann lakini mambo yamekuwa magumu baada ya klabu hiyo ya Hispania kufungiwa kununua wachezaji mpaka Januari mwakani, baada ya kufanya faulo katika masuala ya uhamisho hivi karibuni.
Zlatan ana ofa nyingi mezani kwake kwa mujibu wa wakala wake Mano Riola, ambapo inasemekena amekuwa akitakiwa na klabu mbalimbali za China na Marekani, lakini kwa sasa amejikita katika kuwa fiti kabla ya kuamua ofa zake.
Achilia mbali Zlatan, wachezaji wengine wenye majina makubwa ambao walitazamiwa kuachwa na Ijumaa ni pamoja na beki mkongwe wa Chelsea, John Terry ambaye anakaribia kutua Bournemouth kwa mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki.

                                                                               John Terry 
Wengine ambao walitazamiwa kuonyeshwa njia jana ni pamoja na mastaa wanne wa Manchester City, kipa Willy Caballero, winga  Jesus Navas na mabeki wawili wa pembeni wa Kifaransa, Gael Clichy na Bacary Sagna. Wote hawa mikataba yao imemalizika na Kocha Pep Guardiola yupo bize kutafuta wachezaji wa kuziba nafasi zao kwa sasa.
Kiungo mtukutu wa Burnley, Joey Barton anasaka timu mpya ya kuchezea baada ya kuachwa na klabu hiyo kufuatia kifungo chake cha miezi 18 baada ya kupatikana na hatia ya kujishughulisha na uchezaji wa kamari.

Post a Comment

 
Top