0
                                          IMEANDIKWA NA PRIVA ABIUD
GHAFLA kuna watu wameamua kuwa maafisa wa Uefa  na wameanzisha sheria zao binafsi katika kupanga timu ipi iende au isiende kushiriki michuano ya kimataifa.
Wametokea baadhi ya wachambuzi ambao wao wanadai kuwa wanaijua sheria ya Uefa kuliko ilivyoandikwa kwenye sheria hizo. Huwa najiuliza vigezo vipi hutumika ili mtu kutafsiri maneno ya kiingereza na kuyafanya kuwa ya Kiswahili? Yaani unahitaji nini ili uwe mtafsiri mzuri? Maana hawa wachambuzi wamekuwa wakitafsiri makala za kiingereza huku wengi wao wakiwa hawana ueledi mzuri wa lugha hivyo na wengi wao huishia kupotosha jamii.
Samahani kama nitakuwa nimekukwaza ila kama huna elimu yoyote kubwa ya lugha achana na utafsiri na tafuta mhusika akusaidie ili kulinda uweledi wako katika kuchambua kwako soka.
Ni kweli kumekuwa na mabadiliko mbalimbali katika sheria mbalimbali za Uefa. Watu wanapaswa kuelewa kuwa idadi ya timu zinazoshiriki Uefa huwa zinatofautina kila mwaka kutokana na maendeleo ya kiuchumi katika kuendesha ligi mbalimbali. Mabadiliko ya washindi wa Ligi ya Mabingwa na ligi Ueropa, pia baadhi ya mataifa kujiondoa kwenye shirkisho la Uefa au baadhi ya nchi kujiunga katika shirkisho hilo.
Kwa mfano mwaka 2012 zilishiriki timu 75 kutoka mataifa 52, mwaka 2014-15 zilishiriki timu 77 kutoka mataifa 53, ila kwa mwaka 2016-17 zilishiriki timu 78. Ingawa shirikisho la Uefa linajumuisha mataifa 55, kwa mfano mwaka 2016 mataifa kama Kosovo na Liechtenstein hayakushirki katika michuano hiyo licha ya kuwa wanachama kutokana na kukosa baadhi ya sifa zinatambulika na Uefa.

Ili kushiriki michuano ya Uefa kuna leseni huwa zinatolewa kwa kila taifa kulingana na hadhi ya ligi hiyo, pia wanaangalia vitu kama viwanja na masuala ya bajeti ya ligi hiyo n.k
Sasa nataka niwaeleze baadhi wachambuzi wakubwa ambao wamekuwa wakipotosha habari kuwa mshindi wa nafasi ya nne ya Ligi Kuu ya England msimu huu, Liverpool haitashiriki michuano ya Uefa baada ya Manchester United kutwaa ubingwa wa Europa.
Kwanza hawa wachambuzi wanapaswa wajue kuna makundi makuu yaliyotengwa na Uefa kulingana na alama mbalimbali, kuna kundi la kwanza ambalo linajumuisha nchi tatu (Hispania, Ujerumani na Uingereza) kundi hili linapeleka timu tatu moja kwa moja katika makundi ya Uefa na mshindi wanne anaenda kucheza mtoano.
Kuna kundi la pili linajumuisha mataifa ambayo yanepeleka timu mbili moja kwa moja na mshindi wa tatu ataingia kwa kucheza mtoano, kundi la tatu linajumuisha mataifa ambayo yanapeleka timu moja huku mshindi wa pili ataenda kucheza mtoano,na kundi la mwisho ni lile linalopoleka timu moja tu.
Mbali na hayo makundi sheria ya Uefa pia imeweka nafasi za upendeleo kwa bingwa wa Uefa na bingwa wa Ueropa kuingia kwenye makundi moja kwa moja bila kucheza mtoano wala kuathiri idadi ya timu zinazoingia Uefa kwa makundi tajwa hapo juu, ispokuwa kuna baadhi ya mazingira yatamfanya bingwa wa Ueropa kucheza hatua ya mtoano na ntaelezea hapo mbele.
                                                                        Firmino
Hadi mwaka 2013 kamati ya Uefa ilikaa rasmi na kufanya mabadiliko yafuatayo
1.    Iliongeza idadi ya mwisho kabisa ya timu kuingia kwenye Uefa na kufikia idadi ya timu tano (maximum qualifications teams). Hapo awali ilikuwa timu nne. mabadiliko haya yalifanyika mwaka 2013 lakini yalianza kutumika ramsi 2015-16.
2.    Sheria pia iliweka vigezo kuwa bingwa Ueropa atacheza michuano ya mtoano endapo tu bingwa wa Uefa atatoka ligi moja sawa na bingwa wa Ueropa na mabingwa hao wote kushindwa kuingia Uefa kwa kumaliza nafasi ambazo zinawaruhusu kupita kwa msimamo wa za ligi kulingana na makundi tajwa hapo juu. Kwa mfano (kumaliza nje ya top four). mfano mwaka 2015, Barcelona alitwaa ubingwa wa Uefa na Sevilla ikatwaa ubingwa wa Europa, lakini Valencia alimaliza nafasi ya 4 huku Sevilla ikimaliza nafasi ya tano, Valencia alingia Uefa kwa kucheza michezo ya mtoano lakini Sevilla ilipita moja kwa moja kwa kuwa alikuwa mshindi wa Ueropa na haikuathiri nafasi ya aliyekuwa mshindi wanne katika ligi.
Swali ni je, kwa nini Sevilla hakucheza mtoano?  Sheria inasema kwamba bingwa wa Europa atacheza mtoano angalau/endapo tu kama ikitokea bingwa wa Uefa ametokea ligi hiyo hiyo aliyotokea bingwa wa Europana wote kushindwa kumaliza nafasi zinazomruhusu kuingia kwenye Uefa moja kwa moja. Maana yake ikiwa mabingwa hao wameshindwa kukaa nafasi za nne za juu, basi anayeshikilia nafasi ya nne atanyang’anywa nafasi hiyo na itachukuliwa na bingwa wa Europa, hivyo bingwa wa Uefa ataingia bila kujali nafasi aliyopo ili kufikia lengo la kutozidi timu tano kuingia kupitia ligi moja.
Kwa mfano mwaka 2015 kama Barcelona na Sevilla wote wangetoka nafasi za nne za juu maana yake Valencia aliyekuwa nafasi ya nne nafasi yake ingechukuliwa na Sevilla, ambayo ingeenda kucheza mtoano ikichukua nafasi ya mshindi wa nne, huku Valencia ingeelekea zake Europa, Barcelona ingeingia moja kwa moja hata kama ingemaliza nafasi ya 17 ya ligi.
3.    Idadi ya timu kuingia Uefa kwa kila ligi haiwezi kuathiriwa hata kama bingwa wa Uefa au Europa watatoka nje ya nafasi za nne za juu. Sheria hii ni kwa mataifa yanayopeleka timu nne tu ndio yenye sifa hiyo ya kupeleka timu tano Uefa na sio kwa mataifa mengine.
Watu wengi wamechanganya sheria hii na kipindi kile Chelsea ilipotwaa ubingwa wa Uefa kisha ikamaliza wa sita na ikashiriki Uefa na kumnyang’anya Tottenham Hotspur iliyomaliza ya nne kwenye msimamo wa ligi na kusukumwa Europa. Baada ya malalamiko mengi dhidi ya sheria ile iliyonekana kuzionea timu zinazomalzia nafasi ya nne, basi kamati kuu ya Uefa ilikuja na sheria hii mpya ambayo ilikuwa lengo lake ni kuwabeba mabingwa wa Uefa na Europabila kujali nafsi zilizopo na pia bila kuathiri idadi ya timu ambazo zinapaswa kushiriki Uefa ispokuwa kuwa tu zisizidi timu tano.
                                UTATA UMEKUJAJE?
Wachambuzi wengi wa soka najua wamesoma ile sheria ambayo inasomeka hivi [winner of Uefa and Europa each given additional entry if they do not qualify for Uefa through their domestic league. “Because a maximum of five teams from one association can enter to the champions league, if both the winner of Uefa and Europa are from the same top three ranked association and finish out of top four of their domestic league the fourth placed team will be moved to Europa league.”
                                                               Kikosi cha Arsenal
Kwa akili ya haraka haraka wachambuzi wengi wamekimbilia kwenye neno 'both' kwa uelewa wao wanadhani kuwa eti ili timu ziende tano lazima mabingwa hao watoke ligi moja. Hivyo wasipotoka ligi moja nafasi ya timu tano haipo. Naomba niwasaidie kidogo na kiingereza changu cha shule ya kata chenye cheti original ni kwamba, hapo walipoweka neno 'both' hawakumaanisha kuwa lazima mabingwa hao watoke ligi moja, la hasha, neno hilo limetumika kumaanisha kuwa  ni lazima mabingwa hao watoke kwenye (top three ranked association) yaani lazima watoke kwenye kundi namba moja ambalo linapeleka timu nne Uefa ili huyo wa Europa apewe nafasi hiyo ziweze kutimia timu tano.
Kama hamjaniliewa naomba mrudi tena kwenye makubaliano ya kamati ya Uefa ya mwaka 2013 juu ya sheria hii ambayo yanasema hivi “The previous limit of a maximum of four teams per association will be increased to five, meaning that if the Champions League title holders or the Europa League title holders are from the top three ranked associations (but not both from the same one) and finish outside the top four of their domestic league, the fourth-placed team of their association will not be prevented from participating in the tournament.”
                                                                    Alexis Sanchez
Sheria imeweka wazi mabingwa wakitokea ligi moja na wakamaliza nje ya nafasi za nne za juu hapo ndipo nafasi ya nne hupoteza nafasi ya kwenda Uefa lakini kama hawajatoka ligi moja, basi nafasi ya nne haitaathirika hata kidogo.
Niwakumbushe tu usitumie hisia tu kuchambua sheria, hili suala lipo kisheria kuliko kihisia zaidi na sio porojo za kishabiki wala mapenzi. Watu wamekaa vijiweni na kuanza kuwatia wasiwasi wamashabiki wa Liverpool na hata wa Arsenal lengo ni kuwaaminisha wao kuwa ni Manchester United tu ndio itapata nafasi hiyo. La hasha.

Post a Comment

 
Top