BARCELONA, HISPANIA
LIONEL MESSI amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka mitano wa kuendelea kuichezea Barcelona na sasa kama kutakuwa na timu inayotaka kumsajili ndani ya muda huo, mkataba wake utavunjwa kwa Pauni 350 milioni.
Staa huyo alitajwatajwa kwamba huenda akabadili timu katika dirisha hili la usajili huku Manchester City, Chelsea na Paris Saint-Germain zikionekana kuwa na jeuri ya kulipa pesa za kumnasa Muargentina huyo, lakini kwa sasa ukimtaka lazima ujipange.
Mkataba wa awali wa fowadi huyo ulikuwa unamalizika mwaka 2018, hivyo kulikuwa na hatari ya kuondoka bure kabisa Barcelona kama makubaliano yangeshindwa kufikia mwafaka.
Imeripotiwa kwamba baba yake, Jorge, alikuwa katika majadiliano na mabosi wa Barcelona katika siku za karibuni.
Imeelezwa mkwanja mpya atakaokuwa analipwa Messi utakuwa hatari kweli kweli baada ya kuripotiwa kugomea dili la kutoka China ambalo lingemshuhudia akilipwa Pauni 800,000 kwa wiki.
Kufika mwafaka kwa dili hilo la Messi, kunamfanya kocha mpya wa timu hiyo, Ernesto Valverde, kushusha pumzi na kufikiria mipango mingine ya kupambana na Real Madrid msimu ujao.
Messi (pichani juu) alifunga mabao 54 katika mechi 52 alizochezea Barcelona msimu uliopita ambapo walimaliza nafasi ya pili kwenye La Liga, lakini walibeba taji la Copa del Rey.
Kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Argentina kinachojiandaa na mechi za kirafiki dhidi ya Brazil na Singapore zitakachofanyika Juni 9 na 13 kama zilivyopangwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment