MADRID, HISPANIA
CRISTIANO RONALDO ni mchezaji matata ndani ya uwanja na pia anawaongoza mastaa wengine hadi nje ya uwanja kwa kuwa na pesa nyingi.
Jarida la Forbes limetoa orodha ya wanamichezo 100 waliolipwa pesa nyingi kwa mwaka uliopita na Ronaldo ameshikilia kilele kwa kuvuna Pauni 71.8 milioni. Huu ni mwaka wa pili mfululizo staa huyo wa Real Madrid anashikilia kilele.
Kwenye namba mbili yupo staa wa mpira wa kikapu, LeBron James, aliyevuna Pauni 66.6 milioni na kisha anafuatia Lionel Messi aliyevuna Pauni 61.8 milioni.
Ronaldo, 32, analamba Pauni 44.8 milioni kutoka katika mishahara yake anayolipwa klabuni Real Madrid na Pauni 27 milioni alizipata kutoka kwenye dili nyingine za kibiashara.
Kabla ya Ronaldo kuchukua kilele hicho, wanamichezo waliokuwa wanaongoza walikuwa ama mcheza tenisi Tiger Woods au bondia Floyd Mayweather na ilikuwa hivyo kwa miaka 15 mfululizo.
Lakini, safari hii, Woods anashika namba 17, wakati Mayweather ameshindwa kabisa kuingia kwenye orodha hiyo ya wanamichezo 100 kwa sababu hajapigana pambano lolote kwa karibuni.
Orodha ya wanamichezo 10 bora waliovuna pesa nyingi kwa mwaka uliopita baada ya Ronaldo, LeBron James na Messi kushika namba tatu za juu, kwenye namba nne yupo staa wa tenisi, Roger Federer (Pauni 49.4 milioni), wa tano ni staa wa mpira wa kikapu Kevin Durant (Pauni 46.8 milioni) na wa sita ni nyota wa gofu, Rory McIlroy (Pauni 38.6 milioni).
Nyota na mchezaji wa American Football, Andrew Luck yupo kwenye nafasi ya saba baada ya kuvuna Pauni 38.6 milioni wakati mkali mwingine wa kikapu Stephen Curry na Pauni zake 36.5 milioni anashika namba nane na kuwaongoza James Harden aliyeweka mfukoni Pauni 36 milioni na wa kumi ni dereva wa magari ya Formula One, Lewis Hamilton, aliyevuna Pauni 35.5 milioni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment