IMEANDIKWA
NA PRIVA ABIUD
BABA aliniambia mbinu madhubuti ya kujilinda
ukiwa uwanjani kuhakikisha unakaa na mpira muda mwingi kuliko adui yako. Hayo
si maneno yangu ni maneno ya Pep Guardiola.
Kwa
takribani muongo mmoja na zaid Jose Mourinho amejijengea Heshima kubwa kisoka
Ulaya na hata dunian kwa jumla. Heshima hii ya Mourinho ameijenga kwenye
mazingira magumu sana, kiasi kwamba amejijengea maadui wakubwa kwenye soka na
hata nje ya soka. Kocha huyu wa Manchester United tayari hatihati ya heshima
yake kusahaulika imeanza tokea alipotokea Inter Milan.
Maisha
yake yalianza kuwa magumu ndani ya Real Madrid baada ya kuaanza kujenga makundi
ndani ya klabu kwa kile alichokiamini yeye.
Ni
kweli kila mwalimu anakuwa na falsafa zake kuhakikisha kuwa mwanafunzi wake
anamwelewa ipasavyo. Mourinho ni kiongozi anayeongoza jeshi lake. Lugha yake
huenda ikaunganisha jeshi lake au huenda akawatenganisha wafuasi. Mourinho ni dereva
mzuri ambaye naamini ana leseni sahihi kabisa tatizo naona ni ujuaji.
Kwenye
basi kila abiria ana malengo yake, yupo anyetaka kufika salama, yupo anyetaka
kuwahi na yupo anayetaka gari lifike wakati wowote.
Mourinho
Sina
shaka na uwezo wa Mourinho katika weledi wake kisoka wala sina tatizo na namna
alivyopata mafanikio yake, ila kuna mambo hayapo sawa. Mtangazaji mmoja maarufu
wa Uingereza, John Giles amesema Mourinho ni mtu mwenye vurugu na mbabe akiwa
nje na ndani ya uwanja na hiyo ndio iliyompa mafanikio na ndio njia itakayoporomosha
ufalme. Mwaka 2011 aliwahi kumgusa na kidole kwenye jicho kwa makusudi kabisa
aliyekuwa kocha msaidizi wa Real Madrid. Hata mara baada ya mchezo huo hakuomba
msamaha.
Achia
mbali ugomvi wake mkubwa dhidi ya aliyekuwa dokta wa Chelsea dada, Eva Carneiro.
Ugomvi ambao ulimfanya Eva apoteze kibarua chake ndani ya Stamford Bridge.
Ninachokifahamu mpira wa sasa umebadilika sana. Dunia inalekea kwingine tofauti
na kule tulipotoka. Wakati dunia ya ujamaa ikidondoka miaka ya 1980, Mwl Julius
Kambarage Nyerere aliona isiwe tabu akang’atuka.
Sio
kwamba hakuutamani uraisi, sio kwamba alizeeka, bali aliona falsafa zake
zikipukutika.
Ferguson
Mourinho anarudi tulikotoka, bado anawaenzi kina Alex Ferguson kwa
kuwa mbabe, mkorofi na mwenye msimamo wake bila kupingwa. Kipindi kile cha kina
Ferguson wachezaji walikuwa na nidhamu kama wanajeshi, mchezaji alikuwa
akikoromewa hajibu wala haweki kiburi, tena ilikuwa ukionesha kujaribu kupingana
na maamuzi ya Ferguson unapotezwa kwenye soka kama kina Luis Nani.
Sababu
zilizochangia soka la kipindi kile kuwa na nidhamu kubwa kiasi kile ni
mishahara na sifa za klabu. Wakati ule mchezaji mkubwa alilipwa mshahara sawa
na anaolipwa Luke Shaw kwa sasa. Katika dunia ile hauwezi kusikia kinda mwenye
umri wa miaka 18 anauzwa Pauni zaidi ya 10. Miaka ile klabu kubwa zilikuwa
zinaheshimika kuliko pesa. Leo hii wachezaji wanaheshimu pesa kuliko sifa ya
klabu husika. Miaka hii mchezaji anaikata Manchester United na anajiunga na
Monaco bila tatizo kabisa.
Mbappe
Sifa
za klabu hizi zimepukutika kiasi kwamba mchezaji anangalia kalamu yake
itaandika kiasi gani cha pesa zaidi. Leo hii kinda wa miaka 22 anauzwa Pauni 120
milioni. Leo hii mchezaji mdogo kama Kylan Mbappe anauzwa Pauni 70 milioni,
unajiuliza kwa lipi? Je, mchezaji kama huyu mshahara wake utakuwa kiasi gani?
Je, mchezaji wa namna hii ukimkoromea atakusikiliza? Chukulia mfano mwepesi
ugomvi wa Angel Di maria na Loius Van Gaal? Mwishowe Manchester United ilipoteza
huduma za Di Maria kwa kuwa hakutaka kupelekeshwa na falsafa za Van Gaal kama
mtoto.
Wachezaji
wengi wa siku hizi wanaamini zaidi katika miguu yao kuliko miluzi na makelele
ya makocha wao.
Di Maria
Ndio
wana kiburi maana Waarabu wanaotoa pesa nzuri wapo. Miaka ya nyuma wachezaji
walikuwa wakitega masikio yao kwa waalimu wao zaid kuliko kile alichonacho
mguuni mwake. Mourinho bado habadiliki na anamini kuwa miluzi na makelele na
vijembe kwenye mikutano ya waandishi wa habari itampa mafanikio anayotaka. Swali
linakuja, katika kipindi cha miaka ya hivi karibu Mourinho amekuwa na maisha ya
aina gani katika klabu alizokuwa, je, katika klabu alizotoka za Chelsea na Real
Madrid bado zinamtamani tena?
Kama
hapana ni kwanini? Baada ya kutokea mvutano mkubwa akiwa Real Madrid aliondoka
kama hakuwa kocha mkubwa, hakuna aliyemgeukia, hakuna aliyejali rekodi zake.
Binafsi yangu siuoni mwelekeo sahihi kwa Manchester United chini ya Mourinho.
Sioni Man United ikirudi kule ilipotoka, bali naona ikirudi ilipotoka
Tottenham, naiona ikipambana na West Bromwich na Everton.
Bado
naiona United ileile aliyoicha David Moyes na Van Gaal. Watu wanasema Mourinho
apewe muda, swali linakuja? Mnataka apewe muda wa nini wakati ameshapewa
mabunda ya fedha?
Van Gaal
Leo
hii tukimpa Mourinho fedha na muda, je, kocha mpya ya Sunderland naye atapewa
nini? Ikiwa Crystals Palace yenyewe haikumpa muda Allan Pardew huu mnaotaka
kumpa Mourinho mmeutoa wapi?
Miaka
ya nyuma kocha anapewa muda kutokana na aina ya wachezaji ulionao, miaka ya
nyuma timu ikiwa haina pesa inatumia wachezaji wa academy na kuwapa ushindi,
sio mchezaji wa Pauni 40 milioni apewe muda. Real Madrid haikutaka kumvumilia Rafael
Benitez wakamkabidhi Zinadene Zidane mikoba na aliwapa walichokitaka.
Watu
wanadai kuwa majeruhi ndio chanzo? Hivi mnakumbuka mwaka 2009 Man United dhidi
ya Wolfsburg, kulekule Ujerumani Wolfsburg ilikung’utwa 3 mabeki wa kati wakiwa
Michael Carrick na Darren Fletcher?
Katikati
walikuwepo Gibbs Daron, J sung Park kama beki mbili, kipa Tomasz Kuszczak, mbele
walikuwepo Anderson, Nani, Paul Scholes na Antonio Valencia, huku Gabriel Obertan
akimpokea Danny Welbeck?
Wellback na J Sung Park
Kikosi
hiki angepewa Mourinho dhidi ya Manchester City angefanyaje? Najiuliza kama Man
United dhidi ya Man City unakuwa na kina Ander Herrera, Antony Martial, Marcus
Rashford, Henrikh Mikhitaryan, Valencia, kipa David de Gea, Eric Bailly, Daley Blind
lakini bado timu inaishia kukaba?
Najiuliza
kwenye ule mchezo ambao wengi wanalaumu kukosekana na uwepo wa Paul Pogba ndio
kumefanya timu ikose matokeo, swali linakuja, kama Pogba hakuwepo kuunganisha
timu, je, Martial alikuwa anafanya nini beki ya kushoto? Je, kulikuwa na
ulazima gani wa kumpeleka Mikhitaryan akamsaidie Valencia?
Mikhatryan
Hivi
leo hii Pogba anageuka kuwa matokeo ya Man United? Si aliondoka Ronaldo? Si
waliondoka kina Paul Scholes? Pogba ni nani hadi akikosekana timu icheze mchezo
mbovu kiasi kile? Hivi mnataka kuiaminisha dunia kuwa Morouane Fellani, Herrera
na Carrick waliwekwa ili wakamkabe Yahya Toure?
Hivi
Man United ni ya kujilinda kiasi kile hadi mbele ya kina Leroy Sane, Jesus Navas
na Raheem Sterling eti kisa Pogba hayupo? Sasa kama unajilinda kwenye mchezo
dhidi ya wachovu hiyo Uefa mnaitaka ya nini?
Au
na nyie mnataka 10? Man United hii hii imekosa matokeo sahihi Old Trafford dhidi
ya Anderlecht timu iliyokuja kushangaa Jiji la England hadi mashabiki 70, 000
ilibidi wasubiri hadi dakika ya 117? Man United hii hii?
Ngoja
niwakumbushe kitu mashabiki wenzangu wa Man United dhidi ya Arsenal 2011 Ferguson
alimweka Gibson, Oshea, Rafaeli na Fabio kama viungo kwenye mchezo wa FA na
timu ilipata matokeo sahihi bila ya kujilinda kwa dakika 80. Nikukumbushe tena
mwaka 2014, Van Gaal dhidi ya Arsenal, alikuwa na majeruhi kiasi hakuna
aliyekuwa anaamini kama United ingejipatia
ushindi uwanjani Emirates.
Beki
za United ilikuwa Paddy Macnair, Chris Smalling, Tyler Blackett, Luke Shaw
katikati alikuwepo Fellaini, lakini kwa safu hiyo ya ulinzi mbovu bado ilibidi
Arsene Wenger asubiri hadi dakika ya 95 kupita bao la kufutia machozi kupitia kwa
Oliver Giroud.
Fellaini
Mfumo
mbovu na wa kizamani wa Mourinho, vijembe vyake kwenye mikutano na waandishi wa
habari ndio chanzo cha kuporomosha kiwango cha United. Ni kweli United mbali na
usajili mkubwa bado ni klabu yenye matokeo mabovu ukilinganisha na sifa zake.
Wachezaji wengi wa United kwa sasa wameonekana kuwa wachezaji wabovu. Leo hii
wachezaji wa wawili tu wa United ndio waliovuka zaidi ya mabao matano ya ligi ambao
ni Zlatan Ibrahimovic (mabao17) na Juan Mata (mabao 6). Swali linakuja je, ni
kweli uwezo wa Martial, Mikhitaryan Rashford, Rooney ni wa kufunga mabao manne
tu?
Rooney
Kama wewe unacheza nafasi ya kushambulia ndani ya klabu kubwa kama United na
bado unashindwa kuvuka mabao hata matano maana yake hufai kuwa mahali pale.
Sasa kama ukiwa United unashindwa kuvuka mabao
matano je, ukienda Stoke City timu inayomtaka namba10 akabe kama namba 5
utafunga mangapi?
Je, ni kweli wachezaji wa Man United ni
wabovu? Je, ni kweli Mikhitaryan ni mbovu? Je, ni kweli Mata na Martial ni
wabovu? Je Rashford hafai? Tatizo ni nini?
Je, miaka ya nyuma hawa wachezaji walivuka
idadi hiyo ya mabao? Kama ndio je, nani alaumiwe? Mourinho amekuja na tabia ya
kutumia lugha za kebehi kwa wachezaji hasa pale anapopata matokeo mabaya.
Amekuwa na tabia ya unafiki dhidi ya wachezaji. Anaonesha hisia za wazi kabisa
kwa baadhi ya wachezaji.
Zlatan
Kiungo Pogba alicheza chini ya kiwango kabisa katika
mchezo dhidi ya Liverpool uwanjan Anfield. Lakini mwalimu alikuja kwa waandishi
wa habari na kumsifia. Lakini ni mara nyingi tumeona jinsi Martial na Rashford
wammekuwa wakichezeshwa katika nafasi ambazo zimekuwa ngumu kwao, lakini
mwalimu bado amekuja kwenye mikutano na waandishi na kusema kuwa wachezaji hao
ndio wameshindwa kuipa timu matokeo.
Mourinho
ameshindwa kuficha hisia zake za chuki kwa Martial mara nyingi. Mourinho
amekuwa sio mtu wa kuamini miguu ya wachezaji na amekuwa akitegema zaidi miluzi
yake pale anapombwatukia Martial arudi kukaba.
Martial
na wachezaji wengine ambao kwa uasilia ni washambuliaji na sio wakabaji
wamekuwa wahanga wa makelele ya uwanjani na nje ya uwanja. Mourinho ameondoa ‘apetaiti’
ya wachezaji kuwa na chachu ya kupata mafanikio. Mourinho amejenga mlingoti wa
bendera kwenye barabara ya mashindano ya riadha ambayo ni Zlatan na anataka
kila mwanariadha lazima asimame aiheshimu bendera ambayo ni kichwa chake.
Kila
mchezaji amekuwa akimwangalia Zlatan kama mchezaji pekee mwenye jukumu la
kupewa mipira yote ya kufunga.
Mpira
wa kupiga krosi kila wakati umeathiri kwa kiwango kikubwa wachezaji wanaotumia
miguu na akili zaid kuliko mwili/vichwa. Zlatan ni mchezaji anayetegemea zaid
mwili/kichwa kuliko miguu yake, Martial anategemea zaidi mguu kuliko mwili.
Wachezaji
wanaotegemea miguu wamepewa kazi moja tu, kukaba na kumlisha mipira Zlatan. Angalia
Liverpool ya Jurgen Klopp, Sadio Mane
ana mabao 13, Firmino anayi 11, Milner
amefunga 7, Adam Lallana amepachika 7, Coutinho anayo10 hata Orig anayesugua benchi
amefikisha 6. Hii ina ashiria nini? Klopp hajajenga mlingoti wa bendera,
amawaweka huru washambuliaji wake.
Mourinho
amekuwa na ulinzi mkali wa Marcos Rojo na Eric Bailley, ulinzi ambao hata Klopp hana.
Kiwango kikubwa cha Valencia Pogba, Herrera Na Carrick ilikuwa tayari ni silaha
tosha kwa Mourinho kuwaacha kina Rashford wamletee matokeo kwa namna yoyote
ile.
Pogba
Mourinho
amekuwa na maamuzi ya ‘kibashite’, maamuzi magumu na yasiyo na busara, Mourinho
anataka kuiaminisha dunia kuwa Morgan Schneiderlin alikuwa mbovu kuliko Fellaini?
Bado anazidi kutudanganya kuwa Jesse Lingard ni bora kuliko Mikhitaryan? Bado
anaamini mpira wake wa kukaba zaidi na kuweka mshambuliaji mmoja kuwa bado
utampa mafanikio katika dunia ambayo washambuliaji kwa sasa wanawekwa watatu?
Bendera
alizoziweka Mourinho ya kuwaropokea wachezaji ovyo, kukaba zaidi, kuamini
katika miluzi yake na mengine haziheshimiwi tena.
Luke Shaw
Kama
Mourinho hatabadilika basi naomba nimtakie usiku mwema tu maana kwake tayari giza
lishaingia.
Wachezaji
wa siku hizi hawapelekeshwi, ni kama makandarasi, wanahitaji ajira ila
usiwalazimishe cha kufanya. Ukienda sokoni kununua wachezaji wa gharama kubwa
unapaswa ujue kuwa hununui mitumba. Hawapelekeswhi ovyo. Hawatishwitishwi. Wape
kazi watafanya wakimaliza walipe vizuri. Mourinho naamini zipo njia nyingi za
kuwakosoa wachezaji. Siamini kama Mourinho anatafuta kiki kwa kuwatukana
wachezaji wake.
Ninachojua
hiyo ni tabia yako ila kwa sasa ni usiku usirushe mawe gizani utampiga hata
mwanao.
Post a Comment