0


BARCELONA, HISPANIA
JAVIER Mascherano amecheza mechi 319 ndani ya jezi za Barcelona amefunga bao moja tu, tena kwa mkwaju wa penalti wakati timu yake ilipoangusha kipigo cha nguvu kwa Osasuna cha mabao 7-1 uwanjani Nou Camp kwa La Liga juzi Jumatano.
Barcelona licha ya kufunga mabao lukuki kama yale la kwenda kriketi na mpira wa kikapu kwa muda ambao Mascherano alijiunga na timu hiyo mwaka 2010 cha ajabu staa huyo wa Argentina hakuwa amepata bao lake mwenyewe hadi hapo juzi.
Denis Suarez aliangushwa ndani ya boksi na Barca kupewa penalti kipindi hicho ikiwa mbele kwa mabao 5-1.
                                             Mascherano
Mascherano alipewa kupiga mkwaju huo na alipofunga ilikuwa furaha kubwa kuanzia kwa mashabiki hadi kwa wachezaji wenzake katika kikosi hicho.
Lakini, bao hilo la Mascherano limeandika rekodi nzuri kwa Kocha Luis Enrique pia likiwa la 500 tangu alipoanza kuinoa Barcelona mwaka 2014.

Mascherano akienda kupiga penatli
Baada ya kucheza kiungo karibu sehemu kubwa ya maisha yake ya soka, Mascherano, 32, miaka ya karibuni amekuwa akitumika kama beki wa kati, jambo linalomfanya kuwa adimu sana kusogea kwenye nusu ya timu pinzani. Ukiweka kando bao lake la juzi, mara ya mwisho Mascherano kufunga ilikuwa Juni 2014 akiwa na Argentina ilipocheza na Trinidad & Tobago. Lakini, kwa Barcelona lilikuwa bao lake la kwanza huku kwa timu ya taifa amefunga mara tatu tu katika mechi 136. Kwenye ngazi ya klabu, bao lake la mwisho ukiacha na juzi alifunga wakati huo akiwa Liverpool kwenye mechi dhidi ya Unirea Urziceni, Februari 2010.

Post a Comment

 
Top