0
BARCELONA, HISPANIA
PATRICE EVRA amefanya kitendo cha kishujaa na kuonyesha kwamba kuna maisha baada ya soka kwa kuweka chuki pembeni na kumpongeza hasimu wake, Luis Suarez.
 Beki Evra anayeitumikia Juventus ya Italia amempongeza straika huyo wa Barcelona na kumwita namba tisa bora baada ya Suarez, kutwaa Kiatu cha Dhahabu baada ya kuibuka kuwa Mfungaji Bora wa Ulaya  msimu wa 2015-16.
Wakati walipokuwa Ligi Kuu England wachezaji hao walikuwa na vita vya maneno baada ya beki huyo Mfaransa kumtuhumu Suarez kumtolea maneno ya kibaguzi katika mchezo kati ya Liverpool na Manchester United Oktoba 2011.
Suarez straika wa kimataifa wa The Uruguay alifungiwa michezo minane kuitumikia Liverpool kutokana na tukio hilo, pia alitozwa faini ya Pauni 40,000 lakini hakukubaliana na uamuzi huo na alikataa kushikana mikono na Evra wakati timu zao ziliporudiana Februari 2012.

Suarez na Evra walipokuwa England.
Katika tukio linalohusiana na mwendelezo huo, Evra alishangilia ushindi wa Manchester United siku hiyo mbele ya Suarez na kusababisha majibizano kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa Liverpool.
Hata hivyo, beki huyo wa kushoto wa Juventus ameonekana kuweka tofauti hizo pembeni  na kuposti picha ya Suarez akiwa na tuzo yake kwenye mitandao ya kijamii.

Suarez akiwa na tuzo yake.
Evra aliandika katika ukurasa wake wa Instagram: “Katika Instagram yangu kuna upendo na hakuna chuki!!!
“Luis, wewe ni mchezaji mkubwa, na No 9 bora.  Hongera Luis @luissuarez9. I naupenda huu mchezo!!! hahahaah.”
Katika kutwaa tuzo hiyo, Suarez aliwazidi kete straika wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na mwenzake wa Barcelona, Lionel Messi baada ya kufunga mabao 59 katika michezo 53 akiitumikia timu yake.

Post a Comment

 
Top