0


MANCHESTER, ENGLAND
WAYNE ROONEY (pichani) wa Manchester United ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya England aliyecheza mechi nyingi kwa wachezaji wa kizazi cha hivi karibuni.
Rooney amefanya hivyo baada ya kuiongoza England Jumapili akiwa nahodha dhidi ya Slovakia katika mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha wa United ameitumikia England kwa mara ya 116 katika mchezo huo wa kwanza wa Sam Allardyce akiwa Kocha wa England na kumweka mbele ya nyota wa zamani wa United, David Beckham.

Ni kipa Peter Shilton tu ndiye amecheza michezo mingi zaidi yake 125, lakini Rooney- ambaye ametangaza kustaafu michezo ya kimataifa baada ya Kombe la Dunia 2018 – alisema kabla ya mchezo huo kwamba anaweka akili yake katika kusaka ushindi.
"Nadhani siku zote ni heshima kuiwakilisha nchi yako," aliwaambia waandishi wa habari.
"Kuwa mchezaji wa pili wa muda wote kitakuwa kitu kikubwa- lakini ni kuhusu timu, kuhusu kupata pointi tatu.

"Nina uhakika siku za mbele, nitageuka nyuma kuangalia (kwenye rekodi), lakini kwa sasa naangalia mchezo huo na si kitu kingine."
Rooney aliongeza: "Nimesema mara nyingi kwamba ninajisikia mtu mwenye fahari kuitumikia England.
"Nimekuwapo tangu nilipochaguliwa katika timu, na motisha wangu ni uleule kama ulivyokuwa siku ya kwanza."
Rooney mwenye umri wa miaka 30- alicheza mchezo wake wa kwanza kuitumikia England alipoingia kutokea benchi kuchukua nafasi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Australia, Februari 2003 akiwa na miaka 17  na siku111.

Post a Comment

 
Top