LONDON, ENGLAND
SAM ALLARDYCE (pichani chini) amekubali kuachia
ngazi kuinoa timu ya taifa ya England baada ya kufanya kikao cha maridhiano na Chama
cha Soka cha England (FA). Kocha huyo ameiongoza timu hiyo katika mchezo mmoja
tu.Kocha Allardyce alinaswa katika mkanda wa video akimshauri mwandishi jinsi ya kukwepa sheria ya umiliki wa tatu, kwa mujibu wa Gazeti la Telegraph.
Video iliambatana na ripoti inayoonyesha kwamba kocha huyo alifanya mkutano mara mbili na waandishi akiwa kama mwakilishi wa wakala wa Mashariki ya Mbali akiwa na nia ya kuvunja sheria za Chama cha Soka (FA) na Fifa.
"Tunaweza kupata karibu yake. Namaanisha, bila ya shaka, kuna pesa nyingi hapa," Kocha Allardyce alisema katika video hiyo, huku pia akiziita sheria ‘ujinga.’
Bosi huyo wa zamani wa Sunderland, alichaguliwa kama mrithi wa Roy Hodgson Julai mwaka huu, na aliiongoza timu hiyo katika mchezo mmoja ambapo England iliifunga Slovakia bao 1-0 katika hatua ya kufuzu kwa Kombe la Dunia. Bao hilo la jioni lililofungwa na Adam Lallana.
Chama cha Soka (FA) kimethibitisha kwamba kocha wa kikosi cha England cha U-21, Gareth Southgate atachukua mikoba ya kukinoa kikosi cha wakubwa katika michezo mingine minne dhidi ya Malta, Slovenia, Scotland na Hispania wakati akitafutwa kocha wa kudumu.
Uteuzi wa Allardyce- ambaye amedumu kwenye timu hiyo siku 67 kuwachagua makocha wasaidizi kina Sammy Lee, Craig Shakespeare na Martyn Margetson bado haujatolewa ufafanuzi ikiashiria kwamba wataendelea kumsaidia Southgate.
Post a Comment