HIKI NDICHO KILICHOMKIMBIZA VARDY ARSENAL
JAMIE VARDY (pichani) amefichua sababu zilizomfanya akache kujiunga na Arsenal katika dirisha la usajili la majira ya joto ili ajaribu kuijenga Leicester City katika kutetea taji lake la Ligi Kuu England.
Straika huyo wa Leicester alitakiwa na Arsenal ambayo ilifika dau lililokuwa likimrusu kuondoka la Pauni 20 milioni, lakini baada ya kutafakari kwa muda mrefu – straika huyo wa kimataifa wa England aliachana na mpango wa kujiunga na klabu hiyo ya Kaskazini mwa London kwa lengo la kuendeleana kocha wake, Claudio Ranieri uwanjani King Power.
"Haikuwa kwa sababu ya uaminifu au fikra juu ya wachezaji wenzangu, wachezaji kila siku wanakuja na kuondoka," alisema Vardy.
"Ilikuwa ni zaidi ya kuiona Leicester kama klabu inayotaka kujijenga kwa kile ilichovuna katika ubingwa na nilitaka kuwa sehemu ya hilo. Nina furaha jinsi kila kitu kilivyomalizika.
"'Ndoto zinaendelea,' Claudio (Ranieri) alinitumia ujumbe baada ya kukubali kubaki. Hivyo ndivyo nilivyojisikia, pia."
Kujiunga na klabu ambayo imemaliza chini ya Leicester katika ligi msimu uliopita bila shaka lilikuwa jaribio kubwa kwa Vardy, 29, lakini wasiwasi kuhusu jinsi gani ya kucheza, kama staili yake itaendana na ile ya Arsenal ilikuwa kikwazo kikubwa.
"Nilijaribu kuangalia faida na hasara," Vardy alisema. "Ukiwa na watu kama Alexis Sanchez na Mesut Ozil wanaotengeneza nafasi, Arsenal ningeweza kunufaika zaidi kuliko mimi kuwanufaisha wao.
"Lakini pia nililifikiria suala la ufundi. Unaangalia staili ya uchezaji ya Arsenal na hawana haraka ya kupeleka mpira mbele kama inavyofanya Leicester kupenyeza mipira nyuma ya mabeki kwa ajili ya watu wenye mbio kama mimi.
"Kitu kimoja ambacho hakikunitisha ni wazo kwamba nisingekuwa nyota mkubwa ndani ya Arsenal.
"Kila ninapokwenda, nimejipanga kukabiliana na changamoto mbele yangu. Tunaangalia pia shule mpya kwa ajili ya watoto, lakini nilifikia hatua moyo na kichwa changu vilinitaka kubaki Leicester."
‘Mbweha’ hao (Leicester) wameanza vibaya kutetea taji lao, tayari wameshapoteza michezo mitatu ya Ligi Kuu- ikiwa ni mingi zaidi kuliko ile ya msimu wa 2015-16.
Hata hivyo, Vardy na wachezaji wenzake wamepata ushindi wa mfululizo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Post a Comment