NA PRIVA ABIUD
JUZI
wakati wa mchezo wa Manchester United dhidi ya Hully City, Marouane
Fellaini alionekana
akimsaidia mwanamama mmoja aliyekwama miguu wakati mashabiki wa timu yake
wakishangilia bao la usiku kabisa la Marcus Rashford.
Fellaini huyu misimu mitatu
iliyopita hakuna shabiki wa united aliyekuwa tayari kumshika mkono? Fellaini
misimu mitatu iliyopita alikuwa mchezaji wa kuzomewa sana uwanjani. Hakuonekana
kama Fellaini yule wa Everton. Maisha yanakwena kasi sana, wakati Fellaini akizomewa, Antony Martial alikuwa Mussa wa wana wa Israel ndani ya Old Trafford. Leo nilikuwa nasikiliza Wimbo wa Mwanamama mmoja aitwaye Neema Mwaipopo unaimbwa ‘Anayekudharau Atakusalimia Kwa heshima.’
Hii ni tofauti kwa Martial, msimu huu amebakiza skendo na kutolewa katika mechi kila zinapofika dakika za 70 anapoonekana hana faida tena kwenye dakika zilizosalia.
Anaonekana kama ganda la ndizi, akiendelea kubakia uwanjani, basi wenzake watalikanyaga na kuteleza. kwenye soka kama hutumii nyakati zako vizuri hakuna atakaekukumbuka labda ukishaondoka uwanjani au ukiaga duniani.
Juzi nilimsoma jamaa mmoja anaitwa Ally Kamwe, anakwambia tunawakosea heshima kina Lionel Messi, Criastiano Ronaldo na Usain Bolt.
Tunawasifia waliokwishaondoka uwanjani ambao hawajafanya haya waliliyoyafanya hawa watu. Yaani mtu anakwambia Diego Maradona ni bora muda wote lakini anajifanya haoni wanayoyafanya Messi na Ronaldo.
Tuna tabia ya kusifia kisichokuwapo, tena kwa kujipiga kifua, mbaya zaid wengine hata hao kina Pele na Maradona hatukuwahi kuwaona.
Tuachane na hayo, Everton ilikuwa klabu ya kipekee na yenye mafanikio kwa Fellaini. Klabu ambayo nilimsikia Dr. Rick akisema: " David Moyes alikuwa anakabidhiwa Euro 5 milioni za usajili na anaambiwa, asitoke nafasi saba za juu.
Unajiuliza hiyo pesa atamnunua nayo nani? Mmoja wa wafalme waliomkomboa, Moyes pale Godson Park ni Fellaini. Msimu wa 2012 jamaa alimaliza akiwa na mabao13.
Fellaini aliweka rekodi ya mchezaji ghali kununuliwa Everton ya Euro 15 milioni nadhani huo msimu hakuna mwingine aliyesajiliwa?
Ila hapa naona kama Dr. Rick alitudanganya na kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Ubelgiji kununuliwa ghali kwa wakati huo. Ni mchezaji ambaye alitengeneza ufalme wake Everton.
Huwa kuna wakati namkumbuka sana. Anthony ‘Tony’ Hibbert aliyecheza zaidi ya mechi 260 bila kufunga bao lolote ndani ya Everton.
Yaani hajawahi kabisa kufunga katika maisha yake hata kwenye mchezo wa kumbukumbu yake alipocheza dhidi ya AEk Athens, hakufunga. Jamaa alikuwa ndiye mchezaji pendwa sana pale Everton na palikuwepo na jukwaa lililokuwa limejaa mashabiki wake tu.
Fellaini akiwa Everton, Hibbet hayupo tena uwanjan, lakini Fellaini aliyekuwa kipenzi cha Wana Everton bado yupo uwanjani, ila yupo kwenye ardhi ya laana, ardhi isiyokuthamini ukiwa chini.
Old Trafford ni kiwanda cha mashujaa, ni vigumu kwao kukutukuza ukiwa uwanjani kwa kipindi kirefu, Paul Pogba aliitwa na Sir Alex Ferguson mpuuzi leo zaidi ya mashabiki milioni 500 wanaimba Pogback, akiondoka tu utasikia kejeli zao, eti tulikuwaga na Ronaldo na aliondoka sembuse Di Maria?
Tena watakwambia tuna pesa za kumtengeneza nyota mwingine kama wewe. Thamani ya Fellaini imeonekana ndani ya mechi tatu. Ona wanavyomsifia?
Fellaini aliyetukanwa miaka mitatu? Ona wamesahau kuwa walimwita mzigo? Mzembe? Mzito? Manywele mengi hana akili?
Hii ndio ardhi ya lawama na sifa! Ndani ya Old Trafford kupewa sifa hata kwa kucheza dakika 10 ni kawaida. Unaweza kucheza dakika saba na wakakuita Pele mpya. Alikuja Fredrico Macheda... Unamkumbuka? Aliyedanganywa na Fergie kuwa atasomeshwa bure na familia yake kuhamishiwa England? Mchezo wa dhidi ya Aston Villa ulimfanya aonekana Dwight York ama Andy Cole mpya.
Pogba kulia
Yuko wapi Macheda? Yupo wapi Radamel Falcao aliyevunja rekodi ya vichwa vya habari kwenye mitandao hata kabla ya kutua ardhi ya England?
Alikuja Javier Hernández ‘Chicharito’ wakamwita Ruud van Nistelrooy mpya alipewa sifa zote. Leo Chicharito kapita kama upepo alikuja Robin van Persie ‘RVP’ dunia nzima ilisimama kwa miezi minane pale alipoibeba United na kuipa ubingwa. Ameondoka nani anamkumbuka?
Ukumbukwe kisa mabao 20? Kisa kombe moja? Hapana aameondoka Ryan Giggs juzi kwa kugomea ajira United, kila mtu anamnyooshea kidole kama msaliti.
Hizi ni salamu zangu kwa Fellaini. Leo watakutuza kama Wayahudi walivyompokea Yesu kule Yerusalemu. Jana tulimwita Martial mkombozi leo tunamwona Yuda. Maisha yakibadilika ndani ya Old Trafford uwe na uhakika wa njia mbadala.
Post a Comment