MADRID,
HISPANIA
CRISTIANO RONALDO (pichani) amesema anataka
kuitumikia Real Madrid kwa miaka mingine 10 ili astaafu akiwa na umri wa miaka 41.Ronaldo mwenye umri wa miaka 31, Alhamisi wiki hii alishinda zawadi ya Mchezaji Bora wa Ulaya baada ya kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa akiwa na Madrid na Kombe la Ulaya (Euro 2016) akiwa na timu yake ya taifa ya Ureno.
Gazeti la Marca, limeripoti kwamba Madrid inaangalia uwezekano wa kumuongezea mkataba straika huyo, kwa kuwa mkataba wa sasa utakwisha Juni 2018, ukiwa umebakisha kama misimu miwili na Ronaldo alisema: "Hilo ndilo ninalolitaka.”
"Nipo katika klabu bora duniani na nataka kuachana na klabu hii nikiwa na umri wa miaka 41. Kwa sasa nahitaji kuwa mtulivu lakini lengo ni kuongeza mkataba wangu na kubaki katika klabu ninayoipenda sana."
Ronaldo amefunga mabao 51 na kutengeneza 13 katika michezo 48 katika mashindano yote katika klabu yake msimu uliopita.
"Nataka kudumu katika hatua hii," alisema. "Nitapamabana kufanikisha hilo kama nilivyokuwa nikifanya kila mwaka. Sitaki kumwangalia mtu mwingine yeyote, nitajihamasisha mwenyewe. Kile ninachotaka ni kuwa mshindani kwa mwaka mwingine."
Real Madrid ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Barcelona katika Ligi ya Hispania, La Liga lakini ilifanikiwa kunyakua taji lake la 11 la Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa na Ronaldo ambaye alifunga penalti ya ushindi katika mchezo wa fainali dhidi ya Atletico Madrid.
Baadaye Ronaldo akiwa nahodha aliiongoza Ureno katika michuano ya Euro 2016 na kupata taji la kwanza kubwa, ingawaje alitolewa mapema baada ya kuumia katika mchezowa fainali dhidi ya wenyeji Ufaransa.
"Kwa kufanikiwa kusanya yote, ulikuwa ni msimu bora katika kazi yangu," alisema Ronaldo.
"Ninajivunia nimeshinda Euro na Ligi ya Mabingwa. Nililia baada ya kushinda mataji hayo. Lakini nataka kushinda mataji zaidi. Nataka kushinda taji la Ligi ya La Liga, Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa na kwenda Kombe la Dunia nikiwa na Ureno."
Ronaldo ni mfungaji wa muda wote wa Real akiwa na mabao 362 katika michezo 342 katika masimu minane na Madrid.
Mchezaji huyo anatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza wa nyumbani wa msimu huu dhidi ya Celta Vigo, Jumamosi baada ya kupona majeraha ya goti.
Post a Comment