LONDON,
ENGLAND
ARSENE
WENGER amemfanyia kitu mbaya staa wake
wa zamani, Thierry Henry ambaye alikuwa
kocha wa vijana chini ya umri wa miaka 18 wa klabu ya Arsenal.
Wenger
alimwambia Henry aamue jambo moja kati ya kuendelea kuwa mchambuzi wa soka
katika Kituo cha Skysport anakolipwa dau la Pauni 4 milioni kwa mwaka, au
aendelee kuwa kocha wa vijana wa Arsenal chini ya umri wa miaka 18.
Henry
ambaye alikuwa anafanya kazi siku nne kwa wiki katika kikosi hicho cha vijana
ameamua kuachana na kazi hiyo na kuendelea kuchambua soka huku ikidaiwa kuwa
atafanya katika klabu nyingine za London.
“Ningependa
kumshukuru Andries Jonker kwa kunipa nafasi ya kufundisha U18 Arsenal, nilihisi
heshima kubwa na nilikubali. Hata hivyo naheshimu maamuzi ya Arsene Wenger na
nataka kumtakia kila la kheri kocha wao, Kwame Ampadu, wachezaji na kila mmoja
klabuni. Kila la kheri kwa msimu wao mpya.” Ilisema taarifa ya Henry.
Kuonyesha
kuwa alikuwa na mapenzi na Arsenal huku pesa ikiwa sio tatizo kwake baada ya
kuvuna utajiri mkubwa katika maisha yake ya soka, Henry aliwapa Arsenal ofa ya
kuifundisha timu hiyo bure bila ya malipo yoyote lakini bado Wenger amempa
sharti hilo.
Habari
za ndani zinadai kwamba Wenger alikerwa na kitendo cha Henry kumkosoa vikali
mshambuliaji wake namba moja wa sasa, Olivier Giroud huku akidai kwamba Arsenal
haitaweza kutoa ushindani wa kuchukua ubingwa wa England kama Giroud ataendelea
kuwa mshambuliaji namba moja klabuni hapo.
Wenger,
ambaye yeye mwenyewe amekuwa akifanya kazi ya uchambuzi wa michuano mikubwa
katika kituo cha beIN Sports cha Ufaransa timu yake ilimaliza nyuma ya mabingwa
Leicester City pointi 10 nyuma ya wababe hao wapya.
Watu
wenye ushawishi mkubwa ndani ya Arsenal inasemekana wameshtushwa na kitendo cha
Wenger kumuonyesha mlango wa kutokea nyota huyo ambaye ni mfungaji bora wa muda
wote Arsenal huku pia akitajwa kuwa mchezaji bora wa muda wote kuwahi kutokea
Arsenal.
Indaiwa
pia kuwa Wenger, ambaye amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa
alikuwa na wasiwasi kuwa Henry alikuwa anainyemelea nafasi yake klabuni hapo
wakati huu mashabiki wa Arsenal wakishinikiza mastaa wa zamani wapewe nafasi ya
kuifundisha Arsenal.
Kwa
kuondoka Arsenal pia, nyota huyo anaungana na mastaa wa zamani wa Arsenal ambao
wameamua kufanya kazi kwingineko licha ya umaarufu mkubwa walioupata Highbury
kisha Emirates. Mastaa hao ni kama vile, Patrick Vieira, Dennis Bergkamp, Marc
Overmars na Mikel Arteta ambaye amestaafu soka mwishoni mwa msimu uliopita na
amejiunga katika benchi la ufundi la kocha, Pep Guardiola.
Mlinzi
wa zamani na nahodha wa muda mrefu wa Arsenal, Tony Adams hivi karibuni
alikubali kuwa msaidizi katika timu ya vijana ya Arsenal na alitarajiwa kufanya
kazi sambamba na Henry ambaye sasa ameamua kuondoka.
Henry
anaondoka Ligi Kuu ya England akiwa na mataji mawili ya Ligi Kuu ya England,
matatu ya FA huku akifunga mabao 228 katika mechi 376 na hivyo kuwa mfungaji
bora wa muda wote katika historia ya Arsenal. Alinunuliwa rasmi Arsenal Agosti
3, 1999 kwa dau la Pauni 11 milioni akitokea Juventus kwa ajili ya kuungana na
Wenger ambaye aliwahi kumfundisha Monaco.
Post a Comment