0


LONDON, ENGLAND
CLAUDIO RANIERI amekiri kwamba hana nguvu ya kumzuia N’Golo Kante asiondoke Leicester City anapotakiwa na mtu mwenye pesa kama bilionea Roman Abramovich.
Ndiyo hivyo, kiungo huyo Mfaransa anaondoka na dili lake la kutua Chelsea linaweza kukamilika muda wowote. Ripoti zinafichua kwamba Kante mwenyewe amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano katika klabu hiyo ya Stamford Bridge.

Mkataba wa Kante klabuni Leicester City unahitaji kulipiwa Pauni 24 milioni tu ili kuvunjwa kwa timu itakayohitaji huduma yake, lakini Chelsea wamesema kwamba watalipa Pauni 29 milioni kuinasa saini ya kiungo huyo matata wa kukaba.
Radio moja imefichua kwamba kila kitu kimeshafikiwa makubaliano na Kante ataanguka wino klabuni Chelsea kwa kusaini mkataba wa miaka mitano akichana na uzi wa bluu wa Leicester City na kuvaa bluu nyingine ya Stamford Bridge.
Ranieri alisema kila kitu kitaamriwa na Kante mwenyewe kama atataka kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa England au ataamua kwenda Stamford Bridge kuungana na Antonio Conte, ambaye ni kocha wa Chelsea.
Hata hivyo, kitendo cha Kante kwenda Chelsea kinamfanya asishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa kuwa timu hiyo ilishindwa kumaliza ndani ya nne bora kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.

Conte anataka kutengeneza mazingira mazuri katika kiungo ya timu hiyo kwa kumnasa Kante na hivyo kufanya ushindani wa namba kutarajiwa kuwa mkubwa baada ya uwepo wa Nemanja Matic. Usajili pekee wa maana iliyokuwa umefanya Chelsea kabla ya kuhangaikia dili la Kante ni wakati walipomnasa straika wa Ubelgiji, Michy Batshuayi kutoka Marseille ya Ufaransa.
Chelsea inamsaka pia beki wa kati Kalidou Koulibaly na kama nyota huyo atatua jambo hilo litamfanya Conte kuweza kutumia mfumo wake ambao alitamba nao kwenye vikosi vya Juventus na Italia alivyowahi kuvinoa. Fomesheni inayopendwa na Conte ni 3-4-3.

Post a Comment

 
Top