LISBON, URENO
CRISTIANO
RONALDO na wenzake wa Ureno wamewasili nyumbani
katika Jiji la Lisbon baada ya kuushtua ulimwengu kwa kutwaa taji
la Euro 2016.
Taji hilo halikuwa mbali ya mikono
ya nahodha Ronaldo, ambaye pamoja na
kikosi kizima kilipewa mapokezi makubwa baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Humberto Delgado.Mara baada ya kutua, ndege yao ilipokelewa kwa kurushwa maji yenye rangi nyekundu na kijani juu ya ndege hiyo.
Kwa ushindi huo ambao haukutarajiwa ulilazimisha kujengwa kwa uzio mzito katika mapokezi hayo ya Lisbon, ambapo maelfu ya mashabiki walifurika mitaani, wakicheza, wakiimba na kupunga mikono wakiwa na bendera za Ureno zenye rangi nyekundu na kijani.
Sherehe ziliendelea Jumatatu, na Ronaldo na wenzake walitua katika uwanja huo wa ndege saa 5:15 na kwenda kumuona Rais, Marcelo Rebelo de Sousa katika makazi yake ya serikali kabla ya gwaride kuingia katika mitaa ya Lisbon.
Na Rais alisema : " Sisi ndio bora Ulaya. Tumeonyesha kile tulichokifanya: nguvu, umoja, tumeweza kushinda mambo yote magumu ikiwemo kuumizwa na kumkosa Cristiano Ronaldo."
Ndoto za Ureno kulibeba taji hilo ziliingia katika wasiwasi mkubwa baada ya Ronaldo kuumizwa, nahodha na hirizi hiyo ya Ureno, alianguka uwanjani katika dakika ya nane kufuatia kuumizwa na Dimitri Payet.
Baada ya kutibiwa mara mbili na kujaribu kurudi uwanjani, Ronaldo alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa.
Ufaransa iliendelea kutawala mchezo dhidi ya Ureno na pongezi ziende kwa mchezaji bora wa mechi, beki Pepe na kipa Rui Patricio aliyeokoa hatari kadhaa.
Katika hatua nyingine, Ronaldo alisema: " Haikuwa fainali niliyoitaka lakini nina furaha kubwa. Ni Kombe la Wareno wote, kwa wahamiaji wote, kwa watu wote waliotuamini, kwa hiyo nina furaha na ninajivunia."
Post a Comment