0


PARIS, UFARANSA
SHUJAA wa Ureno katika fainali ya Euro 2016, Eder amesema  nahodha wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo alimwambia atafunga bao la ushindi dhidi ya  Ufaransa.
Na kweli ameipa heshima nchi yake baada ya ushindi wa kihostoria wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji uwanjani Stade de France Jumapili.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 aliingia uwanjani dakika ya 79 kuchukua nafasi ya kiungo, Renato Sanches na akapiga shuti la mbali  na kumfunga kipa wa Ufaransa, Hugo Lloris katika dakika ya 109 na kuipa ubingwa mkubwa wa kwanza Ureno.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Eder anayekipiga  katika klabu ya Lille aliweka wazi kwamba nyota wa Real Madrid, aliyelazimika kutoka nje katika dakika ya 25 kufuatia kuumia goti alimtabiri bao hilo kabla ya muda.
"Cristiano aliniambia nitafunga bao la ushindi,” alisema Eder na kudai kuwa  wenzake wengine walikuwa wakimtia nguvu.
"Yeye (Ronaldo) alinitia nguvu na kwa mtazamo chanya. Na bao lile lilikuwa muhimu.

Eder alicheza kwa dakika 13 katika mashindano hayo ya Euro  kabla ya mchezo huo wa fainali, alisema  alikuwa akiamini siku zote kwamba muda wake wa kufanya madhara utafika tu.
"Tangu siku ya kwanza (nilifikiria nafasi yangu itafika). Tangu (kocha) Fernando Santos aliponiita kwenye timu alifahamu uwezo wangu kama ilivyokuwa kwa kundi zima," Eder alisema.
"Wananiamini na nilifanya kazi kwa nguvu zangu kuchangia na leo na imewezekana. Nina furaha kwa kile tulichofanikiwa."
Aliongeza: "Ulikuwa wakati wa maajabu. Timu yetu ilipigana kwa nguvu.  Tulikuwa tunafahamu kwamba watu wa Ureno walikuwa pamoja  nasi.

"Tulipambana kwa nguvu zote, tulikuwa watu wa ajabu. Nadhani tulistahili taji hili kutokana na kazi tuliyoifanya, wachezaji wote na wafanyakazi. Ureno imekuwa ikisubiri taji hili kwa muda mrefu.

Post a Comment

 
Top