0


MANCHESTER, ENGLAND
SIR ALEX FERGUSON kocha wa zamani wa Manchester United amempaisha  nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo kuwa ni mchezaji maalumu wa kizazi cha sasa.
Ronaldo, 31, ameshinda Ligi Mabingwa na mataji matatu Ligi Kuu katika miaka sita ya mafanikio chini ya Ferguson uwanjani Old Trafford, na ameshinda mataji mawili zaidi ya Ligi ya Mabingwa akiwa na Real Madrid kabla Ureno kushinda taji la Euro 2016 mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ferguson anaamini kwamba kitendo cha Ronaldo kupenda mazoezi, nje ya muda wa kawaida, kinamfanya kuwa juu ya wachezaji wengine.
"Ana mwili mzuri wa kimichezo.  Uwezo wake umekuwa ukiongeza kiasi cha kushangaza," Ferguson aliliambia Gazeti la Bild.
"Na hakuna cha ajabu kwa kuwa soka la sasa ni la ridhaa zaidi na la haraka.
"Kwa kawaida hutokea wachezaji wanaotamba kwa miaka mitano hadi sita kwa kucheza katika kiwango cha juu, kisha wanapotea. Cristiano amekuwa katika ubora wake kwa zaidi ya miaka 10.  Hilo linamfanya kuwa wa kipekee.
"Kila kizazi kinakuwa na mchezaji wake maalumu: Cristiano ni wa kizazi cha sasa."

Akizungumzia walipokuwa pamoja na mchezaji huyo United, Ferguson alisema kiu ya Ronaldo ilikuwa kujituma kitu kilichomfanya kuwa mchezaji bora wa klabu.
"Ana hamu ya ajabu katika soka," aliongeza Ferguson. "Cristiano alikuwa mbele katika kila mazoezi. Kila siku alikuwa anataka kuwa bora, kushinda. Amekuwa akipenda michezo mikubwa kama hii.
"Wakati wangu pale Manchester United, Cristiano alikuwa mchezaji bora na mwenye maendeleo zaidi. Kutokana na kujituma, amekuwa akijifunza mbinu za kupiga mashuti, kwa mguu wa kulia na wa kushoto, uwezo wake wa kupiga mipira ya vichwa na mipira inayorudi kwa kipa."

Ferguson alipigwa picha Jumapili iliyopita akimkumbatia Ronaldo baada ya mchezaji huyo kutwaa taji la Euro 2016.

Post a Comment

 
Top