MADRID,
HISPANIA
KUNA
aliyesema hauwezi kuwa adui kwa kusema ukweli. Na kuna mwingine aliyesema sema
kweli utakuweka huru. Neymar ameamua kusema kweli na kuepuka unafiki wakati
alipoamua kutabiri mwanasoka bora ajaye wa dunia.
Staa
huyu wa Barcelona licha ya kuwa rafiki wa Lionel Messi huku akikiri kipaji
chake katika mahojiano yake mengi ya nyuma, lakini amekiri kwamba safari hii,
staa wa wapinzani wao, Real Madrid, Cristiano Ronaldo anastahili kuwa mwanasoka
bora wa dunia.
Ronaldo
alitwaa ubingwa wa Ulaya Mei mwaka huu na kikosi cha Real Madrid baada ya
kuichapa Atletico Madrid kwa matuta dimba la San Siro, lakini pia amefanikiwa
kuipa Ureno taji lake la kwanza la kimataifa baada ya kutwaa Euro wiki mbili zilizopita
katika Uwanja wa Stade De France jijini Paris wakishinda bao 1-0.
Katika
mchuano uliopita wa kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa dunia Januari mwaka huu
jijini Zurich, Ronaldo alishika nafasi ya pili nyuma ya hasimu wake, Lionel
Messi wa Argentina, huku Neymar akishika nafasi ya tatu, lakini Neymar
amefunguka na kudai kuwa anaamini Ronaldo yupo katika nafasi nzuri ya kushinda
tuzo hizo Januari mwakani.
“Kushinda
mataji kunakupa nafasi kubwa katika mbio za kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia.
Ronaldo alitwaa Ligi ya Mabingwa na sasa Euro 2016 pia. Nadhani yupo katika
nafasi nzuri. Ukijumlisha kwamba ni mchezaji mkubwa. Sina wasiwasi kusema
hilo,” alisema Neymar.
Kauli
hiyo ya Neymar ni mwendelezo wa kauli za mastaa wengi wanaoamini kuwa mwaka
2016 ni mwaka wa Ronaldo. Kiungo wa kimataifa wa Ufaransa na Juventus, Paul
Pogba naye amekiri kwamba Ronaldo ana nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hiyo.
“Una
Lionel Messi, una Ronaldo. Kusema kweli nawapenda wote. Griezmann pia amekuwa
na mwaka mzuri sana. Lakini kwangu, Cristiano Ronaldo inabidi ashinde kwa
sababu ametwaa Ligi ya Mabingwa na Euro 2016,” alisema Pogba.
Wakati
Griezmann akianza kupigiwa debe kwa kuingizwa katika orodha ya wanaotajwatajwa
kuwania tuzo hiyo, mwenyewe ameamua kujiweka kando na kukiri kwamba tuzo hiyo
ni kama vile tayari imechukuliwa na Ronaldo.
“Itakuja
kama imepangwa kuja. Bado nipo katika mbio? Ronaldo ameshinda michuano mikubwa
na nadhani tayari suala hilo limeshamalizika,” alisema Griezmann ambaye hata hivyo
alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Euro 2016 huku pia akitwaa Kiatu cha Dhahabu
kwa kufunga mabao sita.
Endapo
Ronaldo atatwaa tuzo hiyo Januari mwakani bado atakuwa hajamfikia hasimu wake,
Messi ambaye ametwaa tuzo hizo mara tano katika miaka ya 2009, 2010, 2011, 2012
na 2015. Ronaldo ametwaa tuzo hizo mara tatu katika miaka ya 2008, 2013 na 2014.
Hata
hivyo, huenda kukawa na mabadiliko katika eneo la wachezaji watatu watakaongia
katika tatu bora. Kuna uwezekano Neymar mwenyewe akachomoka katika nafasi hiyo
na Griezmann au mshambuliaji mwenzake wa Barcelona, Luis Suarez akaingia katika
tatu bora baada ya kumaliza akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Hispania.
Post a Comment