0


GOTHENBURG, SWEDEN
ZLATAN IBRAHIMOVIC amepiga bao la kideo ikiwa ni dakika tatu tu tangu ashuke uwanjani kuichezea timu yake mpya Manchester United katika mchezo wa kirafiki ambapo, kikosi hicho cha Jose Mourinho kiliichapa Galatasaray 5-2 mjini Gothenburg, Sweden juzi Jumamosi.
Ibra alipiga bao hilo kwa ‘tikitaka’ wakati alipounganisha krosi ya Antonio Valencia na mwisho wa mechi alisema anamsubiri Pogba Pogba atue kwenye kikosi hicho haraka ili wafanye kazi.
Mabao mengine ya Man United yalifungwa na Wayne Rooney, mawili na Juan Mata na Marouane Fellaini kila mmoja alifunga mara moja.
Kikosi cha Man United sasa kinaanza kunoga kiasi cha kumvutia kocha wa zamani wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson, ambaye pia ameunga mkono usajili wa Pogba.

Ferguson ameripotiwa kuunga mkono kwa asilimia 100 matumizi ya Pauni 100 milioni kuinasa saini ya Pogba baada ya kupata mlo wa usiku na Mourinho kwenye uwanja wa mazoezi wa kikosi hicho cha Man United huko Carrington na kukoshwa na mipango ya Mreno huyo.
Awali, kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda Ferguson akaweka ngumu usajili wa Pogba kwa sababu alitibuana na wakala wa mchezaji huyo wa wakala Mino Raiola na kusababisha kiungo huyo kutimkia Juventus miaka minne iliyopita.
Lakini, sasa amempa ruhusa Mourinho ajenge kikosi chake katika namna ambayo anadhani itafaa ili kurudisha heshima Old Trafford.

Wakati Ferguson akisapoti matumizi ya Pauni 100 milioni kwenye usajili wa Pogba, mkongwe mwenzake, Arsene Wenger anashangaa na kusema kutumia kiasi hicho cha pesa kwa mchezaji mmoja ni uchizi.
"Ni uchizi wa waziwazi kama utalichukulia suala hilo katika uhalisia wa maisha halisi. Ndiyo hivyo, lakini tatizo tunaishi kwenye dunia ambayo shughuli zake zote zimelenga kwenye kupata pesa nyingi," alisema Wenger.
"Tangu nilipoanza kuingia kwenye mchezo huu siku zote nilikuwa nikidhani rekodi si tu pesa kuwa nyingi, kumbe nilikuwa nakosea. Miaka michache ijayo mchezaji atakuwa Pauni 200 milioni au Pauni 300 milioni, nani anajua."

Post a Comment

 
Top