PARIS, UFARANSA
PAUL Pogba atasaini Manchester United, anafichua
hilo kinyozi wake.
Ripoti kutoka Ufaransa zinafichua kwamba Man United
imefikia makubaliano na Juventus kulipa ada ya Pauni 105 milioni kwa ajili ya
huduma ya kiungo huyo. Lakini, kinyozi wake aliweka mambo hadharani baada ya kutuma ujumbe katika moja ya mitandao yake ya kijamii
ikiambatana na picha akimnyoa staa huyo kwamba anambadilisha nywele Pogba kwa
ajili ya timu yake mpya ya Manchester United.
Kukamilika kwa usajili wa Pogba kunathibitisha
kwamba Manchester United msimu ujao haitaki mchezo kabisa. Ikiwa zimebaki wiki
tatu tu msimu mpya kuanza, kikosi hicho chini ya kocha wake Jose Mourinho
kimewasajili Zlatan Ibrahimovic, Henrikh Mkhitaryan na Eric Bailly kwa ajili ya
kikosi chao cha kwanza.
Juzi ilibainika kwamba Man United inachelewesha
kutaja namba za jezi za wachezaji wake ikisubiri dili la Pogba kukamilika
kwanza. Ujio wa Pogba utaifanya Man United kuwa na machaguo mengi tofauti ya
fomesheni zao zitakazotumiwa na Mourinho msimu ujao.
Kikosi hiki cha Man United kwa msimu ujao, sijui
labda usilete timu uwanjani, utapigwa tu.
Unamsikia Mourinho lakini unachosema? Mashabiki
wasubiri waone utamu.
FOMESHENI YA 4-2-3-1
Fomesheni hii ndiyo kipenzi cha kocha Jose Mourinho,
mara nyingi amekuwa akitumia 4-2-3-1. Alitumia fomesheni hiyo katika mechi yake
ya kwanza klabuni hapo ambapo Man United iliichapa Wigan kwenye mechi ya
kirafiki Jumamosi iliyopita. Wakati Michael Carrick akiwa na majukumu ya
kuwalinda mabeki wa kati, kwenye fomesheni hii Pogba, ambaye pia atacheza
kwenye kiungo ya kati atakuwa anafanya kazi moja tu ya kuwa kiunganishi wa
mipira kutoka kwenye ulinzi kuwafikia washambuliaji, ambapo mbele yao wakali
watatu watakaokuwa hapo ni Mkhitaryan, Wayne Rooney na Anthony Martial, wakati
straika atakayesimama mbele ni Zlatan Ibrahimovic. Martial na Marcus Rashford watakuwa
wakibadilishana na watabadilishwa kutokana na mpinzani, ama wacheze kulia au
kushoto.
FOMESHENI YA 4-3-1-2
Fomesheni hii ni ya mauaji. Kushambulia mwanzo
mwisho. Kwenye kiungo kunakuwa na wachezaji watatu, wote viungo wa nguvu ambapo
Carrick atacheza sambamba na Pogba na Bastian Schweinsteiger. Wote hao ni
mafundi wa pasi kali. Mbele yao atasimama kiboko ya pasi za mwisho, Mkhitaryan,
atakuwa hapo nyuma ya washambuliaji wawili wote moto, Ibrahimovic na Martial.
Kwenye fomesheni hii, Rooney na Rashford watakuwa wanasubiri kwenye benchi,
wakati kwenye sehemu ya kiungo Marouane Fellaini naye atakuwa anasubiri kwenye
benchi. Juan Mata, Ander Herrera na Memphis Depay hawa watakuwa wanasubiri
nafasi ya Mkhitaryan. Nakwambia Mourinho kama namwona na ule mdomo wake kwa
kikosi hicho alichonacho.
FOMESHENI YA 4-3-2-1
Fomesheni hii italenga kumpa Pogba uhuru zaidi wa
kutawala kwenye sehemu ya kiungo, wakati Wayne Rooney atapewa uhuru wa kutawala
kwenye eneo la mbele. Kwenye fomesheni hii, mabeki watatu kati ya wanne
watasimama kwenye mstari mmoja, wakati beki wa kulia atakuwa amesogea mbele
kidogo. Kwenye sehemu ya kiungo ambapo kutakuwa na wachezaji watatu, kushoto
atasimama Pogba na kulia atakuwa Rooney na katikati kwenye dimba atakuwa
Carrick. Pogba atakayekuwa kushoto, kazi yake itakuwa kutawala kwenye kiungo,
wakati Rooney kwenye upande wa kulia, atakuwa na kazi ya kutawala eneo la
mbele. Mbele ya wachezaji hao watatu kutakuwa na Martial na Mkhitaryan na
Martial na fowadi atakuwa Ibrahimovic. Fomesheni hii itawapa pia nafasi
Schweinsteiger, Morgan Schneiderlin, Herrera na Fellaini.
FOMESHENI YA 4-1-4-1
Hii fomesheni inaitwa unakaba uwanja mzima. Unakaba
mbele, unakaba nyuma. Fomesheni hiyo itatumika kwa timu ngumu kufungika, hapa
lazima utalegea tu.
Kwenye fomesheni hiyo baada ya mabeki wanne wa
kati, mbele yao atasimama kiungo Carrick, kisha unakuja ukuta mwingine wa
wachezaji wanne ambao watakuwa Mkhitaryan, Pogba, Rooney na Martial. Hapa nyota
hao wote wana uwezo wa kukaba na kushambulia. Mbele kabisa atasimama
Ibrahimovic. Fomesheni hiyo, Carrick atakuwa na kazi moja tu ya kumalizana na
mipira ile inayowapita Rooney na Pogba na kisha kupokea mipira kutoka kwenye
safu ya ulinzi kuwapishitia wachezaji wa mbele. Mfumo huo utawabana kidogo
Martial na Mkhitaryan, lakini utawaacha huru Pogba na Rooney, wote ni aina ya
wachezaji wenye nguvu ambao Mourinho ndio anawataka zaidi.
Kwa fomesheni hizo zote, unaweza kuona Mourinho si
shabiki wa wachezaji kama Herrera, Mata na Depay, hivyo kupata namba
watalazimika kujipanga sana na kuhakikisha kwamba wanakuwa na kitu cha ziada
cha kuifanyia timu, la muda mwingi utawakuta kwenye benchi.
Post a Comment