0



MICHIGAN, MAREKANI
ANTONIO CONTE amekiri kwa mara ya kwanza kwamba hana uhakika kama straika wake, Diego Costa atabaki Chelsea.
 Costa hakucheza mchezo wa ambao timu yake ilifungwa mabao 3-2 Jumamosi usiku dhidi ya Real Madrid  jijini Michigan kwa sababu ya kuwa na maumivu ya mgongo na hakuweza kushiriki mazoezi kwa muda mrefu.
Chelsea iko karibu kukamilisha dili la Pauni 60 milioni la kumrudisha straika wake wa zamani, Romelu Lukaku kutoka Everton lakini  mustakabali wa Costa unabaki kuwa wazi kwa Atletico Madrid ambayo ina mkakati wa kumrudisha katika klabu hiyo ya Hispania.

“Ninachoweza kusema leo, Costa ni mchezaji wa Chelsea,” alisema Conte. “Hakuweza kucheza katika mchezo huu kwa sababau ya majeraha na kama atapona  na akiwa  katrika hali nzuri mazoezini atacheza dhidi ya Milan.
“Lakini ni hicho tu ninachoweza kukisema. Nazungumza tu kuhusu  leo na leo Costa ni mchezaji wa Chelsea. Kama mtaniuliza kuhusu kesho kama Costa atabaki nasi, hilo silifahamu.”

Hata hivyo, Atletico Madrid hivi karibuni ilimsajili straika wa Sevila na timu ya taifa ya Ufaransa, Kevin Gameiro kwa Pauni 28 milioni kitu kinachoonekana kumaliza tamaa yao ya kumtaka Costa, ambaye alikuwa na nafasi kubwa kurudi Madrid.
Kocha Conte alisema atakutana uso kwa uso na Bodi ya Chelsea baada ya ziara ya Marekani na kutoa ripoti ya wachezaji anaotaka kubaki nao na wale wa kuuzwa na kutolewa mkopo.
“Kuna wachezaji watabaki na wengine wataondoka,” alisema Mtaliano huyo.
Beki wa kushoto raia wa Ghana, Baba Rahman tayari imefahamika kwamba atajiunga kwa mkopo wa msimu mmoja na Schalke.

Lukaku aliichezea Everton katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Real Betis Jumamosi pamoja na kwamba Chelsea ina uhakika na dau lake ililoliweka kwa Mbelgiji huyo ambaye amestaafu kuichezea timu yake ya taifa, baada ya kumuuza miaka miwili iliyopita kwa Pauni 28 milioni.
“Sitaki kuwazungumzia wachezaji wa timu nyingine,” alisema Conte, alipoulizwa kuhusu Lukaku. 
“Hii siyo heshima kwa klabu au kwa wachezaji hao. Nimeamua kutowazungumzia.”

Mara kadhaa Costa amekuwa akiripotiwa kutaka kuondoka na Kocha Conte amekuwa na wasiwasi wa kuimarisha safu yake ya ushambuliji katika kikosi chake.
Awali, Conte alijaribu kuwasajili mastraika, Gonzalo Higuain, Edinson Cavani au Alvaro Morata lakini alifeli.

Post a Comment

 
Top