0


NA ABEID POLO
WAYNE Rooney anasubiri kuzaliwa upya msimu ujao. Maisha yake ya ndani ya Man United yatakuwa matamu zaidi kama Jose Mourinho atatua mahali hapo. Rooney ni aina ya mchezaji ambaye Mourinho alipenda sana afanye naye kazi.
Wakati alipokuwa Chelsea, Mourinho mara kadhaa alisikitika kuikosa huduma ya Wayne Rooney. Sikitiko lake Mourinho ni kwamba hakuwa na Namba 10 aliyemhitaji klabuni hapo, ambaye angecheza kama Rooney.
Rooney ni mchezaji ambaye alikuwa na uwezo wa kupokea pasi, akaimalizia vizuri kuwa bao. Ni mchezaji mwenye uwezo kurudi nyuma kukaba. Mchezaji anayeweza kufuata maelekezo vizuri na si mbinafsi. Mourinho hakuwa na mtu wa aina hiyo kwenye kikosi chake cha Chelsea baada ya kina Frank Lampard kuondoka. Ndiyo maana alimhitaji sana Rooney. Sasa maisha ya wawili hao yatakuwa matamu zaidi watakapokutana Old Trafford msimu ujao.

Mourinho, anatarajiwa kutua Old Trafford.
Mourinho shida yake anamtaka namba 10 anayekaba pia. Kwenye kikosi cha Chelsea alikuwa na Eden Hazard, Kevin De Bruyne, Pedro, Willian, Andre Schurrle, Oscar na Juan Cuadrado, hawa kwa nyakati tofauti aliwahi kuwachezesha kwenye namba 10. Matokeo yake hayakuwa matamu sana na ndiyo maana mara nyingi alihusudu kuwa na huduma ya Rooney kwenye kikosi chake. Jambo hilo ndilo linaloyafanya maisha ya Rooney kutarajiwa kuwa tofauti msimu ujao. Man United kwa sasa inakokotoa hesabu za fidia itakazomlipa kocha wake wa sasa, Louis van Gaal ili kumpisha Mourinho klabuni hapo.
 United inatambua kwamba kumwondoa Van Gaal kwa sasa kutawaingiza kwenye gharama kubwa zaidi kwa sababu italazimika kumlipa kwa muda wote wa mkataba wake uliobaki na ndio maana inasubiri hadi mwishoni  mwa msimu kuona timu itakuwa imemaliza kwenye nafasi gani na kufanya uamuzi.
Kwa kipindi hicho italazimika kumlipa asilimia 15 ya sehemu ya mkataba uliobaki kama fidia.
Man United inafahamu wazi kuendelea kuwa na Mdachi huyo kuna baadhi ya wachezaji mastaa haitaweza kuwapata. Mmoja wapo ni Zlatan Ibrahimovic. Baada ya kile kilichotokea kwa mastaa wengine makini wa Man United, kama Angel Di Maria, wachezaji wengi wanaogopa kwenda kuwa chini ya Mdachi huyo.

Rooney na Van Gaal
Hivi karibuni, Man United iliwafuatilia wachezaji Renato Sanches, Bernardo Silva na Andre Gomes wakiwataka wachezaji hao wajiunge na timu yao msimu ujao. Lakini, tatizo lililopo ni kwamba wachezaji hao wapo chini ya wakala Jerge Mendes na Mreno huyo hayupo tayari kufanya biashara na kuwapeleka nyota wake kuwa chini ya kocha huyo hasa baada ya kile kilichotokea kwa Di Maria na Falcao.
Man United itaweza kupata huduma za wachezaji hao kama tu kocha wao atakuwa Mourinho. Ujio wa Mourinho pia utawavutia mastaa wengine wa maana kwenda kujiunga na timu hiyo ya Old Trafford huku kukiwa na matarajio ya kumshuhudia Rooney kwenye ubora wake mpya.

Post a Comment

 
Top