0


BARCELONA, HISPANIA
MKATABA wa Neymar umevuja. Football Leaks, ambao ndio waliovujisha mikataba ya Gareth Bale, Sergio Aguero na Anthony Martial, imevujisha kurasa nyingine 13 zilizosainiwa na nyota wa Samba mwaka  2013 pindi alipojiunga na Barca.
 Habari hiyo ya kushtua kama siyo kushangaza inaonesha nyota  mwenye umri wa miaka 24 ambaye aliwahi kuwindwa na Manchester United anachukua kiasi kidogo cha mshahara kuliko nyuta wa juu wanaolipwa zaidi Ligi Kuu England.
Mshahara wa Neymar unakaribia kuwa zaidi ya Pauni 4 milioni. Wayne Rooney anachukua Pauni 13.5 milioni kwa mwaka  wakati wakali wa Manchester City, Sergio Aguero na Yaya Toure wanaingiza Pauni 12.5 milioni.
Mkataba huo wa Neymar umesainiwa na Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu na  mtanguzili wake, Sandro Rosell.
Mtandao wa Football Leaks umeweka hadharani vipengele vya mkataba wa staa huyo wa Kimataifa wa Brazil ambaye ni mmoja kati ya wanasoka wanaolipwa zaidi duniani kwa sasa akiwa amehamia Barcelona kutoka Santos Juni 2013 kwa mkataba wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Neymar atalipwa mshahara wa Euro 5 milioni kwa msimu ingawa kuna bonasi nyingi ambazo zitaongezeka kiasi cha kufikia Euro 49 milioni kwa muda wote wa mkataba wake.

Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa staa huyo wa Brazil kumbe alipokea dau la Euro 8.5 milioni kama ada ya uhamisho wake huku pia ikithibitisha kwamba kuna kipengele kinachomruhusu mchezaji huyo kuondoka Nou Camp kama kuna timu ikilipa Euro 190 milioni.
Kipengele hicho kinaweza kufikiwa na timu mbili tajiri kwa sasa ambazo ni PSG na Manchester City na kumekuwa na hofu kwa mabosi wa Nou Camp kwamba huenda timu hizo zikafanya kweli mwishoni mwa msimu huu na kumchukua mchezaji huyo ambaye alinunuliwa kwa ajili ya kuwa mbadala wa muda mrefu wa staa wao Lionel messi.

Neymar mshindi wa tatu wa Ballon D'or
Neymar, ambaye alimaliza nafasi ya tatu katika tuzo za kuwania mwanasoka bora wa dunia mwaka 2015 ana kipengele ambacho kinaonyesha kuwa atapewa kiasi cha Euro 425,000 kama akifanikiwa kutwaa tuzo hizo.
Kuna vipengele vingine ambavyo vinampa Neymar pesa nyingi nje ya mshahara wake. kama Barcelona ikitwaa taji la La Liga, Barcelona wanalazimika kumlipa Neymar kiasi cha euro 637,500. Kama Barcelona wakitwaa ubingwa wa Ulaya basi wanalazimika kumlipa Neymar Euro 850,000 na kama wakitwaa kombe la Mfalme basi watamlipa Euro 850,000.
Mpaka sasa Barcelona ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa mataji yote hayo matatu na kama hilo likitokea, basi watalazimika kumlipa bonasi ya Euro 1.7 milioni, na kama wakitwaa na ubingwa wa Ulaya na Kombe la Mfalme basi atapata kiasi cha Euro 1,062,500.
Mkataba wa Messi uliovuja ni ule mpya aliosaini na wababe hao wa Catalunya mnamo mwaka 2014 ambao unatazamiwa kumuweka klabuni hapo mpaka Juni 30, 2018.
Mkataba huo una kipengele ambacho kinamruhusu Messi kuondoka klabuni hapo kwa dau la Euro 250 milioni kwa timu yoyote inayomtaka.
Kwa msimu huu mshahara wa Messi ni Euro 22.8 milioni. Hata hivyo kwa mujibu wa mkataba, dau hilo linatazamiwa kuongezeka mpaka kufikia Euro 39.4 milioni katika dirisha la majira ya joto.

Barcelona pia ipo katika mtego mkubwa katika namna ya kumuuza Messi kabla ya dau lake la mshahara halijapanda msimu ujao. Kama itaamua kumuuza kabla ya mshahara wake mpya kuanza kutumika basi italazimika kumlipa fidia ya Euro 19.9 milioni. Kama itaamua kumuuza msimu ujao basi fidia hiyo kwa Messi itapungua kufikia Euro 9.97 milioni.

Post a Comment

 
Top