0



MANCHESTER, ENGLAND
YAYA TOURE kiungo wa kimataifa wa kimataifa wa Ivory Coast ameamua kama mbwai na iwe mbwai (kama ubaya ni ubaya tu),   anataka kuwa mchezaji wa kwanza mwenye jina kubwa kutoa pesa na kuununua mkataba wake mwenyewe.
 Kiungo huyo atafanya hivyo kama Manchester City italazimisha kumbakisha katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake.
Manchester City imegoma kumpa staa huyo wa kimataifa wa Ivory Coast mkataba wa miaka mitatu na sasa Toure na wakala wake, Dimitri Seluk wanataka kutumia kipengele cha kanuni moja za Fifa kununua mkataba huo ili awe huru mwishoni mwa msimu.

Mpaka sasa, klabu haoneshi kama inamhitaji.
Seluk amedai kwamba Mkurugenzi wa Ufundi wa Man City, Txiki Begiristain, amevunja ahadi mbili alizoweka kwao kuhusu mazungumzo ya mkataba mpya na sasa amewapa City kufanya uamuzi wa mambo mawili.
Kwanza anawataka Man City wamuache huru staa huyo mwenye umri wa miaka 32 katika dirisha kubwa la majira ya joto baada ya Toure kuwatumikia kikamilifu kwa miaka sita aliyocheza Etihad.
Kwa kufanya hivyo hatasaini timu nyingine ya Ligi Kuu England.
Lakini chaguo la pili ni kwa Toure kutumia kipengele namba 17 cha uhamisho Fifa kuilipa fidia Man City kwa kununua miezi 12 iliyobaki katika mkataba wake. Kwa sasa Toure analipwa dau la Pauni 230,000 kwa wiki Etihad ikiwa ni karibu na mshahara wa Pauni 12 milioni kwa mwaka.

Yaya amebakisha mwaka mmoja Man City.
Klabu hiyo imeweka bayana kwamba haitaongeza mkataba wa Toure tena kufuatia kuwasili kwa Pep Guardiola.
Hata hivyo, Seluk anaamini kuwa wanaweza kuilipa City chini ya Pauni 10 milioni kama watafikia makubaliano na baada ya hapo Toure atakuwa huru kufanya mazungumzo na klabu yoyote inayomtaka kama mchezaji huru.
“Niliongea na City kuhusu mkataba mpya na walisema nisubiri mpaka Desemba. Niliongea nao Desemba wakasema nisubiri mpaka Machi. Na sasa wanasema Yaya asubiri mpaka mwishoni mwa msimu. Hili halikubaliki. Mchezaji kama Yaya Toure hapaswi kwenda mpaka mwisho wa mkataba wake huku akijiuliza kama atapewa mkataba mpya.
 “Yaya ana 32 na amebakisha miaka mitatu au minne ya kucheza katika kiwango cha juu na City lazima imwambie inachotaka kufanya. Mawazo mazuri yalikuwa ni kumpa Yaya mkataba wa miaka mitatu ili amalizie maisha yake ya soka City. Kingine ni kumwambia ‘Asante sana’ na kumruhusu aondoke.

Guardiola ambaye atatua Man City.
“Baada ya hapo Yaya anaweza kucheza kwa misimu mitatu katika klabu nyingine kubwa. Bado anaamini anaweza kutwaa taji jingine la ubingwa wa Ulaya. Sitamruhusu Yaya apoteze mwaka mwingine City. Sitairuhusu City imuweke kwa mwaka mmoja mwingine kwa sababu baada ya hapo nafasi ya kujiunga na timu kubwa itakuwa ndogo.
“Nitakwenda Fifa. Nitawaandikia na kuwaambia kuwa Yaya atanunua mkataba wake na tunaweza kufanya hivyo. Ni chaguo letu. Hili sio tishio. Nakuahidi kuwa ataondoka City mwishoni mwa msimu huu na hakutakuwa na kitu ambacho Sheikh Mansour anaweza kufanya,” alisema Sulek.
Kwa mara ya kwanza kipengele hicho cha Fifa kilitumika mwaka 2006 na beki wa Scotland, Andy Walker wakati alipoamua kununua mkataba wake katika klabu ya Hearts ya Scotland na kujiunga na Wigan.
Hata hivyo, wachezaji wengi wakubwa wameamua kutotumia kipengele hicho na badala yake wanavutiwa na mpango wa kumaliza mkataba na kuwa huru.

Seluk
“Yaya hatajiunga na klabu nyingine ya England. Watu wengine England ambao wanajifanya wapo karibu na Yaya wanasema kuna uwezekano huo, lakini hawaongei kwa niaba yake. Maneno ya kuaminika ni yale ninayoongea mimi au Yaya mwenyewe,” alimalizia wakala huyo matata.
Toure kwa sasa anaingiza Pauni 230,000 milioni kwa wiki  Etihad kama Pauni 12 milioni kwa mwaka  lakini Seluk amepiga hesabu na kusema anaweza kumtoa Yaya Man City kwa kutumia si zaidi ya Pauni 10 milioni.

Staa huyo wa zamani wa Barcelona na Monaco atakuwa huru kufanya majadiliano na klabu nyingine  na Seluk tayari amefuatwa na klabu zenye majina makubwa Ulaya.

Post a Comment

 
Top