0


MANCHESTER, ENGLAND
MANCHESTER United inamtaka straika Zlatan Ibrahimovic, lakini yeye ameiambia ni kocha Jose Mourinho peke yake ndiye atabadilisha maisha Old Trafford, la sivyo itakula kwao jambo linalowafanya kuwa na presha kwa sababu Real Madrid imeibuka na  inamtaka Mreno huyo.
“Jose anafanikiwa popote pale anakokwenda kuwa kocha, yupo hivyo. Namheshimu sana kwa sababu anazungumza chochote anachotaka, lakini ukimsikiliza siku zote yupo sahihi. Ni kocha mwenye ujuzi na anayejali," alisema Ibrahimovic kuhusu Mourinho.

Ibrahimovic
Hata hivyo, wakati Man United ikijiamini itawanasa mastaa hao wawili kwa mpigo mwisho wa msimu huu, Real Madrid imeibuka na kuweka wazi dhamira yao ya kumrudisha Mreno huyo Santiago Bernabeu kama watatupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne ijayo.
 Rais wa Real Madrid, Florentino Perez alishindwa kumrudisha Mourinho Januari mwaka huu wakati alipomtimua Rafa Benitez, lakini sasa anafikiria kumchukua na kuifanya Man United kuwa na presha.

Van Gaal
Real Madrid ikiwa chini ya Zinedine Zidane ilichapwa 2-0 na VfL Wolfsburg katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo bosi Perez ana wasiwasi huenda wakaishia kwenye hatua hiyo ya robo fainali na kufikiria kumpata kocha mwenye hadhi kubwa wa kiwango cha Mourinho.
Matumaini ya Man United ni kwamba Mourinho atagomea ofa hiyo ya Real Madrid ili atue kwenye kikosi chao, huku akiripotiwa kuanza kutafuta nyumba ya kuishi huko Cheshire, eneo maarufu lenye mastaa wengi wa Man United. 
Wakala wa Mourinho, Jorge Mendes aliripotiwa kuwa na kikao na Makamu Mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward juu ya kumchukua Mourinho awe kocha wao msimu ujao.
Man United inaripotiwa kujiandaa kuachana na kocha Louis van Gaal baada ya mambo kuonekana kwenda kinyume na matarajio licha ya kufanya usajili wa nguvu kwenye dirisha la usajili lililopita ambapo tangu Mdachi huyo atue Old Trafford, ametumia zaidi ya Pauni 250 milioni kufanya usajili.
United kwa sasa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ikipambana kusaka nafasi ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ambao  Jumapili itakuwa na shughuli pevu dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa ligi uwanjani White Hart-Lane.

Mourinho
Kikosi hicho kinahitaji kupata ushindi katika mechi zake zote zilizobaki ili kupenya ndani ya nne bora, kitu ambacho ndicho kitakachoifanya ifuzu kwa michuano ya Ulaya msimu ujao.
Ligi Kuu England itaendelea wikiendi hii, ambapo Jumamosi, Arsenal itakuwa ugenini kwa West Ham, Watford itacheza na Everton, Swansea na Chelsea, Southampton na Newcastle, Crystal Palace na Norwich City, Aston Villa na Bournemouth na Manchester City na West Brom, wakati mechi nyingine za  Jumapili ni Sunderland na vinara Leicester City na Liverpool na Stoke City.

Post a Comment

 
Top