MANCHESTER,
ENGLAND
HAMNA
namna. Hali si shwari kabisa Old Trafford na vigogo wakubwa hawajaridhika na
mwenendo wa Louis van Gaal ambaye ameendelea kujipa moyo kuwa ataendelea kuwa
kocha wa Manchester United msimu ujao.
Inadaiwa
kuwa hata Sir Alex Ferguson aliyekuwa anasuasua kukubali kocha wa zamani wa
Chelsea, Jose Mourinho kupewa timu sasa amebadili mawazo na ameruhusu kocha
huyo mreno awe mrithi wake wa tatu tangu kuondoka kwake.
Ferguson
Ferguson
ambaye ni mmoja kati ya Wakurugenzi wa Old Trafford kwa sasa inadaiwa kuwa
amebadili msimamo wake baada ya awali kuonekana kumsapoti Van Gaal aendelee
msimu ujao au Ryan Giggs apewe timu hiyo.
Achilia
mbali Ferguson, mkongwe wa Manchester United, Bobby Charlton ambaye ni mmoja
kati ya watu wanaoheshimika zaidi Old Trafford naye amebadili msimamo wake na
yupo tayari kuona Mourinho akipewa timu.
Na
sasa inadaiwa kuwa United itamfukuza Van Gaal hata kama timu hiyo itafanikiwa
kutwaa Kombe la FA ambapo sasa wapo katika hatua nzuri baada ya kutinga nusu
fainali kwa kuichapa West Ham mabao 2-1 Jumatano ugenini.
Van Gaal
Man
United wana wasiwasi kuwa huenda timu yao itakosa kushiriki michuano ya Ligi ya
Mabingwa wa Ulaya msimu ujao wakati huu ikishika nafasi ya tano kwa tofauti ya
pointi nne kutoka kwa Manchester City inayoshika nafasi ya nne huku wakiwa
wamebakiwa na mechi sita mkononi.
United
pia ina uhakika wa kumlipa pesa kiduchu za fidia Van Gaal ambaye mwishoni mwa
msimu huu atakuwa amebakiza mwaka mmoja kumaliza mkataba wake wa miaka mitatu
Old Trafford na mabosi wa Man United wanaamini ni wakati mwafaka kwao kufanya
mabadiliko.
Wasiwasi
umeongezeka baada ya timu pinzani kujiimarisha zaidi ambapo watani wao wa jiji
moja, Manchester City wamefanikiwa kuinasa saini ya kocha mahiri wa zama hizi,
Pep Guardiola huku Chelsea wakiwa wamefanikiwa kuinasa saini ya kocha wa zamani
wa Juventus, Antonio Conte ambaye ana rekodi nzuri za mataji.
Wanaamini
kuwa Mourinho ndiye kocha pekee aliye sokoni kwa sasa ambaye anaweza kuirudisha
timu hiyo katika ushindani licha ya kufukuzwa na Chelsea Desemba mwaka jana
kufuatia matokeo mabovu yaliyoiandama timu hiyo msimu huu.
Mourinho
Wasiwasi
umeongezeka miongoni mwa mabosi wa Old Trafford kuwa wakizubaa huenda Mourinho
akakubali ofa kutoka katika klabu za Real Madrid na PSG ambazo inasemekana
zimekuwa zikisaka saini yake.
Hali
si shwari sana PSG ambapo inasemekana mabosi wa timu hiyo hawajaridhishwa na
timu hiyo kutolewa katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Manchester City na
huenda hatima ya kocha Laurent Blanc ikaanza kuwa shakani.
Kwa
upande wa Madrid, bado kuna wasiwasi kama kocha wao wa sasa, Zinedine Zidane
aliyechukua nafasi ya Rafa Benitez ataweza kumudu mikiki ya kazi hiyo akipewa
nafasi ya kudumu kikosini hapo licha ya kufanya vema katika Ligi ya Mabingwa
mpaka sasa.
Post a Comment