0


Flamin
LONDON, ENGLAND
JAMANI imetosha. Mnaweza kwenda. 
Mastaa watano wa Arsenal wameambiwa maneno hayo na sasa wamefunguliwa mlango wa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu kwa sababu klabu hiyo haiwahitaji tena.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Emirates, Arsenal inatarajia kupangua kikosi chake kwa kiasi kikubwa msimu ujao kwa kufanya matanuzi ya nguvu sokoni na kuachana na wachezaji ambao hawaisaidii timu hiyo kwa sasa.

Gibbs
Viungo watatu, Mikel Arteta, Mathieu Flamini na Tomas Rosicky wataachwa rasmi baada ya mikataba yao kumalizika miezi miwili ijayo baada ya klabu kuamua kuwa haitaendelea nao tena na haitawapa mikataba mipya.
Arteta na Rosicky wamekosekana kwa vipindi virefu vya msimu kutokana na kuwa majeruhi huku Arteta ambaye ni nahodha akiwa amecheza mechi 13 tu msimu huu wakati huu akikabiliwa na matatizo ya kiazi cha mguu.
Rosicky, kiungo wa kimataifa wa Czech mwenye kipaji kikubwa amekuwa nje kwa muda mrefu na aliumia msuli, aliporudi tena tu katika mechi yake ya kwanza ya msimu huu baada ya kuumia goti kwa kipindi kirefu.

Rosicky  
Arteta ambaye keshokutwa anatimiza miaka 34 anapigiwa upatu ya kujiunga na benchi la ufundi la Arsenal linaloongozwa na Arsene Wenger kwa ajili ya kuwa kocha siku za usoni wakati huu akifanyia kazi mazoezi yake ya ukocha na amekuwa akifundisha timu ya watoto angali akiwa majeruhi.
Kwa upande wa Flamini ambaye alijiunga na Arsenal Julai 2004 akitokea Marseille ya Ufaransa kabla ya kuondoka mwaka 2008 kwenda AC Milan na kurudi tena mwaka 2013 anajiandaa kuondoka jumla na nafasi yake tayari imeshachukuliwa na kiungo wa kimataifa wa Misri, Mohamed Elneny aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 7 milioni kutoka Basel ya Uswisi Januari mwaka huu na tayari ameshaanza kushika kasi.

Chamberlain
Arsenal pia ipo tayari kusikiliza ofa kwa beki wake wa kulia, Mathieu Debuchy ambaye ilimnunua kutoka Newcastle Julai 2014 lakini akaathirika na majeraha ya muda mrefu huku nafasi yake ikichukuliwa na kinda mahiri wa Kihispaniola, Hector Bellerin ambaye amejimilikisha nafasi hiyo.
Kwa sasa Debuchy ambaye ni staa wa kimataifa wa Ufaransa yupo kwa mkopo katika klabu ya Bordeaux ya kwao Ufaransa tangu Januari mwaka huu na atauzwa jumla katika dirisha la majira ya joto.

Arteta
Wenger pia anataka kuondokana na beki wa kushoto wa Kiingereza, Kieran Gibbs ambaye msimu huu amepoteza jumla nafasi yake kwa beki wa kushoto wa Kihispaniola, Nacho Monreal huku ikidaiwa kuwa anamsaka beki wa kushoto wa klabu ya Lorient ya Ufaransa, Raphael Guerreiro kuchukua nafasi hiyo.
Arsenal imepanga kuwapa mikataba baadhi ya mastaa wake kama Santi Cazorla, Alexis Sanchez, Mesut Ozil, Jack Wilshere na Alex Oxlade-Chamberlain ambaye hata hivyo, kuna utata kuhusu hali yake ya baadaye klabuni hapo.

Wenger
Inadaiwa kuwa Wenger hajaridhishwa na kasi ya maendeleo ya staa huyo wa England aliyenunuliwa kutoka Southampton miaka mitano iliyopita na bado kuna wasiwasi kwamba huenda ikasikiliza ofa kutoka katika timu ambazo zitamtaka.
Ripoti zinadai kuwa, Mfaransa huyo amepewa maagizo ya kugombea wachezaji bora barani Ulaya kama anataka apewe mkataba mwingine wa kuifundisha timu hiyo ambapo mkataba wake wa sasa unatarajiwa umalizika mwishoni mwa msimu ujao.


Post a Comment

 
Top