CATALUNYA,HISPANIA
BADO una mawazo kwamba Mchezaji Bora
wa Dunia, Lionel Messi atacheza soka England?
Au unafikiria kuwa anaweza kwenda kucheza
katika Ligi One ya kule Ufaransa? Utakuwa unakosea.
Staa huyo wa dunia anayeitumikia Barcelona
amesema hana mpango wa kuitumikia klabu nyingine yoyote ya barani Ulaya zaidi
ya Barcelona.
Kama haitoshi Messi amedokeza kwamba
baadaye anaweza kurudi kucheza Argentina kabla ya kutundika daruga.
Messi, aliyechukua tuzo yake ya tano
ya Ballon d'Or mapema mwezi huu, amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia
katika Ligi Kuu ya England kwa kutua Manchester City na Ufaransa kwa vinara Paris Saint-Germain.
Lakini supastaa huyo amekataa
kuondoka katika Ligi ya La Liga na
kujiunga na klabu hizo na kusisitiza hawezi kucheza katika klabu nyingine yeyote
ya barani Ulaya zaidi ya Barcelona.
Messi mwenye umri wa miaka 28, alisema
uwezekano wa kurudi nyumbani Argentina kabla ya kustaafu ni mkubwa zaidi.
“Nimesema siku zote Barcelona ni
nyumbani , nataka kustaafu katika klabu hii, lakini nilikuwa nazungumzia kuhusu
kazi yangu Ulaya,” alisema.
“Kamwe sitacheza kwenye klabu
nyingine ya Ulaya zaidi ya Barcelona. Lakini nitapenda kucheza Argentina, kwa
sababu nimeondoka nikiwa bado mdogo. Nataka
kuonja ladha ya soka la Argentina.
“Lolote linaweza kutokea katika soka,
lakini sina shaka kwa kile ninachokitaka, na ninachokitaka ni kubaki hapa
Barcelona.”
Baada
ya kukosa baadhi ya michezo ya Ligi ya La Liga msimu huu kutokana na majeraha,
Messi amerudi katika kikosi cha kwanza kwa staili, kwa kufunga mabao manne
katika mechi mbili za mwisho.
Barcelona chini ya kocha, Luis
Enrique inajiandaa kwa mchezo wa robo fainali ya Copa del Rey dhidi ya Athletic
Bilbao Jumatano.
Lakini Messi na nyota mwenzake Luis Suarez ambaye
alifunga ‘hat trick’ dhidi ya wapinzani wao katika mchezo La Liga na kushinda mabao 6-0 hawatacheza.
Messi alitolewa wakati wa mapumziko
katika mchezo huo dhidi ya Basque Jumapili na katika mazoezi Jumatatu
alipumzisha kutokana na maumivu ya nyama za paja.
Suarez
alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Espanyol baada ya kufokeana na
mchezaji wa timu pinzani.
Post a Comment