0
Vaan Gaal
...akiwa safarini
.... je atarudi?

MANCHESTER, ENGLAND
TETEMEKO limeikumba Manchester United. Baada ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Southampton kwenye uwanja wao wa Old Trafford, hali ilikuwa tofauti juzi Jumapili kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo.
Man United iliamua kufuta mazoezi hao ya juzi Jumapili, huku kukiwa na hali ya hatari kuhusu kocha wa kikosi hicho, Louis van Gaal juu ya hatima yake katika timu hiyo.
Kulikuwa na ukimya mkubwa katika uwanja wa mazoezi wa timu hiyo huko Carrington, ambapo wachezaji wote na makocha waliambiwa wasije tofauti na ilivyokuwa kawaida yao ambapo walikuwa wakienda kufanya mazoezi baada ya kutoka kwenye shughuli za ibada.
Hii ni mara ya kwanza tangu timu hiyo iwe chini ya Van Gaal kushindwa kufanya mazoezi siku moja baada ya mechi, ambapo walikuwa na kawaida ya kukutana na kufanya mazoezi kwa dakika 45 hadi 90.

...baada ya kipigo
Van Gaal, ambaye amekuwa na misimamo amekuwa akiwataka wachezaji wake kuja mazoezini siku inayofuatia baada ya mechi hata kama watakuwa wamecheza mechi ya ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo tukio la juzi lilitia shaka na mshtuko mkubwa.
Kocha huyo ameripotiwa kurudi kwao Uholanzi kushiriki sherehe ya siku ya kuzaliwa na binti yake, huku kukiwa na mashaka makubwa juu ya hatima ya kibarua chake baada ya kichapo hicho kutoka kwa Southampton.
Kipigo hicho kimeifanya Man United kuwa nyuma ya Tottenham Hotspur kwa tofauti ya pointi tano katika mbio za kuwamo ndani ya nne bora ili kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Uhakika sasa umekuwa mdogo kama Van Gaal ataendelea kubaki hadi mwisho wa mkataba wake ambao umebakiza miezi 17 kufika tamati.
Man United ya sasa haiwezi hata kutengeneza nafasi za kufunga, huku shuti lao pekee lililolenga goli walilopiga kwenye mchezo dhidi Southampton ni lile alilopiga beki Daley Blind kutoka umbali wa mita 30.

Akiwa na benchi lake la ufundi
Kutokana na hali hiyo ya kocha Van Gaal kuifanya Man United kuwa timu ya kawaida sana, makocha wengi wamehusishwa na timu hiyo, akiwamo Jose Mourinho na Pep Guardiola.
Kuhusu hali ya kikosi, kocha Van Gaal huenda akachukua uamuzi wa kung’atuka baada ya kukiri kwamba amewaangusha sana mashabiki wa timu hiyo.
Kocha huyo Mdachi alikumbana na kelele za kuzomewa uwanjani Old Trafford baada ya kipigo. Van Gaal anataka kuachia ngazi mwenyewe kabla ya kusubiri kutimuliwa.
LVG alisema: “Nimehuzunika sana kwa sababu nimeshindwa kufikia matarajio ya mashabiki. Walikuwa na matarajio makubwa kutoka kwangu, lakini nimeshindwa kutatimiza. Nimehuzunika sana.”
Mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, David Gill amezidisha presha kwa kocha huyo baada ya kukosa kushindwa kwake kuleta mafanikio wakati alipewa pesa ya kutosha kufanya usajili.
Gill alisema: “Hakuna ubishi kwamba amefeli hasa baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye dirisha la usajili la mwaka jana.”
Van Gaal, 64, ametumia zaidi ya Pauni 250 milioni kwenye kufanya usajili tangu alipotua klabuni hapo miezi 18 iliyopita.

Post a Comment

 
Top