Ozil
LONDON, ENGLAND
IMEVUJA aisee. Kumbe Arsenal haikumsajili Mesut
Ozil kwa dau walilokuwa wakidai kwamba ni Pauni 42.5 milioni.
Mtandao mmoja wa Football Leaks ulioibuka
kufichua siri nyingi za uhamisho wa wachezaji, umeweka bayana ada na malipo
mengine ambayo Arsenal ililipa kumnasa kiungo huyo fundi
wa mpira kutoka Ujerumani.
Ozil alinaswa na Arsenal kutoka Real Madrid
mwaka 2013 na kila kitu kilichowekwa kwenye mkataba wake kimewekwa bayana na
mtandao huo.
Mtandao huo uliweka bayana pia dili za uhamisho
za wanasoka wengine kama Gareth Bale, Anthony Martial na wachezaji wengine,
ambao walisajiliwa kwa pesa nyingi miaka ya karibuni.
Arsenal imekuwa ikitamba kuweka rekodi ya
uhamisho kwenye timu yao kwamba Ozil ndiye mchezaji ghali zaidi baada ya
kumnasa kwa Pauni 42.5 milioni, lakini siri imefichuka kwamba Wenger hakulipa
kiasi hicho cha pesa.
Uhalisi Arsenal ililipa Euro 44 milioni (Pauni 36
milioni kwa wakati huo) kumnasa kiungo huyo Mjerumani, ada ambayo ni ndogo ukilinganisha
na Pauni 42.5 milioni zilizokuwa zimeelezwa na Arsenal kwamba imelipa kwa awamu
tatu katika kipindi cha miaka miwili.
Kwenye usajili wa mchezaji huyo, Arsenal
itatakiwa kulipa Euro 1 milioni kwa kila mwaka kwa kipindi cha miaka sita watakapofuzu
kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa muda ambao Ozil ataendelea kuwapo kwenye
kikosi hicho.
Kwa sasa, Arsenal imeshalipa Euro 2 milioni na
hadi kulipa pesa zote haziwezi kuzidi Euro 6 milioni.
Habari mbaya kwa Arsenal ni kwamba haiwezi
kumuuza Ozil katika klabu yoyote ya Hispania bila ya kuiambia Real Madrid
kwanza hata kama wamepokea ofa kubwa kiasi gani. Real Madrid imeweka kipengele
kwenye mkataba wa Ozil unaowapa wao nafasi ya kumnunua Ozil kabla ya klabu
nyingine yoyote kutoka Hispania.
Kwa mfano, kama Barcelona imekubali kulipa ada
yoyote watakayoambiwa na Arsenal kuhusu Ozil, basi Wenger atapaswa kuwaambia
Real Madrid kwanza kisha wao ndio wataamua ndani ya saa 48, kama ama auzwe au watoe
ofa kama iliyowekwa na Barca ili kumsajili Ozil wao. Arsenal haina nguvu ya
kuamua moja kwa moja suala la kumuuza Ozil kwenye timu yoyote ile ya Hispania.
Real Madrid wameweka kipengele hicho kwenye
mkataba wake kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa Ozil kurudi nchini Hispania na
kucheza kwenye timu ambayo ni wapinzani wao.
Kwenye mkataba huo wa Ozil, Real Madrid wamekuwa
wajanja sana baada ya kuweka kipengele kingine ambacho kinabainisha kwamba kama
Ozil atauzwa kwa ada inayozidi Euro 50 milioni kwa timu yoyote ya Hispania,
basi wao watachukua asilimia 33 ya faida iliyozidi kwa kulinganisha ada yake
waliyomuuza kwenda Arsenal.
Kwa vipengele vyote hivyo
ni wazi Real Madrid inafanya ujanja wa kumzuia Ozil asijiunge na timu nyingine
ya Hispania zaidi ya timu yao, huku takwimu zikifichua kwamba dau halisi ambalo
Arsenal ililipa kumsajili mchezaji huyo ni wazi sasa kwa mabao yote na pasi za
mabao alizopiga, Ozil ameigharimu timu hiyo Pauni 857,000 kwa kila bao au pasi
ya bao aliyopiga kwenye Ligi Kuu England hadi kufika sasa.
Post a Comment