0


LONDON, ENGLAND
 ARSENE Wenger amechokwa. 
Ndiyo hivyo baada ya kile walichosema mashabiki wa timu hiyo kwamba kocha huyo afungashe tu virago vyake na aende zake kama Arsenal itashindwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Katika utafiti uliofanywa na Mtandao wa Goal.com kupitia wasomaji wake, asilimia 66 wamesema kwamba kocha huyo hakuna haja ya kuendelea kubaki katika kikosi cha Arsenal kama timu hiyo haitabeba ubingwa wa ligi msimu huu.
Arsenal ipo nyuma ya vinara Leicester City kwa tofauti ya pointi tatu, lakini hilo limetokea baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Chelsea Jumapili iliyopita.
Kipigo hicho walichokumbana nacho kwenye uwanja wao wa Emirates kimeibua presha mpya kikosini hapo wakati msimu wa ligi ukieelekea ukingoni.
Mashabiki wa timu hiyo katika utafiti huo, walipiga kura za kumtaka Wenger aachie ngazi kama timu itashindwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England ambao imeshindwa kuubeba kwa miaka 12 sasa.
Jumamosi hii, Wenger ataiongoza timu yake kwenye mbio za kutetea ubingwa wao wa Kombe la FA wakati watakapomenyana na Burnley, kabla ya kurejea kwenye ligi kumenyana na Southampton, ambao kwenye mechi iliyopita walishinda 4-0 walipokumbana na wababe hao wa Emirates.
Mechi nyingine za Arsenal baada ya Southampton itakipiga na Bournemouth, Leicester, Manchester United, Tottenham na Manchester City.

Post a Comment

 
Top