DAR ES SALAAM, TANZANIA
WATU wamebaki wameshangaa, wengi hawaamini kama staa wa zamani
wa Manchester United, Wayne Rooney angekuwapo kwenye msafara wa Everton
Tanzania, hatimaye naye ametua.
Timu hiyo inayocheza Ligi Kuu England imewasili na iko tayari
kwa mchezo wa Alhamisi dhidi ya Gor Mahia utakaofanyika katika Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.
Ujio wa Everton ni wa kihistoria kwani tangu klabu hiyo
ianzishwe, hawajawahi kufika Tanzania na sehemu kubwa ya safari yake imechangiwa
na wadhamini wao, Kampuni ya SportPesa.
Everton iliwasili asubuhi ya Jumatano kwa ndege ya kukodi ya
Shirika la Ndege la Aeronexus, imefikia Hoteli ya Sea Cliff, Masaki, Dar es
Salaam.
Timu hiyo iliwasili saa 2:15 asubuhi ikiwa na msafara wa
wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na watu wengine wanaofikia 80.
Baada ya kuwasili wachezaji walilakiwa na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliyekuwa uwanjani hapo
mapema.
Hali ilivyokuwa Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaambiwa, mashabiki kadhaa
walifika mapema wakiwa na shauku ya kutaka kuwaona Everton na zaidi
wakimzungumzia Rooney.
Unajua Wahenga wana akili sana. Walisema hivi: Wewe ukisema
wanini, wenzako wanawaza watakipata lini. Ndivyo ilivyuokuwa kwa Rooney.
Ukianza na mashabiki, walikuwa wakiuliza kama naye yumo kwenye
msafara, na wengine wakiwaza kupiga naye picha ‘selfie’.
Hata hivyo haikuwa rahisi kwao. Rooney alikuja na alishangiliwa
sana mashabiki waliokuwa nje ya uzio na wengine wakimwita, Rooney…Rooney.
Rooney alitoka tofauti, wakati wenzake wakitoka ndani pekee yao
na mabegi, yeye alikuwa na watu watatu wakimsindikiza, ukweli alikuwa tofauti
na waliokuwa wanatoka VIP Lounge na kuingia kwenye basi lililokuwa limepaki
pembeni ya eneo hilo.
Mchezaji mwingine aliyekuwa kivutio, alikuwa Yannick Bolasie,
Mcongoman anayecheza nafasi ya winga katika timu hiyo.
Unajua ilikuwaje? Alipotoka VIP kelele za kumshangilia
zilisikika kutoka nje ya uzio wa VIP, kumbe walikuwa Wacongoman wanaoishi
Tanzania waliokuja kumshangilia ndugu yao.
Walikuwa kama 50 hivi, walitengeneza na fulana zilizokuwa na
picha ya Bolasie huku wakipiga ngoma.
Walikuja na magari aina ya Toyota-Coaster mawili yaliyokuwa
yamepaki pembeni na bendera kubwa ya Taifa la DR Congo na wengine wakiwa
wameshika bendera ndogo za DR Congo wakizionyesha juu kuashiria kumsifu
mchezaji huyo kwani walinyoosha juu huku wakiimba Bolasie…Bolasie.
Rooney akisalimiana na Waziri Mwakyembe.
Mmoja wa mashabiki hao, Belanga Muyani alisema: “Wameifanya hii
kuwa spesho kwa mchezaji wao. Bolasie ni mchezaji tunayempenda, anaiwakilisha
vizuri Congo sisi Wacongoman tunaipenda Premier League ya England na tunaipenda
Everton kwa iko na Mcongoman mwenzetu,” alisema.
Hata baada ya msafara kuondoka, Wacongoman hao walibaki uwanja
wa ndege na wakipiga ngoma na kuimba nyimbo mbalimbali za kumtukuza na kumsifu
Bolasie.
Baada ya kuwasili, Waziri Mwakyembe alizungumza na wanahabari na
kusema kuwa ujio wa wachezaji hao ni mafanikio ya Tanzania kwa kuwa Tanzania
itakuwa ikimulikwa na vyombo vya habari vya mataifa mbalimbali duniani.
“Kama mnavyojua, jamaa wamekuja na dunia nzima inaiangazia
Tanzania, itakuwa neema kwa Tanzania,” alisema Dk Mwakyembe.
Post a Comment