0
                    LONDON, ENGLAND
DIEGO COSTA ndio basi tena, hataitumikia tena Chelsea msimu ujao wa Ligi Kuu England baada ya bosi wake, Antonio Conte kumtumia ujumbe wa kumwambia hatakiwi klabuni hapo.
Costa ametanganza  mbele ya waandishi wa habari kuwa kwa sasa anajipanga kuondoka Chelsea katika msimu huu wa majira ya joto baada ya Conte kumwambia kuwa hatamuhitaji tena klabuni hapo baada ya kumtumia ujumbe huo.
Awali straika huyo wa kimataifa wa Hispania mwenye asili ya Brazil , 28, alitaka kuondoka Stamford Bridge na kurudi Atletico Madrid, lakini mpango huo umekwama baada ya miamba hiyo ya La Liga kufungiwa kufanya usajili.
Kocha Conte anamtaka straika wa Everton, Romelu Lukaku ambaye ameonyesha nia ya kutaka kurudi katika klabu yake hiyo ya zamani, na amekuwa tayari kumuuza Costa na kufidia dau la Pauni 100 millioni la staa huyo wa zamani.
Costa ambaye ameongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho cha  mabingwa wa Ligi Kuu England anashawishika kuondoka katika majira haya ya joto baada ya kuambiwa na Conte kuwa hatakuwa tegemeo lake katika msimu ujao .
"Conte alinitumia ujumbe akiniambia kuwa sipo kwenye mipango yake," Costa alisema baada ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Hispania na Colombia ulioisha kwa sare ya mabao 2-2 Jumatano usiku.

                                                               Costa
Akionekana kuchanganyikiwa na ujumbe huo, Costa aliongeza: "Inaonekana kama sikuwa na msimu mzuri. Ulikuwa ujumbe mwepesi baada ya mazuri yote niliyoyafanya kwa klabu, kama sitakiwi itanibidi kutafuta klabu nyingine."
Alipoulizwa kama kuna mtu yeyote mwingine ndani ya Chelsea aliyewasiliana naye baada ya ujumbe huo, Costa alisema: " Hapana, lakini kama kocha amefanya mawasiliano na wewe na kukuambia kuwa huhitajiki unapaswa kuondoka tu." 
Atletico Madrid ilikuwa tayari kumchukua straika huyo wa Hispania na kumrudisha nyumbani lakini imefungiwa kufanya usajili hadi Januari 2018.
Costa na Conte walitofautiana Januari mwaka huu kutokana na kiwango cha straika huyo.
Hata hivyo matatizo zaidi ya Costa na Conte yalianzia mwezi huo, wakati Muitaliano huyo alipomuacha London katika kikosi cha Chelsea ambacho kilisafiri kwenda ugenini kukipiga na Leicester City baada ya straika huyo kukorofishana na kocha wa viungo wa Chelsea.
Baadaye zikaja taarifa kuwa Costa alikuwa akitakiwa kutua katika klabu ya Ligi Kuu ya China, Tianjin Quanjian kwa  ofa nono ambayo ilikuwa na thamani ya Pauni 30 milioni kwa mwaka kama mshahara. Wakati ule Chelsea ilidai kwamba, ilikuwa haina mpango wa kumuuza Costa.

                                                 Antonio Conte na Diego Costa
Baadaye mwezi huohuo, mmiliki wa Klabu ya Tianjin Quanjian ambayo ndio mara nyingi imetajwa kumwania Costa alidai mipango ya kumchukua staa huyo ilikuwa imekwama kutokana na kanuni mpya za wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ya China.
Kwa mujibu wa kanuni mpya za Ligi Kuu ya China, kuanzia msimu ujao klabu zitaruhusiwa kupanga wachezaji watatu tu wa kigeni ndani ya uwanja badala ya wanne kama ilivyokuwa katika kanuni za zamani.

                                                                      Costa
 Hata hivyo, Costa mwenyewe alidai angependelea kurudi Atletico Madrid. Na Kama atabaki na msimamo wake huo itambidi kusubiri hadi Januari.
" Kurudi Atletico lingekuwa jambo zuri lakini natakiwa nitafakari kuhusu hilo," Costa aliongeza : "Huu ni mwaka wa mwisho kuelekea kwenye Kombe la Dunia na siwezi kukaa bila ya kucheza kwa miezi mitatu hadi minne."
           

Post a Comment

 
Top