Na Priva ABIUD
NI miaka sita imepita
tangu mkurugenzi wa zaman wa AC Milan, Adriano Galliani afanye kosa aliloliita
la maisha.
Kosa hilo ni lile la kumruhusu
kiungo bora kabisa, Andrea Pirlo kujiunga na mahasimu wao wakubwa
Juventus.
Kosa alilolifanya Gallian
kwa sasa linamtesa mkurugenzi mkuu wa Milan, Marco Fassone ambaye ameingia
mgogoro mkubwa na wakala wa kipa wa klabu hiyo Gianluigi Donnarumma kwa kila
kinachoitwa vita ya pesa.
Donnaruma anashindwa
kuongeza mkataba kwa sababu ametishiwa sana maisha na mashabiki wa klabu hiyo
na hata taifa kwa jumla.
Donnarumma mlinda mlango
kwa AC Milan anaishi kama mkimbizi ndani ya taifa lake. Hivi majuzi tu
katika mchezo wa Timu ya Taifa ya Vijana ya Italia Donnarumma
alitupiwa hela feki na mashabiki kwa kile walichodai kuwa bwana mdogo amegomea
mshahara wa Euro 80,000 kwa wiki akiwa na miaka 18 tu.
Mino Raiola aliyekuwa
dalali wa dili la Paul Pogba, ndiye wakala wa Donnarumma, amekanusha kuwa mteja
wake hajasaini kwa sababu za kifedha ila anahofia usalama wake klabuni hapo.
Donnaruma alijiunga AC
Milan akiwa na miaka 16 na kulipwa mshahara wa Euro 100,000 kwa mwaka.
Pirlo
Amejipatia umaarufu mkubwa
kwa uwezo wake akiwa langoni. Mlinda mlango huyu mpaka sasa amecheza michezo 70
tu, lakini tayari vurugu la mkataba limekwisha anza.
Kuna baadhi ya
mambo ya kuweka sawa, sio kweli kama Donna anataka kuondoka kisa ametishiwa,
nani anamtishia? Tangu lini unamtishia mchezaji wako bora kabisa? Raiola kwa sasa ni dalali wa kuopogwa kabisa.
Walio wengi wanamtukana
Donna wanasema kuwa anapenda hela kuliko AC Milan. Kwa akili ya kawaida ni nani
hapendi pesa?
Yuda Iskarioti alimuuza
Yesu kisa pesa. Makanisa mengi duniani yanahimiza matoleo ya sadaka, wewe ni
nani asiyependa pesa kama viongozi wa dini wanatuhubiria kuhusu sadaka? Hivi
unajua kazi anayoifanya Donnapale golini?
Yaani mtu anajitupa kufuata mashuti ya watu
mnasema anapenda hela? Mlitaka apende nini?
Cha muhimu katika maisha
ya mchezaji kwanza ni maslahi yake. Huwezi kutegemea kazi ya mchezaji bila
kutimiza maslahi yake.
Donna
Wapo watu wanaodai kuwa
wachezaji wa siku hizi wanataka fedha nyingi ukilinganisha na wa zamani.
Naamini watu watakuja na mfano wa Lionel Messi kugowamea Waraabu wa Manchester
City na PSG kuwa hapendi hela.
Kuna tofauti kubwa hapa,
fahamu kuwa kuna tofauti ya mchezaji aliyeridhika na pesa anazopata na yule
ambaye anaona alizonazo bado ni kidogo.
Mshahara wa Messi pamoja
na mafanikio yake yanamtosha kabisa kususia fedha za klabu ambazo haziwezi
kumpa mafanikio hayo.
Donna yupo kwenye timu ambayo haina mbele wala
nyuma kwa sasa na bado mshahara ni mdogo je, aendelee kubaki kisa anaogopa
ataambiwa anapenda fedha nyingi?
Hivi fedha nyingi ndio nini? Kipi ni kipimo
cha fedha nyingi? Dunia imebadilika sana. Ulitegemea mchezaji ambaye ana kipaji
kizuri apatikane kwa ada ya 20 milioni?
Kwani tupo mwaka 2000?
Hivi hao wazungu wanaotoa
hizo fedha kwan wao hawaoni kama ni nyingi?
Ni kweli kiasi ambacho
Alvaro Morata anahitajika nacho Manchester United ni nyingi? Sawa, ila ni
nyingi kwa wakati gani?
Morata
Ngoja leo niongee
kiuchumi kidogo ili nieleweke, kwanza nataka nikwambie kila baada ya miaka saba
mpaka 10 kuna uwezekano mkubwa thamani ya kitu ikawa mara mbili
zaidi ya kilivyo kuwa kiuchumi. Usiniulize
ni nani kasema, nimesema mimi. Nikukumbushe tu, mwaka 2000 Dola moja ya
Kimarekani ilikuwa sawa na Shilingi 800 ya Tanzania, leo hii Dola moja ni sawa
na 2,300, hii inaashiria nini?
Uchumi umebadilika sana. Nikurudishe mbali
sana, mchezaji wa kwanza kabisa duniani kuuzwa alikuwa Willie Grove
aliuzwa kwa Euro100 akitokea West Bromwich Albion kwenda Aston Villa mwaka
1893. Ilipita takribani miaka 12 rekodi
yake kuvunjwa na mchezaji aliyefuata aliuzwa takribani Euro 1,000 mshambuliaji
hatari wa Sunderland kwa wakati ule Alf Common alipouzwa kwa Middlesbrough. Ukiangalia hiyo bei ni sawa na takribani mara
10 ya bei ya hapo awali.
Wenger
Hivi hata nyie mashabiki
wa Arsenal mnaosema Kocha Arsene Wenger ni bahiri, hamjui kuwa kocha wenu wa
zamani, Herbert Chapman aliweka rekodi ya kumnunua mchezaji wa gharama kubwa
mwaka 1928, akitoa kitita cha Euro10,000 ili kumpata David Jack kutoka Bolton
Wanderers?
Hapo ilikuwa takriban
miaka 10 baadaye.
Nadhani mpaka hapo
unaelewa nini nachomaanisha. Bei za wachezaji zinapanda kutokana na hali halisi
ya uchumi kwa wakati huo. Au nikupe mfano rahisi tu, mwaka 2008 gari la
kifahari aina ya Buggati Veyron 16.4 liliuzwa kwa Dola 1 milioni na ushee, lakini gari lilelile kwa
mwaka 2015 linauzwa takribani Dola 2.5 milioni, hii ni mara mbili ya bei ya
hapo awali.
Maisha yanabadilika,
uchumi unapanda, bei ya maisha inaongezeka kwa kiasi kikubwa. Bei ya Pirlo
akiwa na miaka 22 ilikuwa Euro 18 mwaka 2001, lakini huwezi kumpata kiungo
mkabaji mzuri kama Pirlo kwa wakati huu kwa bei hiyo hata kidogo. N’golo Kante
tu ameigharimu bei kubwa sana Chelsea ukilinganisha na bei ya Pirlo ambayo ni
mara mbili.
Nawashangaa sana
mashabiki wa AC Milan ambao wamepoteza muda wao wakizunguka mitaa ya
Santa Maria Dele Gracie kwenye steshenari za Fabriano Boutique, Pettinaroli na
wengine wakijazana maduka ya San Maurilio na Pasini Milano kuprint hela bandia
ili wakamtupie Donna kwa kile wanachodai anataka pesa nyingi. Nimesema hapo awali
kuwa bei ya maisha inabadilika mara mbili zaidi ya hapo awali kwa takribani miaka
mitano na kuendelea. Niwarudishe nyuma kidogo wala sio mbali sana, najua
unamfahamu Zinedine Zidane? Mwaka 2001 si unafahamu alikuwa Juventus?
Zidane
Bila shaka ndio. Unafahamu
kuwa mwaka uleule alihamia Real Madrid? Je, unafahamu alisafirishwa kwa kitita
cha Euro 46?
Jibu ni ndio namba hazidanganyi. Je, unafahamu
ilichukua miaka mingapi kwa bei ile kuzidishwa mara mbili kwenye usajili
mwingine?
Kwa taarifa yako ilichukua
miaka saba tu, ambapo Cristiano Ronaldo alipatikana kwa ada ya Euro 80. Je,
ulitaka Ronaldo naye auzwe sawa na bei ya Zidane aliyeuzwa miaka ya 2001 kisa
tu pesa hiyo ndo sahihi na sio nyingi?
Nimeuliza tangu awali
pesa nyingi ndio nini? Kipi ndio kiwango cha pesa nyingi? Je, tutumie kigezo
gani kusema pesa ni nyingi? Twende taratibu tu utanielewa. Najua unamfahamu
Juan Sebastian Veron?
Bila shaka unamfahamu. Huyu aliweka rekodi ya
kununuliwa kiasi ghali zaidi mwaka 2000, kilikuwa Euro 28, katika Ligi Kuu ya
England alipojiunga na Manchester United. Je, unafahamu ilichukua muda gani ili
mchezaji apatikane kwa mara mbili zaid ya bei ile?
Naam mwaka 2014 Angel Di
maria aliweka rekodi hiyo kwa kitita cha Euro 58 akijiunga Man United ileile
iliyoweka rekodi ya awali.
Di Maria
Nataka niwaambie kitu,
nadhani ni vizuri bei zikalinganishwa kwa miaka ili kupata uwiano mzuri na sio
tu kisa namba zikionekana nyingi, basi hiyo pesa n nyingi sana.
Mfano mwingine rahisi,
tujikumbushe miaka ya 2000 soda tulinunua Sh 200. Je, leo hii 200 unapata nini?
Je, miaka ya nyuma unakumbuka thamani ya senti tano? Je, bei ya soda kwa sasa
na kwa wakati ule sio mara mbili?
Kwa nini tunawalaumu kina
Klyian Mbappe wakitakwa kwa Euro 130? Unadhani wazungu wamewehuka? Maisha
yamebadilika mno.
Thamani ya pesa inapanda
sana. Unategemea Donna hapendi maisha mazuri? Hivi ni kweli hapendi kutembelea gari
la kifahari kama Buggati Veryon? Unadhani hapendi kupumzika hoteli za kifahari
kama Pallazo Parigi kule Milano? Tena kwenye vyumba vya gharama
kabisa? Unafikiri hapendi kwenda fukwe za Puglia na San Vitolo Capo kule sicily
kula bata wakati wa mapumziko na familia yake?
Yaani kwa akili yao unafikiri
Donna anapopigiwa mashuti golini na kudaka kama mtu asiye na akili hawazi kuwa
na maisha mazuri?
Twendeni mbele turudi
nyuma, ukisikia Euro 100 usidhani kwa wenzetu ni nyingi sana kama tunavyowaza
hapa kwetu Bongo. Ukweli klabu Man United na Real Madrid zina takribani utajiri
wa Dola 3 bilioni na ushee kila moja. Sasa kama timu ina utajiri huo kumnunua
mchezaji ghali siye kinatuuma nini?
Yaani leo hii Said Salim Bakhresa amenunua
andazi la Sh 100 kwa Sh1000 unalalamika?
Sioni kama ni matumizi
mabaya ya fedha nachokiona ni mabadiliko yametokea kwenye uchumi wa dunia.
Siku hizi wametokea
mawakala virambasi sana, na wenyewe wanataka cha juu kwenye kila dili wanalo
piga, je, unategemea utampata mchezaji kwa bei za mbuzi?
Huna pesa kaa kimya.
Usiseme kama Man United inaharibu soka kwa kununua wachezaji ghali kwamba timu
ndogo zitashindwa kufanya usajili, kwani timu gani ndogo imenunua mchezaji
ghali? Kama hazijawahi shida iko wapi Man United na Liverpool zikimwaga hela?
Msinielewe vibaya, hapa sizungumzii soka la
biashara la Wachina. Wale wanajielewa wao wenyewe, nao wana mipango yao. Hao si wazungumzii kabisa.
Kwa uhalisia 100 milioni
kwa sasa ni sawa na 40 milioni ya miaka 10 iliyopita wala hilo halipingiki
kabisa.
Labda tu nikukumbushe
rekodi zilitolewa na Delloite kuhusu mapato ya Real Madrid na Man United kwa
kipindi cha kuanzia mwaka 2001 hadi 2011, mwaka 2001 zote kwa pamoja
ziliikusanyia zaidi ya 350 milioni, lakini kufikia mwaka 2011 zote
zilijikusanyia mapato ya takribani 800 milioni, sasa unategema nini?
Kama timu inapata
mafanikio makubwa kiasi hiki kama tunavyoona kwa nini wachezaji nao bei zao
zisipande?
Sasa kama AC Millan
imenunuliwa kwa mkataba wa zaid ya 1 bilioni, lakini bado Donna analipwa Euro100,
000 kwa mwaka unategemea nini?
Ozil
Kwanza Donna anataka zaidi ya Euro 10 milioni
kwa mwaka. Ameshafahamu kuwa ana kipaji ambacho kinauzika kwa gharama yoyote
kwa sasa duniani. Sasa ya nini masikini kumpangia tajiri namna ya kutumia hela?
Umri wa mchezaji sio
tatizo kabisa, kwani Thierry Henry alinunuliwa bei gani na alikuwa na umri
gani?
Je, kuna mtu alitegemea balaa la Henry baadaye?
Maana Henry alinunuliwa Euro 16 akitokea Juve akiwa na miaka 20 tu,
lakini kila mtu alimnyooshea kidole Kocha Wenger.
Lakini Rekodi ya Henry inakuja kuvunjwa baada
ya miaka 13 na Mesut Ozil aliponunuliwa kwa ada ya Euro 47 akiwa na miaka 24.
Je, ulitegemea kumpata Ozil
kwa bei ya Henry ya mwaka 2000 kweli?
Labda nikuulize swali la
kizushi tu, si unafahama Phillippe Coutinho wa Liverpool? Alinunuliwa kwa 7
milioni akitoke Inter Milan mwaka 2013? Je, ingekuwa ndio sasa hivi yupo Inter
angeuzwa bei hiyohiyo kweli? Narudia tena heshima zipo jeshini kwenye soka cha
kwanza maslahi. Siku njema.
Post a Comment