0


PARIS, UFARANSA
ZLATAN IBRAHIMOVIC anataka sana kwenda kumalizia soka lake England lakini unajua anataka kiasi gani?
Habari za kushtua ni kwamba straika huyo wa PSG ya Ufaransa anataka  Pauni 600,000 kwa wiki kitu ambacho kimezishtua klabu zinazomfukuzia.
Zlatan ana umri wa miaka 34 kwa sasa na mkataba wake na PSG unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huku siku zake za kucheza soka katika kiwango cha juu zikikaribia kufika tamati, lakini mwenyewe anaamini ana thamani kubwa zaidi hasa atakapokuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu.

...Zlatan
Mmoja kati ya watu wa ndani katika klabu moja ya England inayotaka kumnunua Zlatan ilidai kwamba ni kweli mshambuliaji huyo anataka mshahara huo unaouweza kuwa mara mbili zaidi ya mchezaji anayelipwa zaidi England.
“Tungependa kumchukua lakini hizo pesa alizotaja ni kama kichaa. Tukimpata atakuwa na faida kubwa sana kwetu, lakini ni kweli ana thamani ya hizo pesa?” Alihoji mtu mmoja wa ndani kutoka katika klabu ambazo zinamwania Zlatan.
 Inadaiwa kuwa staa huyo wa zamani wa Ajax, Inter Milan, Juventus, AC Milan, Barcelona ana ofa ya kusaini mkataba na timu za China ambapo moja imefika mpaka dau la Pauni 1 milioni kwa wiki kwa ajili ya kujitangaza zaidi.
Hata hivyo, Zlatan amegomea dili la kwenda China na badala yake ameelekeza macho yake kucheza katika Ligi Kuu England huku akiwaambia wawakilishi wake kwamba pamoja na kucheza England lakini timu yoyote ambayo inamtaka italazimika kumlipa mshahara mara mbili ya ule anaoulipwa Ufaransa.

Zlatan
Inasemekana kuwa Zlatan anakerwa na makato makubwa ya kodi ya Uingereza na kama kuna timu itajitoa mhanga kumlipa mshahara anaoutaka huo utakuwa mshahara mkubwa zaidi kuwahi kulipwa kwa nyota yeyote ndani ya ardhi ya Uingereza.
Mpaka sasa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika Ligi Kuu England ni nahodha wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Wayne Rooney, ambaye anachukua Pauni 260,000 kwa wiki moja.
Wakala wa mchezaji huyo, Mano Raiola alikiri kwamba timu zote kubwa England isipokuwa Manchester City zinamtaka staa huyo na zimekuwa zikiulizia uwezekano wa kumtwaa mwishoni mwa msimu huu akimaliza mkataba wake PSG.
“Ukiiondoa Manchester City, ambapo kuna Pep Guardiola, klabu nyingine zote kubwa zimegonga hodi kuitaka saini yake,” alisema Raiola ambaye pia anawasimamia mastaa wengine wakubwa kama Paul Pogba wa Juventus na Mario Balotelli wa Liverpool.

                                                  ...akiwa mazoezini.
Zlatan ametwaa ubingwa wa ligi na klabu zote alizochezea barani Ulaya, Ajax, Barcelona, Inter Milan, AC Milan na hivi karibuni ametwaa ubingwa na PSG ya Ufaransa. Zlatan pia ndiye mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha timu ya taifa ya Sweden akiwa na mabao 62.
Kama vile haitoshi, Zlatan amewahi kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Sweden mara 10 huku mara tisa kati ya hizo akitwaa mfululizo kuanzia mwaka 2007 hadi 2015.

Post a Comment

 
Top