0


NA PRIVA ABIUD
HIVI majuzi kuna msanii mkubwa kutoka Ghana anaitwa Sarkodie, alitoa albamu yake mpya kwa jina la Marry. Aliviita vituo mbalimbali vya redio ili vimsaidie kuitangaza albamu hiyo.
Kituo kimoja cha redio kiligoma. Unajua kwa nini? Mmiliki wa hiyo redio alisema: "Muda mwingi tulimwita Sarkodie kwenye mahojiano lakini alikuwa haji, na tukifanya mahojiano na wasanii wakubwa huwa tunapata faida kubwa sana, lakini huyu jamaa alionesha dharau na sisi hatuwezi kutangaza albamu yake."
Kumbe dharau zilimponza sana huyu jamaa, huwa najiuliza je, ingekuwa Bongo halafu Clouds wagome kutangaza nyimbo zake, ingekuwaje?
Tuachane na hayo....

Ronaldinho
Kuna dalili ambazo kisoka ukiziona basi ujue ni zamu ya mbwa kula migomba! Mambo mengi yanatokea kwenye soka la England! Magazeti yamejitahidi sana kurudisha hadhi ya soka hilo. Ndio yamefanikiwa. Yamemleta Pep Gurdiola. Yamemleta Antonio Conte.
Na bado yanadanganya kuwa Jose Mourinho ameshamwaga wino Manchester United. Huenda sio kweli lakini unadhani magazeti yanakurupukia? La hasha! Kama huamini basi, tusubiri tuone.
Miaka kadhaa iliyopita Guardiola alitua Barcelona. Aliikuta Barca ikiwa na  wazee kama kina Thiery Henry (30),  Gianluca Zambrotta (31), Carles Puyol (30), Rafael Márquez (30), Lilian Thuram (36), Sylvinho (31), Edmílson (31), Deco (30), Ronaldinho (29), na Pinto (30).

Guardiola
Hao wote walikuwa chini ya Kocha Frank Rijkaard ambaye kwenye La Liga alimaliza katika nafasi ya tatu, Uefa alifika nusu fainali lakini hakuchukua hata Copa De la Rey.
Kule Italia pia, msimu wa 2010 Mourinho aliikimbia Inter ambayo alibeba nayo ubingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wengi walisema kuwa Mourinho ndio kawaida yake, lakini sikubaliani na hilo.
Kocha huwa anaangalia vitu vingi kabla hajongeza mkataba. Kwa mfano hebu angalia: Julio Cesar umri ni miaka 32, Luca (36), Paolo (39), Ivan Cordoba (35),  Lucio (33), Maicon ndiye aliyekuwa chalii (mdogo) kwa kuwa na umri wa miaka 30, Walter Samwel (33), Chivu (31), Zanetti (38), Dejan (33), Esteban Cambiasso 31, Forlan usajili mpya 30, Milito 32. Kwa msimu ule usajili Euro million 35. Hivi hata kama ni wewe kocha ungeendelea kubaki na timu ya namna hiyo?
Maana hii timu ilimaliza msimu wa sita kwenye ligi. Timu yenyewe usajili wa jumla ni Euro 35 milioni pesa ambayo hata Reheem Sterling isingeweza kumnunua.

Cambiasso
Labda ingejitahid kidogo ingempata Danny Welbeck tofauti na hapo basi ingesubiri kina Ashley Cole, Patrice Evra,  Nemanja Vidić, Rio Ferdinand watupwe kwenye timu zao ndio iwasajili.
Labda msomaji mpaka sasa hujanielewa. Umri wa wachezaji huwa unaonesha mwelekeo wa timu.
Man United inaweza ikaanza kukenua ikidhani kuwa ina kikosi bora. Ni kweli. Ukijumlisha umri wa wachezaji wote wa Man United halafu ukagawanya kwa idadi yao ili kupata wastani, basi utagundua ina wachezaji wa miaka 25 wote, lakini nikiiangalia Leicester City utagundua ina miaka 28!
Hapo utaniuliza bro? Mbona umesema umri unachangia mbona United ndio mbovu kuliko Leicester City?
Wakati Ronaldihno anaondoka Barcelona, Rais wa Barcelona, Johan Laporta alisema mengi sana. Inaonekana ugomvi ulikuwa mkubwa kati ya Dinho na Samuel Eto'o.
Laporta alisema kwa mwaka 2007, kwenye vipindi vya mazoezi 50, Dinho alihudhuria mara nane tu. Ilifika kipindi hata Johan Cruyff akawa anamtukana sana Ronaldinho kwenye magazeti. Hata klabu nayo ililalamika kuwa hauzi tena jezi kama zamani. Kuna kipindi mchezaji huwa anazungumza na umri wake, anajadiliana nao kwa kina kisha akimaliza anapiga stori na kiwango chake, akigundua mazungumzo ya yeye na umri wake na ya yeye na kiwango chake hazieleweki na hazimuingii akilini, basi hapo ndo utaanza kusikia kawa mlevi  kama Steven Gerrard, mara kapigana baa  kama Wayne Rooney, mara kakutwa na malaya kama John Terry hiki ndicho kipindi alichopita Ronaldinho.
Wakati Ronaldinho anaambiwa nenda AC Milan kwa Euro 26 milioni wala hakujali kama AC Milan haijafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alichowaza ni umri wake na mwili wake. Alijua tayari ana mafanikio. Na alipofahamu fika kuwa mazungumzo ya awali ya yeye, umri na uwezo wake yanapishana alichofanya ni kukubali.
Alifika Uwanja wa Ndege wa Italy akiwa anacheka tu kama kawaida yake. Mashabiki wa AC Milan walijawa na furaha wakidhani mkombozi wao amefika.
Hapo juu nimezungumzia kuhusu umri wa wachezaji wa United. Timu inapokuwa na wachezaji wenye umri mdogo wala sio kigezo tu cha mafanikio na kuwa na wazee wala sio kuboronga. Kikubwa ni uhusiano wa umri na uwezo wake. Tatizo je, huyo mwenye umri mdogo ana uwezo gani? Na je huyu mzee ana uwezo gani? Muangalie Pirlo? Mfananishe na Welbeck? Unapozungumzia umri mdogo wa Man United utawataja kina Joe Riley, Donald Love, Cameron Jake Borthwick-Jackson, Memphis Depay, Matteo Darmian, Jesse Lingaard na Adnan Januzaj!

Lingaard
Je, hawa ni ‘World class players’? Je, wamepata namba kwa sababu wana uwezo au kwa sababu wanaozimiliki namba hizo ni majeruhi?
Unapotaja mchezaji mwenye umri mdogo, basi ili tumweke kwenye kundi hili la wabeba timu, hakikisha amepata namba kwa sababu ya uwezo wake!
Sio tu amecheza kwa sababu fulani kaumia. Angalia kina Riyad Mahrez, Mario Götze, Neymar, Isco, James Rodríguez n.k...
Lakin ni kweli Lingaard amepata namba kwa uwezo wake au kwa sababu mhusika hayupo?  Ukimzungumzia Antony Martial hapo nitakubali.
Amekuja Bastian Schweinsteiger! Pale Carrington amepokelewa kama alivyopokelewa Ronaldinho kule San Siro.
Tuliamini ni mtetezi! Lakini Paul Scholes anatuambia Bastian wa Bayern sio huyu. Guardiola alipogundua umri wa Bastian ni wa pensheni aliamua kurudia kilekile alichokifanya kwa Ronaldinho.

Bastian
Aliangalia uwezo wa Bastian, akafananisha na kazi yake? Kisha akamgeukia Javi Martínez, akaangalia faili lake la mkataba akachunguza umri na uwezo wake akaona utofauti?
Nahisi alijiona kama anakosea kumruhusu Bastian lakini alipokuja kugundua bado ana Thiago Alcântara na Gotze na wote ni wadogo na wana uwezo, basi hakuona tabu kumwelekeza Bastian, NSSF wakasalimiane na mzee mwenzake (Carrick).
Labda huenda Bastian hajachoka, au niseme tatizo ni watu anaocheza nao! Leo yupo kati na ‘ball dancer’ the ‘Big Fella’ kiungo fundi muongo muongo anaejifanya anataka kutoa pasi kulia huku akiangalia kushoto lakini anatoa pasi kwa adui Marouane Fellaini. Timu ina wachezaji wazee kwa uwezo lakini wadogo kiumri.
Umri na kicheko cha Ronaldinho kilionesha bado ni mdogo lakini uwezo ulishapungua zamani. Umri wa Bastian ni mkubwa lakini sura yake bado sielewielewi…. Sijajua bado ndio yule wa Bayern au Scholes anamsingizia.
Nina wasiwasi mkubwa na uwezo wake kwa sasa! Sijui uamuzi wa Guardiola kumtema ni kwa sababu alizeeka umri au uwezo! Sura yake inaonesha ana hasira na uchungu mkubwa na Man United, lakin je, ndicho anachomaanisha au ni zile sura za Kijeruman tu?
Maana huenda tukamwona mwenzetu ana uchungu kumbe ndio sura yake! Hupaswi kusajili tu eti kisa ni mdogo.. Hapana.. Lazima awe na uwezo.. Na hupaswi kumdharau mtu kisa umri ni mkubwa..

Post a Comment

 
Top