0


                  PORT OF SPAIN, TRINIDAD& TOBAGO
KWA mara ya kwanza Marekani imeshindwa kufuzu katika fainali za Kombe la Dunia tangu mwaka 1986 baada bao la ‘shetani’ kuipa ushindi Panama dhidi ya Costa Rica.
Marekani chini ya kocha wake Bruce Arena ilifungwa mabao 2-1 dhidi Trinidad &Tobago, wakati Panama ilifunga bao la shetani katika dakika ya 87 na kuifunga Costa Rica kwa matokeo kama hayo.
Lakini kumekuwa na malalamiko kuwa bao la kwanza la Panama halikuvuka mstari – ikimaanisha Marekani inaweza kukata rufaa  dhidi ya uamuzi huo.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Marekani ya Kaskazini na Kati (CONCACAF), malalamiko yanaweza kuwasilishwa na chama cha soka kilichoumizwa na matokeo ndani ya wiki tatu.
Lakini alipohojiwa baada ya mchezo huo, Msemaji wa Timu ya Taifa ya Marekani, Michael Kammarman alisema: "Kwa jinsi ninavyojua hakuna cha kufanya. Uamuzi wa mwamuzi ni wa mwisho."
Panama ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 hadi mapumziko na ilitakiwa kushinda dhidi ya wapinzani wake na kufufua matumaini ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia.

Lakini bao lake la kusawazisha lilikuwa la utata wakati mpira ulipokwama kuvuka mstari wa goli baada ya Gabriel Torres kupiga kichwa na kugonga mwamba.

Straika Blas Perez alianguka chini wakati akijaribu kuupiga mpira ili uvuke mstari kwa kutumia bega lake lakini mpira huo ulizuiwa na beki na kutoka nje, hata hivyo mwamuzi aliizawadia Panama bao.

Hakuna sheria ya ‘goal-line technology’ katika mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia kwa sheria za CONCACAF ikimaanisha uamuzi hufanywa kwa kutumia macho na huenda yakawa sio ya uhakika.

Panama bado ilihitaji bao moja ili kufuzu na Torres alikuwa shujaa baada ya kufunga kwa mpira wa adhabu katika dakika 87 na kuibua shangwe uwanjani.
Baada ya kutolewa, Kocha wa Marekani, Bruce Arena alisema: "Kila kitu kilikuwa kwa ajili yetu.

"Tumefeli siku moja. Hakuna msamaha. Leo tumefeli. Tulipaswa kutoka uwanjani hata na pointi moja.Tusingebaki nyumbani katika Kombe la Dunia na nitafanya maamuzi."

Post a Comment

 
Top