0


                                 AMSTERDAM, UHOLANZI
SERGIO KUN AGUERO amepata ajali mbaya ya gari akiwa Uholanzi na atalikosa pambano la Jumamosi  huku akitarajiwa kukosa mechi nyingine kadhaa.
Aguero alikuwa abiria katika teksi iliyopata ajali wakati akitoka katika tamasha kubwa la mwanamuziki maarufu wa Colombia, Maluma Alhamisi usiku huku akielekea uwanja wa ndege kwa ajili ya kurudi England kujiandaa na pambano dhidi ya Chelsea.
Hata hivyo, dereva wa teksi hiyo alipoteza mwelekeo na gari hilo likagonga nguzo za kando ya barabara na ingawa staa huyo wa kimataifa wa Argentina alikuwa amefunga mkanda lakini bado alivunjika baadhi ya mbavu zake.
Habari zaidi zinadai kuwa, Aguero anaweza kuwa nje kwa wiki sita hadi nane kutokana na majeraha hayo huku pia akitazamiwa kukosa mechi mbili muhimu za Argentina za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Peru itakayochezwa Oktoba 5 na ile dhidi ya Ecuador itakayochezwa Oktoba 10.
Klabu yake ya zamani ya Independiente ya Argentina ambayo ilimuuza Aguero kwenda Atletico Madrid Mei 2006 kwa dau la Euro 23 milioni ilikuwa ya kwanza kumtakia afya njema staa wao huyo wa zamani wakiandika: “Tunakutakia nguvu na upone haraka. Independiente yote ipo na wewe katika wakati huu mgumu.”
Aguero pia amekuwa akitoka kimapenzi na mwanamuziki maarufu wa Argentina, Karina Tejeda ambaye alikutana naye baada ya kuachana na mtoto wa staa wa zamani wa soka wa Argentina, Diego Maradona, Gianina Maradona ambaye amezaa naye mtoto mmoja, Benjamin Aguero.

Hilo ni pigo la pili kwa Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ambaye juzi ilithibitika kuwa huenda akamkosa beki wake wa kushoto, Benjamin Mendy kwa msimu mzima baada ya kuumia vibaya goti lake katika pambano dhidi ya Crystal Palace wikiendi iliyopita.

Timu ya madaktari wa Manchester City ilikuwa ina matumaini kwamba huenda staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa alikuwa ameumia kidogo na angeweza kwenda Barcelona kwa ajili ya kukutana na mtaalamu wa goti, Dr Ramon Cugat.
Hata hivyo, vipimo vimeonyesha aliumia vibaya sehemu ya ndani ya goti na Alhamisi alitazamiwa kufanyiwa upasuaji na ingawa City haijasema atakuwa nje kwa muda gani lakini kwa aina ya majeraha yake anatazamiwa kuwa nje hadi miezi tisa.
Mendy alidhani angerudi uwanjani mapema baada ya kuandika katika mtandao wake wa Twitter akisema :“Habari mbaya jamani. Nitajiunga kwa mkopo katika klabu ya majeruhi kwa miezi kadhaa lakini natazamiwa kurudi haraka nikiwa imara.”

Kocha wa City, Pep Guardiola alisema mara baada ya pambano la Jumanne dhidi ya Shakhtar Donetsk ambalo walishinda akiweka wazi hofu yake kwamba Mendy alikuwa ameumia zaidi kuliko alivyofikiria awali.

Kuumia kwa Mendy kunamuacha Guardiola akiwa na beki halisi wa upande wa kushoto huku akitoa ishara huenda akaingia sokoni kwa ajili ya kununua beki mwingine wa upande wa kushoto.

Post a Comment

 
Top