LONDON, ENGLAND
ANTONIO CONTE (pichani chini) amekiri kwamba Chelsea
ni timu kubwa kwenye magazeti baada ya kuishuhudia Arsenal ikiitafuna Chelsea 3-0
uwanjani Emirates Jumamosi.Mabao ya kipindi cha kwanza ya Alexis Sanchez, Theo Walcott na Mesut Ozil yaliipa Arsenal ushindi wa kwanza katika Premier League dhidi ya wapinzani wao hao wa London tangu Oktoba 2011, huku Chelsea ikishindwa kupiga shuti hata moja lililolenga goli hadi dakika ya 82.
Baada ya vipigo kutoka kwa Liverpool na Arsenal, Chelsea inashika nafasi ya nane.
Na baada ya mchezo dhidi ya Arsenal, Conte alikubali kwamba wachezaji wake wamepoteza heshima yao uwanjani.
"Nini kimetokea? Nilifikiria tangu dakika ya kwanza kwamba hatukuwa na mtazamo sahihi. Nadhani tumecheza vibaya dhidi ya timu ngumu, iliyojipanga, iliyojiandaa kiakili na kimwili.
"Nafikiria kwamba baada ya leo tunapaswa kufikiria kufanya kazi sana, kwa sababu sasa sisi ni timu kubwa kwenye karatasi."
Sanchez akimpita Cahill.
Arsenal ilipewa bao la zawadi katika
dakika ya 11 pale Sanchez alipouwahi mpira mfupi wa beki Gary Cahill kabla ya
kukimbia kwenye lango la Chelsea na kumchambua kipa Thibaut Courtois. Lakini Conte alipozungumza baada ya mchezo huo aliponda kiwango cha timu nzima na wala hakutaka kumuonyesha kidole mchezaji mmoja.
"Sitaki kuzungumza kuhusu makosa kwa sababu siyo sawa kwa wachezaji," alisema.
Conte amekataa kumlaumu Cahill.
"Tunashinda kama timu,
tunapoteza kama timu. Tunajua tunapaswa kufanya kazi kubwa na kama kuna mtu
anafikiri hii timu iko tayari kwa ushindani, nadhani tunapaswa kusubiri na
kufanya kazi zaidi na kurudi kuwa timu kubwa sio kwenye karatasi bali uwanjani."Alipoulizwa kufeli kwa Eden Hazard na Diego Costa katika mchezo huo, Conte aliongeza: "Nadhani kila siku ni tatizo la timu, sio la mchezaji binafsi.
"Kama timu itajituma, wachezaji watacheza vizuri. Kama haitajituma, itakuwa vigumu kwa wachezaji binafsi kucheza vizuri."
Post a Comment