0


LONDON, ENGLAND
ALEXIS SANCHEZ (pichani juu) amesema ana uwezo sawa na wachezaji wawili bora wa dunia, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wakati akiwa katika majukumu ya kimataifa ya kuitumikia Chile.
Tangu ajiunge na Arsenal akitokea Barcelona kwa dili la uhamisho la  Pauni 31.7 milioni, fowadi huyo amefunga mabao 43 na kutoa asisti 25 katika michezo 96, ajijengea  jina na kuwa nyota wa Emirates. 
Sanchez alitoa kauli hiyo alipokuwa katika mahojiano baada ya Chile kukatisha tamaa na kutoka sare bila ya kufungana dhidi ya Bolivia.
“Nimefikia kiwango ambacho ninaweza kushindana na wachezaji wakubwa,” alisema Sanchez. “Sijisikii kumhofia mtu yeyote.”
“Najifananisha (kiwango changu) na Messi na Ronaldo. Nina uwezo sawa kama wao.”
Mastaa Messi na Ronaldo wamekuwa wakibadilishana tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia ya Ballon D'or tangu mwaka 2008. 
Katika Ligi ya La Liga msimu wa 2015-16, Messi na Ronaldo walichangia mabao mara mbili zaidi ya yale ambayo Sanchez aliyafunga katika Premier League. 
Messi alifunga au kuchangia 1.39 katika kila dakika 90 na Ronaldo alichangia 1.3, wakati Sanchez alichangia wastani wa 0.63.

Maneno hayo ya Sanchez yanaweza kuwashangaza baadhi ya watu baada ya raia huyo wa Chile kushindwa kuwamo katika timu ya Wachezaji Bora wa Kulipwa (PFA) katika Premier League msimu uliopita, ingawaje alijumuishwa mwaka mmoja nyuma.
Akiwa amebakisha miaka miwili katika mkataba wake, mashabiki wa Arsenal wanatarajia klabu yao itaingia naye katika majadiliano ya kuongeza mkataba mpya haraka. 
Habari za ndani ya Arsenal, zinadai Sanchez anahitaji kupewa mkataba wenye maslahi sawa kama wa Mesut Ozil, ambaye pia mkataba wake unaisha 2018.

Post a Comment

 
Top