0




MANCHESTER, ENGLAND
JOSE MOURINHO  wa Manchester United, anafikiria kumpanga kinda Marcus Rashford kwa mara ya kwanza katika pambano linalosubiriwa kwa hamu duniani kote, lakini bado haijafahamika kama ameamua hivyo.
Rashford mwenye umri wa miaka 18 tu, Jumanne usiku aliongeza presha kubwa kwa Mourinho baada ya kufunga ‘hat trick’ katika pambano la U-21 kati ya England dhidi ya Norway na kumekuwa na kelele za kumtaka aanzishwe katika pambano dhidi ya Man City.
Kabla ya hapo, Rashford alikuwa ameiokoa United katika pambano dhidi ya Hull City akifunga bao la ushindi katika dakika za majeruhi na kuifanya United izoe pointi zote tisa katika michezo mitatu ya awali Ligi Kuu ya England.
Kinda huyo amekuwa akifunga kila anapopewa nafasi katika mechi zake za kwanza baada ya kufunga katika pambano lake la kwanza tu la Manchester United ambalo pia lilikuwa pambano lake la kwanza la michuano ya Europa dhidi ya Midtjylland Februari mwaka huu.

Mourinho
Akafunga tena siku tatu zilizofuata katika pambano lake la kwanza la Ligi Kuu ya England dhidi ya Arsenal katika ushindi wa mabao 3-2 na hivyo kumfanya awe mfungaji mwenye umri mdogo zaidi kwa Manchester United katika historia ya Ligi Kuu ya England baada ya  Federico Macheda na Danny Welbeck.
Kama vile haitoshi, Rashford alifunga bao lake la kwanza katika siku yake ya kwanza kuvaa jezi ya timu ya wakubwa ya England katika pambano dhidi ya Australia Mei mwaka huu kiasi kwamba kocha wa England wa wakati huo, Roy Hodgson aliamua kwenda naye katika michuano ya Euro iliyofanyika Ufaransa.
Msimu huu, Rashford amecheza dakika 18 tu katika utawala wa Mourinho kutokana na nafasi yake kujazwa na mastaa waliojaa klabuni hapo eneo la ushambuliaji, Zlatan Ibrahimovic, Wayne Rooney na Anthony Martial.

Ibrahimovic
Hata hivyo, mashabiki wa United wameanza kumpa presha Mourinho ampange kinda huyo ambaye mwenyewe amedai kwamba mabao yake yatamsaidia kumpa presha Mourinho kuhusu suala la kumpanga  au vinginevyo.
“Hicho ndicho ambacho anachopaswa kufanya mchezaji mdogo, unampa kocha maamuzi ya kufikiria akupange au vinginevyo. Nasubiri kwa hamu kucheza,” alisema Rashford akizungumzia mechi dhidi ya City.
Sio Mourinho tu, Rashford amemuweka katika presha kubwa kocha mpya wa timu ya taifa ya England, Sam Allardayce ambaye alimtupa nje kinda huyo katika kikosi chake cha timu ya wakubwa ambacho kilicheza mechi ya kufuzu dhidi ya Slovakia ugenini na kushinda bao moja kwa shida katika dakika za majeruhi.

              Kocha wa England-Sam-Allardyce.
Kocha wa kikosi cha England U-21 amedai kwamba hakushangazwa na kiwango cha Rashford na anaamini kuwa Allardyce atakuwa amemuelewa kinda huyo mzaliwa wa Jiji la Manchester kufuatia hat trick yake hiyo.
“Haikunishangaza kabisa. Kitu ambacho tulikiona kwake kwa wiki nzima ndicho tulichokina. Nisingeweza kuwa na furaha zaidi kuliko kile ambacho alikionyesha. Nitaongea na Sam siku chache zijazo na nina uhakika kiwango cha Rashford kimemfanya ajifikirie upya,” alisema kocha huyo baada ya kumalizika kwa pambano dhidi ya Norway.

Post a Comment

 
Top