0


MANCHESTER, ENGLAND
KOCHA Louis van Gaal amekiri kufanya makosa makubwa kwa kuwaondoa washambuliaji wake akiwemo Javier Hernandez ‘Chicharito’ katika kikosi cha Manchester United wakati wa dirisha lililopita la usajili.
Mdachi huyo aliwafungulia milango wa kutokea washambuliaji watano, akiwamo fowadi huyo wa Mexico, ambaye amekuwa moto kweli tangu alipotua kwenye Bundesliga na kwamba anamuumbua.
Chicharito ambaye jina lake jingine la utani ni Little Pea alijiunga na Bayer Leverkusen kwa ada ya Pauni 7.3 milioni.
Mshambuliaji huyo amefunga mabao 19 katika mechi 22, ikiwa ni mabao mengi kuliko waliofunga washambuliaji wote wa Man United, Wayne Rooney, Anthony Martial na Memphis Depay kwa msimu huu.

Mbaya zaidi, Chicharito ambaye alisema aliambiwa na Van Gaal kwamba ana asilimia moja tu ya kupata namba kama atabaki Old Trafford, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi kwenye Bundesliga kwa mara ya pili mfululizo.
Kwa rekodi hizo, Van Gaal amekiri kufanya makosa kwa kumwaachia mshambuliaji huyo kuondoka kwenye kikosi chake.
Mdachi huyo aliwaacha pia Robin van Persie, Radamel Falcao, Adnan Januzaj na James Wilson na kuifanya Man United kukosa makali kabisa kwenye fowadi yake.
Kikosi hicho cha Old Trafford kimefunga mabao 24 tu katika mechi  20 ilizocheza kwenye Ligi Kuu msimu huu, mabao sita katika mechi saba za hivi karibuni.
Lakini, Van Gaal alisema kwamba hakutaka kuwapo kwa ushindani wa namba katika kikosi chake na ndiyo maana aliamua kuwapunguza baadhi ya wachezaji na kuwaacha wengine.

Van Gaal alipoulizwa kama alifanya makosa kwa kumwaacha Chicharito, alisema: “Pengine unaweza kuona ukweli kwenye hilo, lakini usingeweza kulifikiria hapo kabla. Unaweza kuwaaacha washambuliaji wote kwenye timu, lakini matokeo yake kungekuwa na mafowadi wengi. Ikiwa hivyo hawatakuwa na furaha na watalazimisha kuondoka.
“Kwa mfano wa hadithi ya Hernandez, alitaka kucheza. Mimi siamini ushindani, naamini kujiamini na kuaminika. Pengine hilo ni kosa, lakini nimekuwa nikifanya hivyo katika maisha yangu yote ya ukocha. Napenda kuwaamini wachezaji.”

Post a Comment

 
Top